ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 6 Julai 2016

Tathimini kuamua hatma waliozembea madawati

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene
 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amesema wanaendelea kukusanya takwimu za madawati mikoa yote nchini ambazo zitabainisha mkoa wa kwanza hadi wa mwisho katika kufanikisha kampeni hiyo na hatua zitakazochukuliwa kwa walioshindwa.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati akikabidhiwa hundi ya Sh milioni 900 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati nchini iliyotolewa na Benki ya NMB.
Alisema tatizo la uhaba wa madawati lilikuwepo tangu awamu zilizopita za uongozi wa nchi, hata hivyo tatizo hilo liliongezeka mwaka huu kutokana na serikali kuanza kutekeleza utoaji wa elimu ya msingi bila malipo.
Aliongeza kuwa, utekelezaji huo ulihamasisha wazazi na jamii kwa ujumla kuwaandikisha watoto wengi kuanza darasa la awali na darasa la kwanza, hivyo idadi kubwa ya uandikishaji imeongeza upungufu wa madawati uliokuwepo.
Waziri huyo alisema Januari mwaka huu, watoto waliotegemewa kuanza darasa la kwanza walikuwa milioni moja, lakini walioandikishwa walifikia milioni 1.3.
“Tunaendelea kukusanya takwimu za madawati na tutajua wa kwanza hadi wa mwisho na hatua zitakazochukuliwa kwa walioshindwa,” alisema na kuongeza kuwa pamoja na hayo, sasa wanaelekeza nguvu kwenye kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa, kwani vilivyopo havitoshi.
Alisema katika shule za msingi kuna upungufu wa vyumba vya madarasa 127,799 sawa na asilimia 54 kati ya vyumba 236,092 vinavyohitajika huku kwa upande wa sekondari kuna upungufu wa vyumba 10,636 (asilimia 23.7).
Aidha, Simbachawene ameishukuru NMB kwa kuitikia mwito wa Serikali ya Rais, Dk John Magufuli kwa kuchangia Sh milioni 900 za kununulia madawati. Naye Ofisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Waziri Barnabas alisema sera yao ni kutoa asilimia moja ya mapato yao kwa ajili ya shughuli za kijamii.

Hakuna maoni: