Hatua hiyo imekuja baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania kufaulu katika majaribio yake aliyokuwa anafanya katika klabu ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Hispania, Deportivo Tenerife.
Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi wa Azam FC, Yussuf Bakhresa akisema klabu hiyo sasa inatarajiwa kuingia katika mazungumzo na Azam juu ya kumnunua moja kwa moja mchezaji huyo, badala ya kumtwaa kwa mkopo kama walivyokuwa Wahispania hao.
Mtandao wa binzubeiry.co.tz, umemnukuu Bakhresa akisema; “Tunatarajia kuanza mazungumzo nao juu ya suala la Farid, ingawa wazo lao la awali ni kumchukua kwa mkopo wa miaka miwili. Sasa tunasubiri ofa yao rasmi, kisha Bodi ya Ukurugenzi itajadili na kutoa maamuzi.”
Naye Farid ameelezea kufurahia matokeo ya majaribio yake, akisema haikuwa kazi nyepesi kwake kuweza kuwaridhisha maofisa wa benchi la ufundi la Tenerife.
“Kwa kweli nimefurahi sana na ninamshukuru Mungu kwa kufuzu majaribio, ila haikuwa kazi nyepesi, mpira wa Ulaya mgumu,” alisema.
Awali, Farid ilikuwa apelekwe moja ya klabu za Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama La Liga, kati ya Las Palmas na Athletic ya Bilbao kwa majaribio, lakini wakala wake akashauri mchezaji huyo aanzie timu ya Daraja la Kwanza Hispania ili kupata nafasi ya kucheza na kuinuka haraka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni