ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 26 Mei 2016

Vigogo wa TCU watumbuliwa

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
RAIS John Magufuli amewasimamisha kazi watendaji wakuu wa Kamisheni ya Tume vya Vyuo Vikuu (TCU). Amechukua hatua hiyo baada ya kubainika inadahili wanafunzi wasio na sifa, wakiwemo wenye ufaulu wa daraja la nne, kujiunga na vyuo vikuu na kuwapatia mikopo.
Pia serikali kupitia kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako imetangaza kufanyika kwa udahili upya vyuo vikuu vyote nchini kuondoa wanafunzi wote wasio na sifa. Aidha, imebainika kuwapo wanafunzi hewa wanaotafuna mikopo ya elimu ya juu, jambo ambalo Dk Ndalichako pia ametangaza vita dhidi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Profesa Ndalichako alisema kwa idhini aliyopewa na rais, amewasimamisha kazi mara moja watendaji hao akiwemo Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya kwa kushindwa kusimamia kazi za tume akiwa mtendaji mkuu wa taasisi.
Wengine ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora, Dk Savius Maronga kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya vyuo vikuu. Mkurugenzi wa Udahili, Rose Kiishweko amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia udahili wa wanafunzi na kusababisha kudahiliwa wanafunzi wasio na sifa. Mtendaji mwingine aliyesimamishwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Kimboka Istambuli.
Walioziba nafasi Waziri Ndalichako alisema ili shughuli za TCU ziendelee, Profesa Eliuter Mwageni ameteuliwa kukaimu nafasi ya katibu mtendaji. Kabla ya uteuzi huo, Profesa Mwageni alikuwa Naibu Makamu Mkuu (Utawala na Fedha) wa Chuo Kikuu cha Ardhi. Aidha Dk Kokubelwa Mollel atakaimu nafasi ya ukurugenzi wa udahili na nyaraka na kabla ya uteuzi wa kukaimu nafasi hiyo, Dk Mollel alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Udahili waliofeli St Joseph Alisema kwa muda mrefu, kumekuwa na taarifa za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St Joseph wanaodahiliwa kutokuwa na sifa. Waziri alisema baada ya ukaguzi kufanyika katika chuo hicho katika Kampasi za Arusha na Songea, kulionekana upungufu mkubwa katika utoaji elimu.
Wanafunzi 489 walibainika kutokuwa na sifa za kusoma chuo kikuu, kwani walikuwa ni wa kidato cha nne waliofaulu daraja la nne huku wengine wakiwa na pointi 32, lakini wakadahiliwa kusomea shahada ya kwanza .
“Mwanafunzi wa kidato cha nne anasoma digrii ya sayansi, mtu kasoma mkondo wa biashara lakini kadahiliwa asomee sayansi na analipiwa mkopo na TCU, si tu hana sifa ya kusoma chuo kikuu, hata cheti cha ualimu hana sifa, hafai hata cheti cha ualimu kupelekwa kwenye digrii,” alisema.
Profesa Ndalichako alisema rais amekuwa akihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu. “Lakini cha kusikitisha, kuna wanafunzi waliofaulu vizuri kidato cha sita wanakosa mikopo, ila wale waliofeli wanaipata mikopo hiyo,” alisema. “Divisheni four (daraja la nne) pointi 34 yuko chuo kikuu, hata ualimu simkubali mtu wa namna hiyo,” alisema.
Alisema baada ya serikali kufunga chuo hicho, wanafunzi hao walihamishiwa vyuo vingine, lakini hata huko walikopelekwa uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo, hali iliyolazimu kuwarudisha madarasa ya nyuma. “Wanafunzi waliotoka St Joseph na kupelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma, uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo, ambapo wanafunzi wa mwaka wa pili na wa kwanza wamerudishwa nyuma muhula mmoja huku wale wa mwaka wa tatu wamerudishwa nyuma mwaka moja,” alisema.
Alisema wanachuo wa St Joseph Kampasi ya Songea waliopelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro, waliokuwa wakisoma mwaka wa nne, wamerudishwa mwaka wa tatu. Aidha, wametengewa muda wa ziada kurekebisha upungufu huo. Alisema pia waliopelekwa vyuo vikuu vingine vya Ruaha na Mkwawa mkoani Iringa, wameonekana kuwa na upungufu pia.
“Kibaya zaidi, hao wanafunzi walikuwa wanapata mikopo, Division four anapata mkopo haki iko wapi? Tulipoona jambo hili si sawa tulichukua hatua tukaieleza bodi ya TCU kusimamisha kazi waliohusika lakini hilo halikufanyika,” alisema.
Alisema kilichoonekana, Mwenyekiti wa TCU, Awadh Mawenya na tume yake, walikataa kuwasimamisha kazi waliohusika. Alisema mwenyekiti wa bodi muda wake uliisha, lakini rais alimuongezea muda mwingine.
“Nimeongea na Rais kaondoa muda alioongezewa mwenyekiti nao unasitishwa,” alisema. Wanafunzi kurejesha fedha Alisema wanafunzi hao 489 ambao walikuwa wanalipiwa na bodi ya mikopo, tayari wameondolewa chuoni na kutakiwa kurejesha fedha walizokopa. “Huo ni mkopo lazima urejeshwe na tumeshatangaza vita kali kwa wanafunzi hewa wanaopata mikopo kutoka elimu ya juu na kazi hiyo imeanza,” alisisitiza.
Wakati huo huo, akijibu maswali bungeni jana, Waziri Ndalichako alisema serikali imejipanga kufanya uhakiki wa viwango vya wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu nchini. Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Mmasi (CCM) aliyetaka kufahamu mkakati wa serikali kupata wanafunzi wenye uwezo, maarifa na tija. Mbunge Mmasi alisema licha ya kuwepo kwa TCU, bado nchi imekuwa ikizalisha wanafunzi wasio na uwezo.
Profesa Ndalichako alisema serikali inajipanga kufanya uhakiki wa vigezo vya kujiunga na vyuo vikuu. Alisema ufafanuzi juu ya hatua hiyo, utatolewa katika hotuba yake ya bajeti itakayosomwa leo.

Hakuna maoni: