Yanga ambayo mwishoni mwa wiki ilisherehekea kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara 26, ikiwa ni rekodi kwa klabu za Tanzania, iliondoka nchini jana mapema asubuhi.
Akizungumza na gazeti hili juzi kabla ya kuondoka nchini, Pluijm alisema anatambua ugumu wa mechi hiyo hasa kwa vile watacheza ugenini, lakini akaahidi ushindi ni lazima.
“Tunakwenda kucheza ugenini mechi itakuwa ngumu kwa vile wenzetu wanacheza kwao, lakini nafurahi kitu kimoja kwamba wachezaji wangu wanakwenda wakijiamini zaidi kutokana na kutwaa ubingwa, sidhani kama watakubali kufungwa kirahisi, bado wana morali ingawa najua wanaweza kuja na mbinu mpya, lakini hata sisi tumejiandaa,” alisema.
Yanga inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa mbele kwa mabao 2-0 iliyoyapata katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuhitaji ushindi au sare ya aina yoyote kuweza kuandika historia ya kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo inayokwenda sambamba na utajiri mkubwa wa fedha, kwani ukiachilia mbali kitita cha dola za Marekani 150,000 kwa kila timu itakayofuzu hatua hiyo, timu zitaogelea fedha ikiwa ni pamoja na bingwa kutwaa dola 625,000 (Sh bilioni 1.36), wakati mshindi wa pili atapata dola 432,000 (Sh milioni 907).
Mbali ya morali ya ushindi katika mchezo wa kwanza, Yanga inakwenda ikiwa na nguvu ya ziada ya nyota wake wawili, mshambuliaji Donald Ngoma na kiungo Thabani Kamusoko ambao walioukosa mchezo wa kwanza kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni