ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumanne, 10 Mei 2016

Wabunge wanawake walaani kejeli dhidi yao

Imeandikwa na Maulid Ahmed, Dodoma.
UMOJA wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) umelaani na kueleza kutokubaliana na tabia ya baadhi ya wabunge ya kutumia lugha za matusi, kejeli, dharau na udhalilishaji wa wabunge wanawake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa wamepata nafasi hiyo kwa njia ya mapenzi.
Mwenyekiti wa TWPG, Margaret Sitta alibainisha hayo wakati akiwasilisha maelezo binafsi bungeni jana, akisema lengo la kutoa maelezo hayo ni kuhitimisha mjadala wa kauli hiyo dhidi ya wabunge wanawake wa Chadema uliotokea Mei 5, mwaka huu na kusababisha wabunge hao kutoka nje ya Bunge na kutishia kujitoa TWPG.
Kauli ya kuwadhalilisha wabunge hao wa Chadema ilitolewa bungeni na Mbunge wa Ulanga mkoani Morogoro, Goodluck Mlinga (CCM) ambaye alisema wabunge hao wanawake wamekuwa wakipata nafasi hiyo hadi wawe ‘baby’ (wapenzi) wa wanaume ndani ya chama hicho.
Sambamba na hilo, alisema wabunge wa ndani ya chama hicho wamo pia wenye uhusiano wa jinsia moja. Hata hivyo, hakuwataja kwa majina wabunge hao. “Chadema kuna wanachama wengi wa kike, iweje ichukue wa CCM.
Chadema ndiyo inakandamiza demokrasia, Tundu Lissu anajua sheria lakini ndani ya Chadema kuna wapenzi wa jinsia moja”. Hata hivyo, kauli hiyo ilifutwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na baadaye Mlinga aliifuta, lakini wabunge wa Chadema hawakukubaliana na kuonesha kukerwa sana.
Jana, Sitta alisema licha ya kauli hizo kufutwa, inasisitiza kuwa inalaani tabia hiyo dhidi ya wanawake inayofanywa ndani na nje ya Bunge na kushauri wabunge wote kuzingatia kanuni zote za Bunge hasa kanuni ya 64(1)(f) na (g) inayokataza lugha ya matusi na ya kuudhi dhidi ya mbunge mwingine.
“TWPG inashauri mara inapotokea mbunge amekiuka kanuni hizi, kiti kichukue hatua za haraka kudhibiti hali hiyo…Tunashauri wabunge wote kuheshimiana ili kulinda hadhi ya Bunge letu na tuwe mfano wa kuigwa katika jamii yetu, tukio hili liwe la mwisho na wakati huohuo liwe fursa kwetu wanawake na kuimarisha umoja wetu, kamwe tusikubali kugawanywa,” alisema.

Hakuna maoni: