Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu muafaka wa awali wa walimu kupanda bure daladala baada ya yeye (Makonda) na wamiliki wa gari hizo, kukubaliana kuwasafirisha bure.
Alisema sasa ni mapema kuanza kuzungumzia suala la walimu katika mabasi yaendayo haraka, hivyo aliwataka walimu wanaotumia usafiri huo kuwa na subira kwa kipindi hiki. “Mradi huu wa UDART ndio kwanza unaanza na bado una changamoto zake, hatuwezi kusema leo walimu waanze kupanda bure, mabasi haya pia yana uongozi wake na taratibu zake, lazima tukae tuzungumze nao ili tuone tutafanyaje kuhusu walimu,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa Serikali inamiliki kwa asilimia 49 katika UDART na wenye mradi huo wanamiliki asilimia 51, hivyo lazima kuwepo na utaratibu ambao pande zote kukubaliana kuhusu suala la walimu. Kauli hii ya Makonda imekuja baada ya mradi huo wa mabasi yaendayo haraka, kutoitambua ofa ya walimu hao kupanda bure.
Baada ya kauli hiyo ya Makonda, gazeti hili lilitembelea maeneo mbalimbali yanapopita mabasi hayo, kuangalia hali ya usafiri na changamoto zinazoukabili maradi huo. Gazeti hili lilipita katika vituo vya Feri, Kariakoo, Fire, Ubungo, Kimara na Morocco na kukuta wananchi wakiwa wanakata tiketi kwa foleni na kupanda katika mabasi hayo kwa utaratibu bila usumbufu.
Changamoto kubwa kwa mabasi hayo ni kuwa bado wamiliki wengine wa vyombo vya usafiri, ikiwemo pikipiki, magari madogo na maguta, wakiendelea kutumia njia hiyo ambayo wameonywa kuitumia.
Tatizo lingine ni ukosefu wa umeme katika daraja la juu lililopo Kimara, hivyo kusababisha abiria wengi kukataa kutumia daraja hilo. Wengi walishutumu wenye mradi huo, kushindwa kuweka taa kwenye njia ndefu za juu za daraja hivyo, hivyo kuwatia hofu abiria.
Tatizo lingine katika kituo hicho cha Kimara ni uchafu katika daraja hilo la juu, ambalo limejaa vumbi jingi na makaratasi. Uchafu huo hauzolewi na vumbi nalo halisafishwi na hakuna deki inayopigwa, hivyo vumbi imejaa kila kona. Pia, kituo hicho cha Kimara hakina maji hadi vyooni, hivyo hali ya usafi ni mbaya
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni