ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 1 Julai 2016

Yanga hatarini kuadhibiwa Caf

Imeandikwa na Vicky Kimaro
KLABU ya Yanga huenda ikaondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho inayoendelea baada ya vurugu kubwa ikiambatana na mabomu kurindima katika mchezo wao na TP Mazembe uliofanyika Jumanne iliyopita Juni 28, kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ambao Yanga ilitangaza kiingilio bure, ulifurika mashabiki zaidi ya 60,000 ingawa walitakiwa kuhakikisha mashabiki wao wasizidi 40,000 na Kamisaa wa mchezo ambaye aliwatadharisha Yanga iwapo watu watazidi, basi angeufuta mchezo huo.
Hata hivyo, vurugu zilizozuka zilisababisha uharibifu wa mali za uwanja ikiwemo kuvunjwa kwa mageti na viti ndani ya uwanja huo wa taifa ambao kwa sasa zinafanyika tathmini ya uharibifu huo na Yanga watalazimika kulipa.
Juni 18 mwaka huu, CAF iliitoa Entente Setif ya Algeria katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya vurugu za mashabiki na kuipa ushindi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Agosti 2011, wawakilishi wa Tunisia kwenye michuano hiyo ya klabu bingwa, Etoile du Sahel waliondolewa mashindanoni baada ya mashabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi ya hatua ya makundi.
Adhabu hiyo huenda ikaikumba pia Yanga, na jana Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alisema Yanga wakiwa na wawakilishi wao katika mkutano wa maandalizi wa Alhamisi Juni 23 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam walitangaza juu ya kuchapisha tiketi 40,000 na wakatangaza na viingilio.TFF baada ya kikao hicho iliwajulisha CAF juu ya jambo hilo kama ilivyo ada.
Mkutano wa kawaida wa maandalizi ya mechi (pre-match meeting) baina ya timu zote mbili,yaani Yanga na TP Mazembe ulifanyika Juni 27 katika ukumbi wa hoteli ya Coral Beach, Masaki jijini Dar es Salaam na uliendeshwa na Mratibu Mkuu wa CAF wa mchezo huo, Sidio Jose Magadza – Raia wa Msumbiji, ambapo katika kikao hicho, Yanga walitamka kuwa mchezo wao utakuwa bure.
Malinzi alisema kuwa msimamizi wa CAF alikiambia kikao kuwa kama hayo ndiyo maamuzi ya Yanga watambue kuwa itakuwa ni kwa gharama zao.
Aidha, aliagiza watazamaji 40,000 tu ndio waruhusiwe kuingia uwanjani hata kama ni bure, hii ni kwa sababu za kiusalama, “Hilo halikufanyika na badala yake uwanja ulijaa watu 60,000 na kutokana na pilika pilika za watu kutaka kuingia uwanjani zilitokea vurugu, ambazo zilisababisha wana usalama kutumia nguvu. “Hili nalo lilishuhudiwa na wawakilishi wa CAF na hatujui wameripoti vipi tukio hili, ikumbukwe wajibu wa TFF, CAF na FIFA ni kuhakikisha mashindano yao yanafanyika kwa utulivu na amani bila kuathiri maisha ya watu, mali zao na miundombinu ya michezo,”alisisitiza Malinzi.
Alisema kutokana na suala hilo TFF inafuatilia kwa karibu kujua nini yatakuwa maamuzi ya CAF baada ya ripoti za msimamizi na kamisaa wa mchezo kuhusu matukio yaliyotokea nje ya uwanja kabla na wakati wa mechi.
“Siku zote TFF imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha mchezo wa mpira unachezwa katika eneo salama, hivyo kuanzia sasa jukumu la kusimamia michezo ya kimataifa litakuwa linaratibiwa kwa karibu zaidi na TFF, ikiwa ni pamoja na mapokezi ya timu.” “Kingine litakachoratibiwa na TFF ni kuwapokea maofisa, kuangalia malazi kama yako sahihi, usalama, maamuzi kuhusu viingilio na uuzaji wa tiketi, usafiri wa ndani, viwanja vya mazoezi.”
Alisema mamlaka ya TFF katika mashindano ya ndani na ya kimataifa ni pamoja na usimamizi wa maandalizi ya mchezo, usimamizi wa mapato,usimamizi na uhakiki wa haki za matangazo, usalama ndani na nje ya uwanja, usimamizi wa upelekaji taarifa CAF na FIFA.
Alisema kwa yeyote anayetaka kucheza mpira unaotambuliwa na FIFA, CAF, CECAFA na TFF ni sharti akubaliane na kutii mamlaka hizo. Kauli hiyo ya Malinzi imekuja, ikiwa ni siku moja baada ya uongozi wa Yanga kudai kuwa hailipi chochote kwa TFF wala CAF na badala yake italipa gharama za uwanja na ulinzi pekee kwa kuwa hawajaingiza mapato yoyote katika mchezo huo, ambao waliingiza mashabiki bure.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa na Yanga kunyukwa bao 1-0, wametakiwa kulipa makato yote yanayohitajika, ikiwemo asilimia tano ya makato za CAF, asilimia 10 gharama za mchezo, nyingine gharama ya uwanja asilimia 15, TFF asilimia tano, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), asilimia 10, DRFA asilimia tano pamoja na makato ya TRA asilimia 18.
Tayari Yanga ilikuwa imechapisha tiketi 31,000, ambazo zingeuzwa Sh 7,000 ambazo zingeingiza Sh 217,000,000 huku zile za Sh 25,000 zilikuwa zimechapishwa tiketi 8,200 zilitarajiwa kuingiza Sh milioni 205 huku VIP zilikuwa tiketi 5,000, ambazo zingeingiza Sh milioni 150.
Jumla ya fedha zote ambazo zingepatikana katika mchezo huo zilitarajiwa kuwa Sh milioni 572. Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdetit alisema jana kuwa hawapo tayari kulipa fedha hizo kwa vile mchezo ulikuwa bure na kwamba watalipa gharama za uwanja, ulinzi na Msalaba Mwekundu pekee, CAF, TFF na makato mengine wawasemehe.
Kwa mujibu wa kanuni za CAF, katika hatua ya makundi shirikisho la soka la nchi husika inalazimika kuilipa CAF dola 2,000 sawa na Sh 420,000 katika mauzo tiketi ya mechi za makundi.
“Sasa tiketi hatujauza, watu wameingia bure hizo fedha za kulipa TRA, CAF, TFF na wengineo zingepatikana kwenye mapato, tulimuliza mratibu wa CAF kuhusu kuingiza watu bure akasema ni sahihi, kwa hiyo watusamehe tu,” alisema Baraka.
Hata hivyo, kwa upande wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), umesema kuwa wanachofahamu Yanga walichapisha tiketi 40,000 na taratibu wanazijua na walielezwa sasa kama wao wanasema hawalipi, basi hatua za kisheria zitachukuliwa.
Aidha, Malinzi amewaangukia mashabiki wa mpira kwa kuwaomba radhi kwa kadhia yote iliyotokea kutokana na kitendo cha klabu hiyo ya Jangwani kuruhusu watazamaji kuingia bure na kusababisha vurugu. Malinzi amevishukuru vyombo vya vya ulinzi na usalama kwa hatua walizochukua ili kuepusha maafa, ambayo yangeweza kutokea.

Hakuna maoni: