CHUO
Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), kimetoa ufafanuzi wa taarifa
zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa vyuo vyake vishiriki
vimezuiwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kufanya udahili wa
wanafunzi.
Taarifa
hizo zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimedai kuwa vyuo
vishiriki vya SAUT ambavyo ni Stella Maris Mtwara University College
(STEMMUCO) na Archbishop James University College (AJUCO) vimefungiwa na
TCU kufanya udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2016/2017.
Kwa
mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Makamu Mkuu wa
Chuo cha SAUT, Dk Thadeus Mkamwa, taarifa hizo ni za upotoshaji na kuwa
hawajapokea taarifa kutoka TCU ikivizuia vyuo hivyo viwili kufanya
udahili.
Aidha,
Dk Mkamwa aliiomba jamii na wadau wa elimu kwa ujumla kupuuzia taarifa
hizo kwa kuwa zina uwezekano wa kuwa ni mbinu chafu zinazofanywa na
baadhi ya watu kuuhadaa umma hasa katika kipindi hiki ambacho ni muafaka
kwa waombaji kufanya maombi katika vyuo vikuu.
“Tunauomba
umma wa Watanzania kufahamu kuwa, Chuo Kikuu cha SAUT na vyuo vyake
vikuu vishiriki vilivyotajwa hapo juu vinaendelea na udahili wa
wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2016/2017,” alisema Dk Mkamwa.
Alisema
SAUT ni Chuo Kikuu kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Tanzania, na
kwamba kimepiga hatua kubwa katika kujiendeleza na kufanikiwa kuanzishwa
kwa vyuo vingine vikuu vishiriki vya SAUT ambavyo ni STEMMUCO kilichopo
Mtwara, AJUCO kilichopo Songea na Jordan University College (JUCO)
kilichopo Morogoro.
Vyuo
vingine ni St. Francis University College of Health and Allied Sciences
(SFUCHAS)- Morogoro, Archbishop Mihayo University College (AMUCTA)-
Tabora, na Cardinal Rugambwa Memorial University College (CARUMUCO)
kilichopo Bukoba, Marian University College (MARUCO) kilichopo Bagamoyo.
Dk Mkamwa aliongeza kuwa, chuo kimeweza kuanzisha vituo vingine vitatu vya SAUT vilivyoko Mbeya, Arusha na Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni