ALIYEKUWA
mgombea urais kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
Edward Lowassa amewataka vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kumlinda Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kama nyuki
wanavyomlinda malkia wao.
Lowassa
ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitoa kauli hiyo wakati
akifungua kikao cha Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vijana (Bavicha)
jijini Dar es Salaam jana.
Waziri
mkuu huyo wa zamani, pamoja na mambo mengine aliwataka vijana wa chama
hicho kuacha vita vya ndani kwa ndani na badala yake washikamane na
kuwang’ang’ania viongozi wanaowaongoza.
“Tuache
vita vya ndani kwa ndani, Mbowe ndiye mwenyekiti wetu wa chama…tumlinde
kama nyuki wanavyomlinda malkia wao. Mtu akishakuwa kiongozi
tumg’ang’anie,”alisema Lowassa.
Lowassa
ambaye alijiunga na upinzani mwishoni mwa mwaka jana alisema kumekuwapo
na kawaida ya kuibuka kwa makundi uchaguzi unapomalizika.
Azungumzia uchumi
Katika
mkutano huo, Lowassa pia alizungumzia uchumi ambapo alisema hivi sasa
maisha ya Watanzania walio wengi hayana uhakika, huku matumaini kidogo
yakielekezwa kwa watu wachache.
“Binadamu
anaishi kwa matumaini, lakini mambo yanayoendelea hapa nchini hayatoi
matumaini hayo…hali ya uchumi inakwenda vibaya sana, kuna rafiki yangu
mmoja ana msamiati wake anasema maisha ni pasua kichwa hivi sasa kwa
sababu hayana uhakika,” alisema Lowassa.
Aidha
Lowassa alieleza kusikitishwa kwake kwa baadhi ya watu kuacha kuzikana
kwa sababu ya siasa ambapo alisema hayo ni mambo ya ovyo.
Ajivunia vijana
Katika
hotuba yake hiyo, Lowassa aliwapongeza Bavicha kwa kutii maelekezo ya
Mbowe kuhusu kusitisha uamuzi wao wa kwenda Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Niwapongeze
kwa kutii maelekezo ya mwenyekiti wetu, najua haikuwa rahisi, mlikuwa
mmeshajipanga lakini maelekezo ya mwenyekiti ni mazuri, vitu vingine si
lazima uende mbali sana ni kama kwenye simu kwamba ‘message sent’
mlifikisha ujumbe mahsusi hata kama hawakubaliani lakini ujumbe umefika.
“Wala
msione aibu mnachofanya, vijana mngefanya tofauti ningeshangaa, nyie
ndio chachu ya mabadiliko lazima mje na kitu kipya na mawazo mapya,
ninyi ni jeshi la chama.
“Kwa
uzoefu wangu CCM lazima watakwenda kumtambulisha mwenyekiti wao mpya
katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, hivyo wananchi wenyewe
wataangalia na kupima kama Chadema wanazuiwa kwa nini wapinzani wazuiwe,
waachane wapate tabu kujieleza kwa umma” alisema Lowassa huku akishangiliwa.
Kuhusu
uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli hivi karibuni, Lowassa
aliuponda na kusema ni wa kibaguzi kwa sababu umewatenga vijana wa vyama
vya upinzani.
“Kama
wewe ni CCM utakuwa mkuu wa wilaya, mkoa na hata mkurugenzi wa
halmashauri lakini hali ni tofauti kwa vijana wa upinzani, wanabaguliwa
utadhani si Watanzania.
“Hili
ni jambo la kutafakari na kukemea kwa sabu ajira ni tatizo hapa nchini,
lakini hata hizo chache zinatoka kwa kubaguana pamoja na jitihada zote
lakini hazisaidii,”alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni