ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumanne, 5 Aprili 2016

CUF tutadai haki kwa amani


CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesisitiza kuwa kitaendelea na juhudi za kutafuta haki yake kwa njia yoyote, lakini ya amani ambayo itaungwa mkono na wananchi wa Zanzibar na kwa kuanzia wametangaza kutoitambua Serikali itakayoundwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad aliwataka wananchi na wafuasi wa chama hicho kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho alisema CUF ipo katika juhudi za kutafuta haki wanayodai ilitokana na kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Maalim Seif alisema hayupo tayari kukaa meza moja na Dk Shein kwa ajili ya kutafuta suluhu ya Zanzibar.
“Sipo tayari kukutana na Shein Ikulu kwa ajili ya mazungumzo ya kuleta amani na utulivu Zanzibar...... nitakutana na yeye kama nani kwa sababu sisi CUF hatutambui ushindi wa Shein katika uchaguzi wa marudio pamoja na serikali yake,” alisema Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Aidha, Baraza Kuu la CUF limepitisha maazimio ya kuunga mkono uamuzi wa Marekani kuinyima Tanzania msaada kupitia Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) hivi karibuni.
Kwa upande wake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa juhudi zake ikiwemo kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi zake za kuleta maendeleo kwa wananchi wake na miradi ya maendeleo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Serikali ya Watu wa China ni miongoni mwa nchi marafiki makubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya nchi mbili kuwa Jamhuri viongozi wake walikuwa marafiki wakubwa wakitembeleana na kubadilisha wataalamu.

Hakuna maoni: