ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 5 Mei 2016

Mabasi 25 yaendayo haraka yagongwa

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko MABASI yaendayo haraka jijini Dar es Salaam yanayoendelea na majaribio katika njia zake, zaidi ya 25 yamegongwa na vyombo vingine vya usafiri vilivyopita katika barabara hizo maalumu, licha ya kuzuiwa.
Aidha, ujenzi wa mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya ukatishaji tiketi imekamilika kwa asilimia 90 na asilimia iliyobaki inatarajiwa kukamilika wiki hii.
Msemaji wa Kampuni inayoendesha mabasi ya haraka ya UDA RT, Sabri Mabruk alisema kati ya ajali hizo ni moja pekee walifanikiwa kuwakamata wahusika na ajali kupimwa.
Wengine walikimbia baada ya kusababisha ajali. Mabruk alisema kumekuwa na mwingiliano wa vyombo mbalimbali vya usafiri kwenye barabara hizo ikiwamo magari, pikipiki na maguta.
Alisema kutokana na ajali hizo wamesababisha kampuni uharibifu wa magari unaowalazimu kufanya marekebisho kabla hata hawajaanza rasmi kutoa huduma. Aliwataka watumiaji wa vyombo vya usafiri kuzingatia sheria za barabarani kuepusha ajali hizo.
“Pia inatakiwa kusaidiana wadau wote kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya barabara hizo, ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wa kukamata wale wanaokiuka sheria wanapoonekana wakipita katika njia hizo,” alisema Mabruk.
Alisema miundombinu ya njia hiyo imejengwa kulingana na mahitaji ya mabasi yaendayo haraka, hivyo haipaswi kutumiwa na chombo kingine cha usafiri wala waendao kwa miguu.
Akizungumzia kuanza rasmi kwa mradi huo, alisema kwa sasa wanasubiri kukamilisha kwa suala la nauli kwa kuwa ujenzi wa mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya ukatishaji tiketi umebaki asilimia 10 kumalizika na wiki hii utakuwa tayari.
Alisema baada ya kutangazwa kwa nauli ndipo wataweza kutengeneza kadi kulingana na nauli hizo hivyo kuanza kwa huduma hizo.

Hakuna maoni: