ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumanne, 10 Mei 2016

Tanesco: Nchi haitaingia gizani

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limewatoa hofu wananchi kuwa nchi haitaingia gizani baada ya Kampuni ya uzalishaji umeme ya Songas kutishia kuzima mitambo yake kutokana na kulidai shirika hilo.

Aidha, imeelezwa kuwa tayari kampuni hiyo inayozalisha megawati 178 za umeme imeshazima asilimia 81 ya mitambo yake na hivyo kufanya uzalishaji wake wa sasa kuwa megawati 35.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Felchesmi Mramba alisema kampuni hiyo imeenda kinyume cha mkataba wao kwa kuzima mitambo yake bila majadiliano.
Mramba alisema Tanesco itachukua hatua za kisheria kama inavyoelekezwa kwenye mkataba wao, ingawa alikiri Songas inawadai kulingana na mkataba lakini si kweli kuwa wanadai Dola za Marekani milioni 90.
“Kampuni ya Songas imezima asilimia 81 ya mitambo yake ya kuzalisha umeme kwa madai ya kutolipwa na Tanesco. Vilevile kampuni hii imekwenda kwenye vyombo vya habari na kutishia kuzima mtambo mmoja uliosalia ifikapo Mei 11 na kujaribu kuwatia hofu Watanzania kwamba kutakuwa na uhaba wa umeme,” alisema Mramba.
Mramba alisema kampuni hiyo inazalisha megawati 178 lakini imezima mitambo yake na kubakiza megawati 35, pia Tanesco isingependa mitambo hiyo izimwe lakini isiwatishe wananchi kuwa nchi itaingia gizani.
Alisema mahitaji ya umeme ni megawati 1,000 kwa siku na kwamba mitambo ya maji inazalisha megawati 500, Kinyerezi megawati 150, Ubungo (I) 100, Ubungo (II) 29, Tegeta 42, Nyakato, Mwanza 42 pamoja na mitambo mingine.
Mramba alifafanua kuwa hatua zilizochukuliwa na kampuni ya Songas ni kinyume cha makubaliano ya mkataba na imekiuka mkataba wake yenyewe. Aidha, kampuni hiyo pia imefanya kosa kubwa kuzungumza na vyombo vya habari na kujaribu kuwatisha wananchi juu ya kukosekana kwa umeme.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu namba 4.4 kinaitaka Songas kutoa notisi ya siku 90 za kuwa na majadiliano na Tanesco endapo itakuwa haijaridhishwa na jambo lolote la kimkataba.
Aidha, kifungu cha 4.6 cha mkataba huo kinaitaka kampuni hiyo kutoa notisi kwa Serikali na Tanesco baada ya notisi ya awali ya siku 90 kumalizika kabla ya kuzima mitambo yao.
“Lakini pia kifungu cha 17 cha mkataba kinakataza na kuzuia upande wowote unaohusika na mkataba huu kutoa taarifa za mkataba au masuala yanayohusiana na mkataba kwa vyombo vya habari au kwa asiyehusika na mkataba huo pasipo kupata ridhaa ya upande wa pili,” alisema.

Hakuna maoni: