ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatatu, 11 Julai 2016

Mwenyekiti wa Chadema Awazuia Vijana wa Chadema ( BAVICHA ) Kwenda Dodoma

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiacXY69F6eDNr-zExmYxmRgr1kuSWaSZVcMGRe1DJjVak36KkYZQLO67miRiC_s06FUu95oF0AMAphBc1uO2NRcy2eh1WmmIsuSVmANijrKdG_pQlGDwsCsW2iiJi5aRKHcG2mEm63eAE/s1600/1.jpg
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kusitisha mpango wa vijana wa chama hicho kwenda Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM ili kuepusha maafa ambayo yanaweza kutokea. Badala yake, Mbowe amesema wataendelea kusaka haki ya kufanya mikutano ndani na nje ya nchi. 
Sambamba na uamuzi huo, chama hicho kimetaka viongozi sita wa Baraza la Vijana (Bavicha) wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kuachiwa mara moja. 
Mbowe alitoa tamko hilo jana wakati akizungumza na wanahabari jijini Arusha, katika mkutano wa mameya na wenyeviti wa halmashauri 18 zinazoongozwa na Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa).
 Sababu za kusitisha 
Mbowe alisema wamewataka vijana wa Chadema nchi nzima ambao walianza kujiandaa kwenda Dodoma kuisaidia polisi kuzuia mkutano huo wa Julai 23 kutokwenda kwa sababu polisi wamepewa maagizo ya kuwapiga na kuwajeruhi, hivyo wao hawataki kupambana nao. 
“Nawataka vijana wote wa Chadema waliokuwa wanajiandaa kwenda Dodoma wasitishe na wasubiri maelekezo mapya ya Chadema,” alisema Mbowe. 
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema wana taarifa Jeshi la Polisi limejipanga kuwanyima dhamana viongozi wa Bavicha hadi baada ya mkutano wa CCM, ingawa viongozi wote wa chama hicho hawana hofu ya kukaa mahabusu. 
Aliwataka vijana hao kutokwenda Dodoma na wawaache CCM waendelee na mkutano wao kwa kuwa Chadema haina hofu na mkutano wa chama hicho, bali walitaka dunia ione jinsi polisi wanavyofanya kazi kwa maelezo ambayo yanakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya nchi. 
“Wakati sisi tunazuiwa kufanya siasa, Rais anafanya siasa, Waziri Mkuu anafanya siasa, mawaziri wanafanya siasa, wakuu wa mikoa na wilaya wanafanya siasa jambo ambalo si sahihi,” alisema.
 Alisema lengo la Bavicha kwenda Dodoma ni kuchoshwa na uonevu wa kuzuiwa kufanya mikutano ya ndani na hadhara wakati CCM wanaendelea na mikutano yao. 
“Waliona pengine itakuwa busara washinikize polisi kuona maagizo yao ya kuzuiwa mikutano yanatekelezwa kwa wote,” alisema. 
Alilitaka jeshi la polisi kufanya kazi kwa kufuata taratibu kwa kutoa haki sawa kwa wote, kwa kuruhusu vyama vyote kufanya mikutano yao. 
Apinga tamko la Mwigulu
Kuhusu tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuhusu mikutano hiyo, Mbowe alisema hawakulielewa tamko hilo la Rais, kuwa mikutano ambayo imezuiwa ni ya hadhara na maandamano na si ya ndani. 
Alisema mikutano ya ndani ya chama hicho imezuiwa kwani Chadema Wilaya ya Kahama walikuwa na mkutano wa ndani wa uchaguzi ambao umezuiwa. 
 Alisema mkutano wa ndani na wabunge wa Chadema mkoani Shinyanga ulizuiwa na pia mahafali za Vijana wa Vyuo Vikuu wa Chadema (Chaso). 

“Lakini wakati haya yanafanyika, CCM waliendelea na mikutano yao na mahafali yao,” alisema. 
Alisema Chadema itaendelea kudai haki ya mikutano na maandamano katika mahakama za ndani na nje ikiwamo ya Afrika ya Mashariki. 
Viongozi wa madiwani 
Katika mkutano wa wenyeviti wa halmashauri 18 zinazoongozwa na Chadema, Mbowe alisema Calist Lazaro, Meya wa jiji la Arusha amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa madiwani wa Chadema nchini.
Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alichaguliwa kuwa katibu wa madiwani wote wa chama hicho na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime, Moses Matiku alichaguliwa kuwa mnadhimu wao. Wote hao watakuwa wajumbe wa Kamati Kuu Chadema. 
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema katika mkutano huo wenyeviti hao wamepatiwa elimu juu kuongoza vyema halmashauri zao ili kuchochea maendeleo. 
“Siku mbili za mkutano huu tumekaa na kuweka mikakati bora ya kuhakikisha halmashauri zinazoongozwa na upinzani zinafanya vizuri,” alisema.

Hakuna maoni: