ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 6 Julai 2016

#MAGAZETINI:Kampuni za simu zaadhibiwa, zatozwa milioni 650/-

Imeandikwa na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezitoza faini ya jumla ya Sh milioni 649 kampuni sita za simu nchini kwa kosa la kukiuka masharti ya usajili na matumizi ya laini za simu.
Aidha, TCRA imetoa siku saba kwa kampuni za simu kuzima laini zote zilizokiuka masharti ya usajili zilizoko sokoni ambazo zimewashwa na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wake kwa mamlaka hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema hatua hiyo imetokana na mamlaka hiyo kufanya ukaguzi katika mifumo ya usajili wa laini za simu na kugundua baadhi ya namba kutolewa bila mteja kujisajili, kusajiliwa kwa majina, vitambulisho na nyaraka za watu wengine.
“Pia TCRA imebaini baadhi ya kampuni kutofunga namba hadi usajili ukamilike na kusajiliwa usajili wa awali ikiwa ni kinyume na Kanuni ya 33 ya Kanuni za Leseni za mwaka 2011 zilizotolewa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010,” alisema Kilaba.
Kampuni zilizopata adhabu hiyo ni Airtel Tanzania Limited, Benson Informatics Limited, MIC Tanzania Limited, Viettel Tanzania Limited, Vodacom Tanzania Limited na Zanzibar Telecom Limited.
Akifafanua adhabu hizo kwa kila kampuni, Kilaba alisema Airtel imetozwa faini ya Sh milioni 182.7.
Akichanganua faini hiyo ya Airtel, alisema Sh milioni 74 ni kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 148 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi, Sh milioni 33.5 kwa kuruhusu laini 67 ziuzwe bila kujaza fomu, Sh milioni 32.5 kwa kuruhusu laini 65 ziwashwe kabla ya kuuzwa na Sh milioni 42.5 kwa kuruhusu laini 85 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
Alisema kwa upande wa Benson Informatics Limited imetozwa faini ya Sh milioni 17. Sh milioni saba kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 14 bila kitambulisho halisi, Sh milioni saba kwa kuruhusu laini 14 ziuzwe bila kujaza fomu na Sh milioni tatu kwa kuruhusu laini sita ziwashwe kabla ya kuuzwa.
Kilaba alisema kwa Kampuni ya MIC Tazania Limited, imetakiwa kulipa faini ya Sh milioni 189 ikiwa ni Sh milioni 93.5 kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 187 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi, Sh milioni 43.5 kwa kuruhusu laini 87 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili, Sh milioni 41 kwa kuruhusu laini 82 ziwashwe kabla ya kuuzwa na Sh milioni 11 kwa kuruhusu laini 22 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
Alisema Viettel Tanzania Limited wametozwa faini ya Sh milioni 107 ikiwa ni Sh milioni 36.5 kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 73 bila kutumia kitambulisho halisi cha ununuzi, Sh milioni 36 imeruhusu laini 72 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili na Sh milioni 34.5 kwa kuachia laini 69 ziwashwe kabla ya kuuzwa.
Alisema Vodacom Tanzania Limited imetozwa faini ya Sh milioni 96.5 ikihusisha Sh milioni 49 kwa kuacha laini 98 zisajiliwe bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi, Sh milioni 24 kwa kuruhusu laini 38 ziwashwe kabla ya kuuzwa na Sh milioni 4.5 kwa kuruhusu laini tisa zifanyiwe usajili wa awali kwa kutumika kwenye mtandao wake.
Alisema kwa upande wa Zanzibar Telecom Limited imetakiwa kulipa faini ya Sh milioni 57 ikiwa ni Sh milioni 36.5 kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 73 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi, Sh milioni 11.5 kwa kuruhusu laini 23 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili na Sh milioni saba kwa kuruhusu laini 14 ziwashwe kabla ya kuuzwa na Sh milioni mbili kwa kuruhusu laini nne zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
“Kabla ya kutolewa hukumu hii, tuliziita kampuni za simu zilizogundulika kutenda makosa hayo na kutakiwa kutoa utetezi wao kuhusu ukiukwaji wa masharti ya usajili wa namba za simu. “Ikumbukwe kuwa Aprili 2013, TCRA na kampuni walikubaliana kuondoa kasoro zilizojitokeza katika usajili wa namba za simu kwa kutowezesha laini kutumika kabla ya usajili kukamilika na taarifa za mteja kuhakikiwa na kutofanya kile kinachoitwa usajili wa awali,” alisema.
Sheria ya EPOCA ya 2010 inataka kampuni za simu kusajili laini ili kumlinda mtumiaji kutokana na matumizi mabaya ya huduma za mawasiliano, kuwezesha kuwatambua watumiaji wa huduma za ziada za simu na kuimarisha usalama wa taifa.
Pia kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kuwafahamu wateja wao na kuwa na taarifa za matumizi ya simu za mkononi kwa ajili ya mipango ya maendeleo.
Akizungumzia ukomo wa matumizi ya simu bandia na uanzishwaji wa rajisi kuu ya namba tambulishi, Kilaba alisema mpaka sasa namba tambulishi ambazo hazikidhi viwango 1,713,337 na zilizonakiliwa 117,389 zimezimwa.

Hakuna maoni: