ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 21 Mei 2016

MAGAZETINI:#Wanafunzi wengi zaidi vyuo vikuu kukopeshwa

Imeandikwa na Regina KumbaWANAFUNZI zaidi wa elimu ya juu, wanatarajiwa kuanza kupata neema baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kuongeza makusanyo yake kuanzia mwezi ujao kutokana na kujipeleka wenyewe kwa wadaiwa wa bodi hiyo.
Neema hiyo inatarajiwa baada ya bodi hiyo kupokea mwitikio mkubwa wa wadaiwa wa mikopo, kuanzia mwezi Juni wanatarajia kuanza kukusanya Sh bilioni nane kwa mwezi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo wa bodi hiyo, Robert Kibona alisema ongezeko hilo la fedha litasaidi kukopesha wanafunzi wengi zaidi, ambao awali walikuwa wakiachwa kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha.
Alisema baada ya kufanikiwa kongeza idadi ya wadaiwa na bodi, wanatarajia kuongeza makusanyo ya fedha ambayo ni Sh bilioni nane kwa mwezi kuanzia mwezi Juni mwaka huu ikilinganishwa na hapo nyuma walipokuwa wakikusanya Sh bilioni 2.7 tu.
“Fedha hizo tutakazokusanya zitatusaidia sasa kukopesha wale ambao walikuwa wanakosa mkopo, kazi yetu sisi ni kukusanya fedha na kukopesha,” alisema Kibona.
Hii itakuwa msaada mkubwa hasa ikizingatiwa kumekuwa na malalamiko mengi ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutopata fedha za mikopo kwa wakati na wengine kukosa kabisa ingawa fani wanazosomea zinafaa kupewa mkopo.
Kibona alisema mwitikio huo wa watu kujitokeza kuanza kulipa mikopo yao, ni baada ya bodi kutoa notisi ya siku 60 tangu Machi 14 mwaka huu kwa wanufaika wote wa mikopo wanaodaiwa kujitokeza na kuanza kulipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kibona alisema siku hizo 60 zilikamilika Mei 13 mwaka huu na katika muda huo, waajiri pia walitakiwa kuhakikisha wanawasilisha taarifa za waajiri wao waliohitimu katika vyuo vya elimu ya juu ndani ya nchi.
“Lengo la tangazo hilo ilikuwa ni kuhakikisha madeni yanakusanywa ili kuongeza uwezo wa kukopesha watanzania wengi zaidi, hivyo tulipata jumla ya wanufaika wa mikopo 21,721 ambao wanadaiwa Sh bilioni 151.5,” alisema Kibona.
Aidha Kibona alisema katika kipindi hicho cha siku 60 wanufaika 2,007 ambao wanadaiwa jumla ya Sh bilioni 1.93 waliwasiliana na Bodi ya Mikopo kwa kwenda ofisini au kwa barua ili kuanza kurejesha mikopo yao.
Alisema katika siku hizo 30 zilizoongezwa ambazo zilianza jana na zitaisha Juni 20 mwaka huu, Bodi inatoa mwito kwa wanufaika wote, wadhamini au wazazi pamoja na waajiri waliobaki kujitokeza kwani baada ya hapo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hakuna maoni: