Leo ndiyo mwanzo wa utekelezaji wa Sheria Fedha (Finance Act, 2016) iliyopitishwa katika Bajeti ya 2016/17 ambapo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) itatozwa katika huduma za mitandao ya simu, benki na taasisi za fedha.
Akisoma
hotuba ya bajeti bungeni hivi karibuni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Philip Mpango pamoja na mambo mengine, alipendekeza kuongeza kodi hiyo
katika huduma za kibenki zinazotozwa na benki hizo ili kupanua wigo wa
kodi isipokuwa riba kwenye mikopo.
Vilevile,
Waziri Mpango alieleza azma ya Serikali kutoza ushuru wa bidhaa wa
asilimia 10 kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma katika kutuma na
kupokea fedha badala ya ushuru huo kutozwa tu kwenye kutuma fedha pekee.
Akizungumzia
uamuzi huo, mtaalamu wa kodi wa kujitegemea, Deogratias Peter alisema
ongezeko hilo litawakatisha tamaa wateja wa benki na watumiaji wa
miamala ya simu.
“Kwa
zaidi ya miaka 10 sasa, Serikali inafanya jitihada za kuongeza
watumiaji wa benki kwani katika nchi za Afrika Mashariki ilikuwa nchi ya
nne mbele ya Burundi kwa kuwa na idadi ndogo ya watu wanaotumia benki.
Lakini hatua hii inaweza kurudisha nyuma jitihada hizo,” alisema Peter.
Alisema
Serikali ilianzisha utaratibu wa Saccos, Vicoba na kulegeza masharti ya
kuwa na akaunti ya benki ili kuwawezesha wananchi wa kawaida kumudu
kuweka fedha kwenye taasisi za fedha na ilianzisha Benki ya Rasilimali
Tanzania (TIB), Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), wakala wa benki na
miamala ya simu ili kuongeza watumiaji wa benki.
“Watanzania wengi wasio na utamaduni wa kuweka fedha benki watakubali kukatwa fedha zao kiasi hicho?” alihoji.
Alisema
mfumo huo kwa sasa haueleweki hasa kwa watumiaji wa miamala ya simu kwa
kuwa mawakala wake hawatoi risiti kama ilivyoagizwa na Serikali.
Aliongeza kuwa hata katika mashine za ATM, hakuna mashine za kukata kodi ya VAT hivyo hakuna maandalizi ya kukokotoa kodi hizo.
Mkurugenzi
wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Richard Kayombo alipoulizwa kuhusu makato hayo, asisitiza azma ya
Serikali kukusanya mapato kwa njia yoyote ile, bora tu iwe ni ya
kisheria.
“Sina
tafsiri yoyote ya kodi hiyo. Sisi kazi yetu ni kukusanya tu mapato…
Sheria zinaruhusu kuwa na mabadiliko ya kodi kama hayo, kwa hiyo sisi
tunatekeleza maagizo tu ya Serikali, haturuhusiwi kutafsiri kwa njia
yoyote,” alisema Kayombo.
Jana,
benki za CRDB,NMB na Standard Chartered zilitoa maelekezo kwa wateja
wake juu ya kuwapo kwa makato hayo zikisema kuwa kutakuwa na ongezeko la
asilimia 18 litakalotozwa katika gharama za huduma za benki kunzia leo,
zikiungana na NBC ambayo ilitangaza azma hiyo wiki iliyopita.
“Kufuatana
na Sheria ya Fedha (Finance Act, 2016) ongezeko la asilimia 18
litatozwa katika gharama za huduma za benki kuanzia Julai 1, 2016.
Ongezeko hili (VAT) litakatwa kutoka katika akaunti na kama muamala
hautapia kwenye akaunti, mteja atalipa kwa fedha taslimu,” ilisema sehemu ya taarifa ya Benki ya CRDB.
Hata
hivyo, kama zilivyo taarifa za benki nyingine, ilisema ongezeko hilo
halitahusika katika riba kwenye mikopo. Benki ya NMB, ilisema katika
taarifa yake kuwa ongezeko hilo litakuwa katika gharama zote za miamala
ya kibenki kuanzia leo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni