ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 6 Mei 2016

Azam FC majanga, Yanga bingwa Jumapili?

Imeandikwa na Vicky Kimaro
KIMAHESABU Yanga tayari ni bingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu wa 2015/2016, labda itokee miujiza ya kupoteza mechi zake zote tatu zilizosalia katika ligi hiyo, huku mahasimu wao Simba wakishinda mechi zote nne walizobakiwa nazo.
Lakini sare au kipigo kimoja tu kwa Simba kitaihakikishia Yanga taji la 26 katika ligi hiyo iliyoingia katika msimu wa 51 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965.
Hii ina maana kwamba, mbio za ubingwa kwa sasa zimebaki kwa Yanga na Simba tu, baada ya jana Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuipoka Azam FC pointi tatu na mabao matatu, hivyo kuirudisha kutoka nafasi ya pili hadi ya tatu ikiwa na pointi 57.
Na hata kama ikishinda mechi tatu zilizosalia, itakuwa na jeuri ya kufikisha pointi 66 ambazo zimeshavukwa na Yanga yenye pointi 68.
Simba ina pointi 58 na ikishinda zote nne itakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 70, lakini wakati huohuo ikiomba Yanga ipoteze mechi zake zote tatu ili ubingwa huo utue Mtaa wa Msimbazi kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2011/2012.
Keshokutwa, Simba itacheza na Mwadui FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hivyo sare au kipigo kitapeleka chereko kwa Yanga, kwani huenda wakatangazwa mabingwa bila hata kugusa mpira katika siku husika.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alithibitisha jana kuwa, Azam imepokonywa pointi tatu na mabao matatu na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kosa la kumchezesha beki wake mahiri Erasto Nyoni akiwa na kadi tatu za njano katika mchezo dhidi ya Mbeya City mjini Mbeya.
“Azam wanatakiwa kutunza kumbukumbu za wachezaji wao, bodi imefikia uamuzi wa kuipokonya pointi tatu Azam FC baada ya kubaini ilimtumia Erasto Nyoni kinyume cha sheria,” alisema Lucas.
Katika mchezo huo, Azam ilishinda 3-0.
Kwa mujibu wa kanuni ya 37 (4) toleo la 2015 ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara juu ya udhibiti wa wachezaji; “mchezaji atakayeonywa kwa kadi tatu za njano katika michezo mitatu, basi atalazimika kukosa mchezo unaofuata wa timu yake.”
Aidha kanuni ya 14 (37) ya kanuni hiyo imempa ushindi wa mabao matatu na magoli matatu timu ya Mbeya City.
Kutokana na adhabu hiyo kwa Azam, ni wazi Yanga sasa imebakiza mechi moja kutwaa ubingwa msimu huu na huenda ikatangaza ufalme Jumanne ijayo mjini Mbeya itakayokwenda kupambana na Mbeya City. Ikishinda, itafikisha pointi 71 ambazo hazitafikiwa na Simba.
Msemaji wa Azam, Jaffari Maganga akizungumzia adhabu hiyo, alisema; “Tumesikia taarifa tu bado hatujapata barua rasmi ya kutujulisha kupokonywa pointi, tutakapoipata tutalizungumzia suala hili.”
Adhabu ya aina hii imewahi kuikumba Simba 2006 na 2007 na pia Yanga mwaka 2012 huku ligi ikielekea ukingoni. Ilivyokuwa; Mwaka 2006 Simba ilinyang’anywa pointi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, baada ya kudaiwa kumchezesha Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Mwaka 2007 Simba ikakutana tena na adha kama hiyo ikiwa imebakiza michezo minne mkononi kwa kupokwa pointi tatu na mabao matatu na ushindi kupewa Azam FC baada ya kumchezesha Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Mwaka 2012 Coastal Union ilinufaika kwa kupewa ushindi wa chee wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha mchezaji Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Machi 31 mwaka huo Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Hakuna maoni: