Imeandikwa na Rahel Pallangyo
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Snura aliyekuwa amefuatana na Meneja wake, Hemed Kavu `HK’ aliomba radhi vyombo vya serikali vinavyosimamia sekta ya sanaa kwa kutofuata sheria, kanuni na taratibu katika uendeshaji wa sanaa nchini.
“Mimi na Meneja wangu tunaahidi kutorudia tena kufanya tukio hilo la udhalilishaji na iwapo tutarudia basi tupewe adhabu kali kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Snura.
Pia aliahidi kuwa mfano na balozi kwa wasanii wenzake na jamii katika kutunza na kufuata maadili na utamaduni wa kitanzania pamoja na sheria za nchi.
Wakati akijibu maswali ya wandishi wa habari juu ya sababu za kutengeneza video hiyo, alijitetea kwa kusema; “Kwa upeo wetu wa kufikiri tuliona tumpeleke chura maeneo yake ambayo ni kwenye maji na walivaa mitandio na miziki mingi watu wanacheza na mitandio. “Tulipoona mitandio imelowa tukaona tuweke yotube kwani huko mtu akiingia atakuwa ametaka mwenyewe na sidhani kama mtoto hawezi kuacha kwenda maktaba na kuingia yotube”, alisema Snura huku meneja wake akijitetea kuwa walirekodi wakati mvua inanyesha.
Snura aliahidi kutekeleza maazimio na maelekezo yaliyotolewa katika kikao cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Sanaa la Tanzania (BASATA) na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuhusu video hiyo.
Tayari ameshajisajili BASATA kama sharti la kuruhusiwa kufanya maonesho, ameiondoa kwenye mtandao video ya Chura hivyo ataifanya upya video ya muziki wa chura.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni