ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 6 Julai 2016

#MAGAZETINI:Serikali yaagiza maandalizi kupokea wa kidato cha 5

WAKUU wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini wameagizwa kujiandaa kuwapokea vizuri wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na kuwaandalia chakula wanafunzi wa bweni kabla shule hazijafunguliwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene alisema hayo jana mjini hapa wakati akizungumzia maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2016 kwenye shule mbalimbali walizopangiwa.
Wanafunzi hao wanatakiwa kuripoti shule walizopangiwa Julai 11, mwaka huu. Alisema ni vizuri kwa watendaji hao kujipanga ili wanafunzi wanapofika kwenye shule walizopangiwa wakute mazingira mazuri. Alisema wanafunzi hao wamepangwa katika shule 329 zote za kidato cha tano na sita nchini, na kati ya hizo 50 ni mpya.
Simbachawene alisema wanafunzi wa awamu ya kwanza waliopangwa kujiunga na kidato cha tano ni 65,720 kati ya 90,248 na awamu ya pili inasubiri nafasi zitakazojitokeza kutokana na wanafunzi watakaoacha kuripoti kwa kupelekwa na wazazi wao kwenye shule za binafsi.
Alisema chimbuko la kuanzisha shule mpya za kidato cha tano 50 imetokana na maombi ya mikoa kwenye maeneo yao ili kuendana na lengo la serikali la kuongeza shule za kidato cha tano na sita hapa nchini.
Alisema wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa wana wajibu wa kuzihudumia shule hizo kwa karibu, na pia kuhakikisha miundombinu yote inakamilika ikiwemo mabweni, madarasa, vyoo, maabara, samani, huduma za maji na umeme.
Wakati huo huo, Waziri Simbachawene amesema kuanzia sasa shule zote za serikali zifungwe na kufunguliwa siku moja tofauti na sasa kila shule imejiwekea utaratibu wake.

Hakuna maoni: