Waziri
wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba amewasili mkoa wa Geita kwa
ziara ya kikazi, kubwa ikiwa ni kufuatia taarifa za mateso na mauaji
yaliyodaiwa kufanywa na raia wa China wanaomiliki sehemu ya mgodi wa
Nyamhuna uliopo Katoro, Geita dhidi ya wafanyakazi/vibarua ambao ni
Watanzania.
Takribani wiki moja sasa kumekuwa na hali ya sintofahamu dhidi ya picha zinazoenezwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zikionesha raia wa Tanzania anayefanya kazi kwenye mgodi tajwa akiteswa na kufanyiwa vitendo ya kinyama na mwajili wake ambaye ni raia wa china.
Ilimlazimu
Waziri mwenye dhamana na usalama wa raia na mali zao kupitia Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi kufika eneo la mgodi kujiridhisha kwa taarifa
zilizotapakaa na kubeba simanzi kwa Watanzania.
Mwigulu
Nchemba amejiridhisha kuwa kulikuwepo na tukio hilo la Mtanzania
kuteswa na mwajiri wake, kipigo kilichosababisha kupoteza fahamu na siyo
kifo.
Hatua
za awali Waziri Nchemba alizozifanya ni kwenda gereza la Geita mjini
alikohifadhiwa kijana huyo kwa madai ya kushitakiwa na mwajiri wake kwa
kosa la wizi lililosababishwa apigwe.
Katika
mahojiano ya Waziri Mwigulu Nchemba na kijana huyo, Mwigulu alibaini
kuwa kijana huyo aliyepo gerezani ndiye mhusika hasa wa tukio lile kwa
uthibitisho wa makovu yaliyopo mwili mwake na mavazi aliyovalia wakati
anateswa na akiwapo gerezani.
Katika
hali hiyo, ilimlazimu, Mhe. Mwigulu kwenda mgodini akiwa ameambatana na
kijana huyo kwa ajili ya kutambua waliofanya vitendo hivyo vya
kinyama.
Katika
oparesheni hiyo, kijana aliyeteswa na kujeruhiwa aliwabaini Watanzania 5
ambao ni walinzi wa eneo hilo na Mchina mmoja walioshirikiana kumpiga,
kumtesa na kumjeruhi.
Kufuatia
utambuzi huo na maelezo ya wahusika, Nchemba akaagiza wahusika
wakamatwe mara moja na akaondoka nao kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika
hali nyingine ya kusikitisha, Waziri Nchemba amebaini uwepo wa
wahamiaji haramu raia wa China katika mgodi huo ambapo nyaraka za
uhamiaji mkoa wa Geita zinaonesha raia 28 wenye vibali ndio waliruhusiwa
kukaa kwenye mgodi huo, lakini katika operasheni ya kushitukiza
aliyoifanya Mhe. Nchemba amebaini uwepo wa raia wa china zaidi ya 50
wanaoishi katika mgodi huo kinyume na sheria.
Hivyo
amemuagiza Mkuu wa Mkoa na timu yake ya uhamiaji kuhakikisha wote wasio
na vibali wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni