Kambi ya Upinzani bungeni jana imesusia kuwasilisha na kujadili hotuba
ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, huku
kiongozi wake, Freeman Mbowe akitoka nje ya ukumbi huo, akitaja kasoro
tatu zilizosababisha wachukue uamuzi huo.
Staili ya kususia
kujadili hotuba hiyo ya bajeti ni mpya kwa kambi hiyo ya upinzani baada
ya kutumia njia ya kutoka nje ya ukumbi wakati wa vikao vya Bunge la
Katiba na baadaye kutumia njia ya kupiga kelele kukwamisha shughuli za
chombo hicho wakati wa Bunge la Kumi.
Jana, Mbowe aliwaambia
waandishi nje ya ukumbi kuwa kasoro zilizofanya wachukue uamuzi huo ni
kukiuka masuala ya kisheria katika utekelezaji wa bajeti, kutotangaza
kwenye Gazeti la Serikali mabadiliko ya wizara na kutorushwa kwa vipindi
vya Bunge kwenye televisheni.
Mbowe, ambaye alikuwa akitarajiwa
kusoma bajeti ya upinzani kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu, aliibuka na hoja
hizo tatu kabla ya kuamua kutoka nje.
“Bajeti inakuwapo kwa
sababu ni hitaji la kisheria. Inapokuwa Serikali inataka kupitisha
bajeti, lakini haiheshimu bajeti hakuna sababu ya wabunge kukaa hapa
kujadiliana, kutoa povu, kupitisha vifungu vya Katiba, halafu yenyewe
haitekelezi wajibu wake kisheria,” alisema Mbowe nje ya ukumbi wa Bunge.
Alisema Serikali imekuwa ikikiuka sheria ya utekelezaji wa
majukumu ya mawaziri inayomtaka Rais kutengeneza mwongozo wa muundo wa
utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake, ikiwa ni pamoja na kutangaza
katika gazeti la Serikali mabadiliko ya wizara zake.
Alisema
“Tulichelewa kuunda (Baraza Kivuli la Mawaziri) kwa sababu tulikosa
instrument (nyaraka rasmi). Tukalazimika kuunda hivyohivyo. Sasa
tumefika kwenye (Bunge bado Serikali haijaundwa officially (rasmi),
kisheria. Haijawa gazetted (haijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali),”
alisema Mbowe.
“Mpaka leo Serikali hii inafanya kazi kwa kutumia
instrument iliyosainiwa na Rais (wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya)
Kikwete mwezi wa 12 mwaka 2010.
“Na wizara kuu kwa mujibu wa
instrument ya mwaka 2010 ilikuwa ni Wizara ya Waziri Mkuu Tamisemi. Na
Tamisemi ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo baada ya
uchaguzi wa 2010, Tamisemi imerudishwa Ofisi ya Rais, haiku tena Ofisi
ya Waziri Mkuu. Lakini haijawa gazetted.”
Alitaja hoja nyingine
kuwa ni uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi kuhusiana na bajeti
unaofanywa na Serikali pamoja na kuminya uhuru na madaraka ya mhimili wa
Bunge kwa kuzuia matangazo ya wasusia Bunge kurushwa moja kwa moja na
vituo vya televisheni.
“Hatutashiriki mjadala tunaendelea
kutafakari hatua nyingine za kuchukua kama Serikali na Bunge
hawatatafuta ufumbuzi wa masuala hayo matatu,” alisema Mbowe.
Mbowe
aliingia ukumbini saa 9:56 alasiri akiongozana na mbunge wa Momba,
David Silinde na alikwenda kusalimiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG) George Masaju na Waziri wa Kilimo, Mwigulu Nchemba.
Mara
baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge, Mbowe
alieleza sheria ya utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ambapo alidai
kifungu cha 5(1) kinaweka masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu yake.
Alisema
mpaka sasa Serikali inafanya kazi bila kuwa na mwongozo wa utendaji kwa
wizara mbalimbali hivyo kazi nyingi za Serikali zinafanywa kwa kauli ya
Rais.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo mpaka sasa mwongozo wa
utendaji wa Serikali kwa kila wizara unaotumika ni uliochapishwa kwenye
Gazeti la Serikali Namba 494 A la Desemba 17, 2010 ambao pia umetoa
majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kiongozi huyo alinukuu baadhi ya
majukumu katika mwongozo huo kuwa ni kuratibu shughuli za Serikali,
kiongozi wa Serikali ndani ya Bunge, kiungo kati ya Bunge na Serikali,
shughuli za kisiasa na serikali na kuratibu sherehe na misaada
mbalimbali.
“Kazi nyingine ni kusaidia urahisishaji wa mipango
ya serikali katika kuhamishia makao makuu Dodoma, uwekezaji, uchumi,
sekta binafsi na kusaidia maendeleo katika sekta za ndani,” alisema
Mbowe.
Alisema Rais John Magufuli alifanya mabadiliko ya kuziunganisha wizara bila kubadili muongozo wa kisheria.
“Kitendo
cha Serikali hii kuendesha kazi zake kwa mwongozo wa 2010 kina maana
kwamba majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu bado ni yale yale ya mwaka 2010
kwa sababu gazeti hilo halijafutwa,” alisema.
Alifafanua kuwa
jambo hilo ni uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi kuhusu bajeti
unaofanywa na serikali na kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (b) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge limepewa mamlaka ya kujadili
utekelezaji wa kila wizara na kuidhinisha bajeti ya Serikali.
Mbowe
alisema ikiwa fedha zilizoidhinishwa na bunge hazikutosha kutekeleza
majukumu, kifungu cha 41 (1) cha Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015
kinaelekeza kuwa serikali itawasilisha bungeni maombi ya idhini, bajeti
ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango.
Alituhumu
kuwa kumekuwa na uvunjwaji wa kifungu hicho na kutolea mfano bajeti ya
Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka wa 2015/16 ilikuwa Sh 883.8
bilioni ambazo kati ya hizo, fedha za ndani zilikuwa Sh191.6 bilioni.
“Jambo la kushangaza ni kwamba hadi kufikia mwezi Machi 2016 Wizara
ilikuwa imeshapokea kutoka hazina Sh607.4 bilioni ikiwa ni fedha za
ndani, kitendo kinachoonyesha kuwa na ongezeko kubwa la fedha za ndani,”
alisema.
Alitaja kuwa tangu kuidhinishwa kwa bajeti ya Wizara
ya Ujenzi, hakuna bajeti ya nyongeza iliyopelekwa bungeni na Serikali
kwa ajili ya kupata idhini kutokana na matakwa ya Sheria ya Bajeti ya
mwaka 2015 au sheria ya fedha ya 2015.
“Kitendo cha Serikali kuamua
kuhamisha kiasi cha fedha ya bajeti bila ya kupata idhini ya Bunge ni
dharau kwa bunge lakini mbaya zaidi ni uvunjwaji wa Katiba na sheria.”
alisema.
Nje ya ukumbi wa Bunge alisema:”Ukiwauliza wanapata wapi hizi
fedha, wanasema ni maelekezo ya Rais kwamba fedha ziondolewe kwenye
fungu hili, zipelekwe wizara hii.”
Vipindi vya Bunge
Kadhalika,
Mbowe alisema uamuzi wa Serikali kuminya uhuru na madaraka ya Bunge
umewapora wananchi haki yao ya kupata habari kwa kuzuia mijadala bungeni
kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari.
Alisema jambo hilo
ni uvunjwaji wa Ibara ya 18 ya Katiba inayotoa uhuru kwa kila mtu kutoa
maoni na kueleza fikra zake, kutafuta, kupokea na kutoa habari.
“Bunge
ndipo mahali ambapo wananchi wanahoji na kuiwajibisha Serikali na
wanajadili hoja za maendeleo kupitia wabunge wao waliowachagua, hivyo
huwafuatilia kupitia kwenye luninga zao pia ubadhirifu wa miradi mingi
uibuliwa huko,” alisema.
Alisema wapinzani wataendelea kutafakari kwa kina na makini hatua za kufuata na kisha akawasilisha.
“Kwa
mazingira kama hayo, kambi rasmi ya upinzani bungeni haiko tayari
kuendelea kushiriki katika uvunjaji Katiba, sheria na haki za msingi za
wananchi,” alisema.
“Kambi rasmi haitakuwa tayari kuwasilisha
hotuba yake katika mazingira haya na inaushauri uongozi wa Bunge
kutafuta ufumbuzi wa haraka wa kadhia hii ili kurejesha heshima ya Bunge
na haki za msingi.”
Baadaye, Chenge aliipinga kauli ya Mbowe
kuwa Katiba imevunjwa na kusema alitumia maneno mazito na badala yake
alimtaka atumie maneno kuwa Katiba ilitaka kuvunjwa.
Chenge
aliitaka kambi ya upinzani kufuata taratibu kama wanaona kuwa wameonewa,
badala ya kutumia maneno hayo na pia akata watafakari kama wangependa
kuendelea na mjadala.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani
walionyesha kususia kwani hata walipoitwa na mwenyekiti hawakuchangia
licha ya kuwapo ndani ya ukumbi wa Bunge.
Kauli ya Mbowe kwa
wanahabari
Akizungumza na wanahabari Mbowe alisema uamuzi huo haujakiuka
sheria kwa sababu Bunge liko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kwamba
hawawezi kwenda mahakamani ili kupata tafsiri kuhusu suala hilo kwa
sababu shughuli za Bunge zinatatuliwa na Bunge lenyewe si mahakama.
“Rais
kama kiongozi wa nchi ana mamlaka ya kulisemea hili, atueleze kama ni
yeye ndiye aliyeruhusu Bunge lisirushwe moja kwa moja. Awali walisema
TBC hawatarusha ila kwa sasa vyombo vyote vimezuiwa,” alisema.
“Hivi
sasa luninga zilizopo ndani ya Bunge zilizokuwa zikionyesha matangazo
nazo hazionyeshi kinachoendelea. Sasa watumishi wa Bunge watafuatilia
nini?” alihoji Mbowe.
Kauli ya AG
Alipoulizwa kuhusu suala
hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema: “Nitashukuru
kama mtavuta subira majibu ya Serikali yatatolewa wakati wa kufanya
majumuisho.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni