ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 6 Mei 2016

Atuhumiwa kumuua mkewe na mtoto kwa wivu wa mapenzi

POLISI mkoani Pwani inamshikilia Frowin Mbwale (26) mkazi wa Kawe jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuwaua kwa kuwachinja; mkewe Oliver Erasto (23) na mtoto wake, Emmanuel (3) kutokana na kilichodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi, alisema mauaji hayo yalifanyika juzi saa 10.30 jioni eneo la Zinga katika kata ya Dunda , tarafa ya Mwambao wilayani Bagamoyo.
Mushongi alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida juzi siku ya tukio mtuhumiwa akiwa na mwenzake aliyejulikana kwa jina la Rajabu Juma (20) mkazi wa Makongo jijini Dar es Salaam waliwaua watu hao kwenye vichaka vilivyopo kwenye eneo hilo la Kaole.
Juma pia anashikiliwa na Polisi. “Muda huo mtuhumiwa akiwa na mwenzake alimhadaa mke wake kuwa waende kwenye nyumba yao ambayo inaendelea kujengwa kwa lengo la kuitazama ambapo mke wake alikubali na kumbeba na mtoto wao na kwenda huko ambako aliwachinja shingoni,” alisema Kamanda Mushongi.
Alisema mtuhumiwa kumbe lengo lake halikuwa kuangalia ujenzi wa nyumba yao huko Kaole bali alikuwa na lengo lingine la kufanya unyama huo ambao aliutekeleza akiwa na rafiki yake huyo ambaye walishirikiana kumchinja mke na mtoto wake.
“Chanzo cha mauaji hayo ni mtuhumiwa huyo alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa ana uhusiano na mwanamume mwingine aitwaye Hamza mkazi wa Kawe jijini Dar es Salaam na kusababisha mauaji hayo ya kusikitisha ambayo yamewaumiza watu wengi,” alisema Mushongi.
Alibainisha kuwa miili ya marehemu hao ilikutwa ikiwa imechinjwa na watu hao umbali wa mita 100 kutoka barabara ya magari itokayo Kaole kwenda eneo la Mbegani. Alisema watuhumiwa hao walikamatwa saa 3.30 usiku baada ya wananchi Zinga kuwatilia shaka walipokuwa wakijaribu kutaka kutoroka na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika. Miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kusubiri ndugu kwa ajili ya maziko.

Hakuna maoni: