ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 1 Julai 2016

Mjadala wa Sakata la Lugumi WAZIKWA Rasmi.......Naibu Spika Aipa Serikali Miezi Mitatu

Kiu ya wabunge kujadili sakata la utekelezwa mbovu wa mkataba baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enteprises Limited, imezimwa baada Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuiagiza Serikali kukamilisha utekelezaji wa mradi huo ndani ya miezi mitatu ijayo. 
Kwa muda mrefu, wabunge walikuwa wakisubiri ripoti ya uchunguzi kutoka Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) ili waweze kujadili kwa kina sakata hilo linalohusisha mradi wa Sh37 bilioni wa kufunga vifaa vya kielektroniki vya kuchukua alama za vidole (AFIS). 
Mapema Aprili mwaka huu, wakati PAC ikipitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka ulioshia Juni 30, 2014 ilibaini kuwa Lugumi ilikuwa imefunga mashine katika vituo 14 tu kati ya 108 ilivyotakiwa kuvifunga wakati ikiwa imeshapokea asilimia 99 ya malipo yote.
 PAC ilimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani apeleke taarifa ya utekelezaji wa mradi huo ambayo aliipeleka Aprili 18 na kubaini kuwa vifaa hivyo vilifungwa katika vituo 153 pamoja na makao makuu ya polisi. 
Kutokana na utofauti wa takwimu za CAG na PAC iliunda kamati ndogo kufanya uhakiki wa vifaa vya AFIS na sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa mradi, huku wengi wakitarajia ripoti hiyo ingejadiliwa bungeni. 
Katika sakata hilo, wabunge walimtuhumu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kuwa na masilahi kwa madai kuwa alikuwa mmoja wa wanahisa wa kampuni ya Infosys iliyoshirikishwa kwenye mradi huo na kushinikiza ajiuzulu kupisha uchunguzi. 
Hata hivyo, Kitwanga alitimuliwa kazi kwa kosa jingine la kuingia bungeni kujibu maswali ya wizara yake akiwa amelewa. 
Jana, Dk Tulia alitumia kanuni 117(17) kukabidhi matokeo ya uhakiki huo kwa Serikali, yakiwemo maoni, ushauri, mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto zilizoanishwa na taarifa ya kamati ya PAC na kutoruhusu mjadala kwa wabunge
Dk Tulia alieleza kuwa amefanya uamuzi huo baada ya kupokea taarifa hiyo na kuangalia maudhui yake, kuzingatia matokeo ya uhakiki huo uliofanywa na kamati ndogo na PAC kujiridhisha uwepo wa vifaa hivyo, ukiacha kasoro zilizojitokeza. 
Pia, alisema suala hilo si jipya kwa kuwa linatokana na hoja ya ukaguzi wa miaka ya nyuma na kilichokuwa kimebaki ni vifaa hivyo kufanya kazi.

“Naagiza sasa kwamba Serikali ihakikishe mfumo huu unafanya kazi ndani ya miezi mitatu kuanzia leo (jana) ili kuboresha uwezo wa Jeshi la Polisi kuwa na utambuzi wa haraka wa wahusika wa matukio ya kihalifu katika vituo vyote nchini,” alisema huku akishangiliwa. 

Dk Tulia aliitaka pia Serikali kuyapatia ufumbuzi haraka masuala yote yaliyobainika kuwa na dosari za kiutendaji. 
Alisema ameielekeza kamati ya PAC kuhakiki maagizo aliyoyatoa kwa Serikali na baada ya uhakiki huo itoe taarifa bungeni wakati ikiwasilisha taarifa yake ya mwaka. 
“Natarajia kuwa suala hili sasa litafikia mwisho na CAG atafunga hoja yake baada ya kujiridhisha na utekelezaji wa maagizo niliyoyatoa,” alisema Dk Tulia. 
Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly alisema walishamaliza kazi yao baada kumkabidhi Naibu Spika ripoti hiyo, kama kanuni zinavyotaka na kwamba yeye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho. 
Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ndogo ya kuchunguza suala hilo, Japhet Asunga alisema baada ya uchunguzi, walibaini vituo 15 tu kati ya 153 ndivyo vimeunganishwa na mfumo wa taarifa za polisi. 
Asunga, ambaye ni mbunge wa Vwawa (CCM), alimwambia mwandishi wetu kuwa kamati ilibaini kuwa vifaa vyote vya AFIS vilivyokuwapo katika vituo vimetelekezwa bila kuunganishwa katika mfumo wa mtandao.
Alisema sehemu nyingine walikuta vifaa vimetupwa huku vingine vimeharibika kwa sababu vimekaa muda mrefu kama wino wa printa umeisha muda wake. 
“Tumeagiza Serikali ichukue hatua stahiki kuhakikisha vifaa vinatumika na kuwaadhibu wote waliochelewesha na nani hakufanya kazi ipasavyo.
“Ndiyo maana Naibu Spika baada kupima maagizo yaliyotolewa ameona Serikali ianze kuyafanyia kazi mapungufu badala ya kusubiri kuyawasilisha Septemba. Naona busara imetumika,” alisema Asunga. 
Alisema kamati haina tatizo na maazimio ya miezi mitatu aliyotoa Spika kwa kuwa ndiyo mapendekezo yao na kwamba PAC wao awali walipendekeza miezi sita.

Hakuna maoni: