ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumanne, 10 Mei 2016

Sukari kaa la moto

SUALA la uhaba bandia wa sukari limeendelea kuitikisa nchi, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vikifanya kazi nzuri baada ya kuwatia nguvuni wafanyabiashara wengine, waliohodhi bidhaa hiyo kinyume cha sheria huku ikiwamo kukamata tani 622.4 za mfanyabiashara Haruni Zakaria mkoani Morogoro.
Mwishoni mwa wiki, mfanyabiashara huyo anayemiliki Kampuni ya Al Naeem, alikutwa akiwa ‘ameficha’ tani 4,579.2 za bidhaa hiyo katika maghala yake yaliyoko Tabata, Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wachunguzi wa taasisi hiyo na wa Jeshi la Polisi, walifanya ukachero wao katika maghala ya kampuni hiyo yaliyopo Mbagala na Tabata, Mei 5, mwaka huu.
Lakini siku chache baada ya kunasa sukari hiyo. Kikosi kazi cha Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoa wa Morogoro kilichoundwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk Kebwe Steven Kebwe kufuatilia wafanyabiashara walioficha sukari, kimebaini kiasi cha tani 622.4 za sukari zilizofichwa katika maghala mbalimbali yaliyomo mkoani humo. Dk Kebwe amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ulrich Matei kuweka ulinzi kwenye maghala hayo yaliyokutwa yameficha sukari hiyo na kuhakikisha inauzwa kwa bei elekezi, iliyowekwa na serikali kwa wananchi.
Pia alimwagiza kuwafikisha wafanyabiashara walioficha sukari hiyo mahakamani mara moja na kumsaka mfanyabiashara Sadick Yassin ambaye alifunga duka lake wakati wa ukaguzi na kutokomea kusipojulikana.
Mali ya Zakaria wa Dar
Akizungumza jana, Dk Kebwe alisema sukari hiyo imebainika kuwa ni mali ya mfanyabiashara mmiliki wa Kampuni ya Al Naeem Enterprises na kuhifadhiwa katika maghala mbalimbali ya Kiwanda cha Sukari Kilombero (K1) tani 429, Kiwanda cha Sukari Kilombero (K2) tani 135 na katika Manispaa ya Morogoro tani 58.4, jumla kuwa ni tani 622.4.
“Nimeunda kikosi kazi cha kufuatilia wafanyabiashara walioficha sukari katika maghala yao katika ukaguzi wa awali, jumla ya tani 622.4 za sukari zimebainika kwenye maghala mbalimbali na sukari yote iliyobainika ni mali ya Al-Naeem Enterprises na tayari maghala hayo yenye sukari yapo chini ya ulinzi wa vyombo vya dola,” alisema.
Licha ya kumwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa kuweka ulinzi katika maghala hayo na kusimamia sukari hiyo inauzwa kwa bei elekezi ya serikali, pia alimwagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakiki iwapo sukari hiyo imelipiwa kodi ya serikali.
Dk Kebwe pia aliwataka wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani humo, kutoa taarifa za wafanyabiashara au watu walioficha sukari ili hatua zichukuliwe mara moja dhidi yao. Kabla ya kuweka msimamo wa Serikali ya Mkoa dhidi ya wafanyabiashara dhalimu, Dk Kebwe na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa walifanya ziara ya kushtukiza ya kuhakiki upya maghala ya wafanyabiashara wa maduka ya jumla katika Manispaa ya Morogoro.
Katika ghala la Kampuni ya Sukari Kilombero lililipo mjini Morogoro lilikuwa na tani 58.4 za sukari ambayo ni mali ya Al Naeem Enterprises. Msimamizi wa ghala hilo, Robert Charles alimfahamisha Mkuu wa Mkoa na timu yake kuwa sukari hiyo ipo kwa muda wa mwezi mmoja sasa baada ya kununuliwa na mfanyabiashara huyo kutoka kiwandani Kilombero.
Alisema sukari tani 58.4 iliyokutwa ndani ya ghala hilo ni mali ya mfanyabiashara Zakaria aliyeinunua kutoka kiwandani Kilombero na kuihifadhi hapo akisubiri kusafirishwa na kuwauzia wanunuzi wa jumla. Baadhi ya wauzaji wa maduka ya jumla waliokaguliwa na timu ya Mkuu wa Mkoa, Thabit Islam na Hassan Binzoo walisema hali ya upatikanaji wa sukari katika kipindi hiki ni mgumu kutokana na kuadimika ghafla.
Dar yanaswa nyingine
Katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, zimekamatwa tani 2,700 za sukari zikiwa zimefichwa katika ghala moja eneo la Mbagala. Akitoa taarifa hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam jana, Paul Makonda, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Photidas Kagimbo alisema sukari hiyo imekamatwa baada ya Rais kutoa agizo la kuwabaini wale wote walioficha sukari na kusababisha wananchi kuteseka kupata bidhaa hiyo.
Kagimbo alisema licha ya kukamatwa kwa sukari hiyo Manispaa hiyo bado inaendelea na msako ili kuwabaini na wafanyabiashara wengine waliohodhi bidhaa hiyo.
Msako mkali Kahama
Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Polisi imefanya upekuzi katika baadhi ya maghala ya kuhifadhia sukari na kuwabaini baadhi ya wafanyabiashara wanne wanaojihusisha na kazi hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Michael Nyange alisema wamefanya ukaguzi katika maghala ya wafanyabiashara wakubwa wa sukari, ambayo ni ya wafanyabiashara John Hango (walikuta mifuko miwili ya kilo 50), Nyorobi Kisabu (hakuna kilichokutwa), Mshaka Kaziro (hakuna kilichopatikana) na Alex Magina (mifuko 40, yenye kilo 50 kila mfuko). Alisema kazi hiyo itakuwa endelevu.
RC Dodoma aagiza iuzwe
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ameagiza tani 154 kuuzwa kwa wananchi kwa bei elekezi, huku akiwataka wafanyabiashara ambao bado wameficha sukari kuitoa mara moja kabla rungu halijawashukia.
Takukuru kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapa walikamata na kuzifungia tani 154 za sukari katika ghala la mfanyabiashara Haidary Gulamali na sasa Rugimbana ametoa agizo la kufunguliwa kwa ghala hilo ili litoe huduma kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa akiwa amefuatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa alisema wameamua kufungua ghala na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ambao wanauhitaji mkubwa kwa sasa wa sukari.
Lindi yagawiwa kwa shule
Mkoani Lindi, TRA mkoani humo imegawa sukari ya magendo mifuko 5,319 yenye thamani ya Sh 373,521 kwa taasisi mbalimbali za mkoani humo baada ya kuthibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa kubaini kuwa ni salama.
Sukari hiyo ilikamatwa Februari mwaka huu katika bandari ya Lindi ikiingizwa nchini kinyume cha sheria kutoka Brazil kupitia bandari ya Zanzibar, na imegawiwa kwa shule za sekondari, Magereza na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, alisema sukari hiyo ilikamatwa kwa ushirikiano na taasisi nyinginezo.
Taasisi hizo mojawapo ni shule ya Ilulu Sekondari ya Kilwa mifuko 300, Chuo cha Maendeleo Kilwa mifuko 149, shule maalumu Kilwa mifuko 80, Hospitali Kilwa mifuko 50, Mitole Sekondari mifuko 42, Njinjo Sekondari mifuko 73, Nyangao Sekondari mifuko 150, Hospitali ya Nyangao mifuko 150, Lindi Sekondari mifuko 166, Hospitali ya Sokoine mifuko 216, Kambi ya Wazee mifuko 16 Shule ya Sekondari Mahiwa mifuko 210, Shule maalumu ya Nyangao mifuko 44, Veta Lindi 156, Mnolela Sekondari mifuko 57 na Mtama Sekondari mifuko 49.
Kawambwa, Serukamba wanena
Mbunge wa Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa (CCM) amemtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kumuondolea adha Rais John Magufuli ya kugombana na wafanyabiashara wa sukari kwa kusaidia kuanza uzalishaji kwa Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo.
Dk Kawambwa alisema “Ni aibu wananchi wanakuwa na uhaba wa sukari, Rais (Magufuli) anaangaliwaje nchi inapokuwa na uhaba wa sukari, mwondolee aibu hii Rais, serikali isaidie Kiwanda cha Sukari Bagamoyo kianze kazi, kimesubiri mwaka wa 11 sasa…kina uwezo wa kuzalisha tani 150,000 kwa mwaka.”
Dk Kawambwa alitoa maelezo hayo bungeni jana wakati akichangia mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2016/2017. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) aliitaka serikali kuachana na mpango wa kuanzisha viwanda vingi vya kila aina, badala yake ijikite kwenye viwanda vya sukari kwani vina uwezekano wa kuzalishwa tani milioni mbili na kiwanda cha mbolea kuwa na uhakika wa soko kwenye nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Zitto awasilisha hoja mahsusi
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo), jana jioni aliwasilisha hoja ya kuomba mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, uahirishwe ili mawaziri wa Kilimo na Viwanda wakapange mikakati ya kuondoa tatizo la sukari. Alisema mikakati hiyo iwe ni kuongeza uzalishaji miwa pamoja na uzalishaji wa sukari ili miaka mitatu baadaye Tanzania isiwe na tatizo la sukari.
Alitumia Kanuni ya 69 kutaka Bunge liahirishwe. Hata hivyo, hoja iliungwa mkono na wabunge wa upinzani pekee na Waziri William Lukuvi alisimama kwa niaba ya serikali na kusema hoja hiyo haiwezekani kuahirishwa na kumtaka Zitto ashike mshahara wa waziri.
Komu, Kubenea watetea, wabanwa Kwa upande wao, Chadema imeonekana kuwatetea wafanyabiashara wanaoficha sukari na kudai kuwa agizo la Rais Magufuli la kuzuia sukari kutoka nje kuingizwa nchini, ndio sababu ya bidhaa hiyo kupotea sokoni.
Pia chama hicho kimedai kuwa kitendo cha serikali kuwataifisha sukari wafanyabiashara walioficha, kinaharibu mazingira ya biashara nchini, lakini pia kinaweza kusababisha benki kufilisika kwa kuwa wafanyabiashara wengi wamechukua mikopo kwenye benki hizo.
Kutokana na hali hiyo kiliitaka Serikali iwaruhusu wafanyabiashara waendelee kuagiza sukari kutoka nje kwa kuwa kuna uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo tangu Februari, mwaka huu.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu aliyefuatana na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea walijikuta wakikanusha vikali baada ya waandishi wa habari kuwahoji kama wamelipwa fedha na wafanyabiashara ili kuwaunga mkono katika suala hilo la sukari.
Komu ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini alimtupia lawama Rais Magufuli, na kueleza kuwa suluhisho la kudumu ni kuwaruhusu wafanyabiashara hao waendelee kuagiza sukari kutoka nje, kuliko kuendeleza hatua za kuwaadhibu wale walioficha sukari kwenye maghala yao kwa kuwa hilo si suluhisho.
Naye Kubenea aliwataka waandishi hao wakague hata simu zao, kuona kama kuna fedha yoyote iliyoingia kwani lengo lao ni kufikisha ujumbe kwa serikali kuwa wao ndio chanzo cha gharama kupanda kwa bidhaa hiyo.
Kwa upande wake, Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja alisema serikali imekosea kuingilia soko hilo pamoja na kupanga bei elekezi, jambo ambalo alisema limechangia kupanda bei kwa bidhaa hiyo muhimu kwa matumizi ya nyumbani na viwandani.
“Unapozungumzia sukari, ni bidhaa muhimu kwa matumizi ya nyumbani na viwandani, hili sio soko la nchi moja, ni soko linalohusisha nchi nyingi; ambalo likiingiliwa hata kwa kutekenywa kidogo tu kunalifanya soko lenyewe lishtuke na bei inaweza kuongezeka kama ilivyotokea sasa,” alisema Profesa Semboja wakati akizungumzia mfumuko wa bei wa taifa ambao ulitangazwa jana na NBS.
Habari imeandikwa na John Nditi, Moro, Halima Mlacha, Maulid Ahmed na Sifa Lubasi, Dodoma, Raymond Mihayo, Kahama, Kennedy Kisula, Lindi na Sophia Mwambe na Shadrack Sagati, Dar.

Hakuna maoni: