ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatatu, 8 Juni 2015

Waliochukua fomu urais kupitia CCM wafikia 18


Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akionyesha begi lenye fomu za kuomba kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Makada watatu wa CCM jana walijitokeza katika makao makuu yake mjini hapa kuchukua fomu kuomba kupewa ridhaa na chama hicho ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani
Waliochukua fomu jana ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kada wa chama hicho, Leonce Mulenda na Ofisa Mwandamizi mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Peter Nyalali na kufanya idadi ya wanaCCM waliokwisha fanya hivyo kufikia 18.
Nyalandu: Ninafahamu changamoto
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Nyalandu ambaye alisindikizwa na wabunge wa viti maalumu, Mary Chatanda na Martha Mlata alisema amechukua fomu akifahamu umuhimu wa kuyaendeleza yote yaliyofanywa na serikali ya awamu ya nne... “Ninafahamu changamoto zinazotukabili. Nazitazama, naziona hatua ambazo zipo tangu wakati wa Baba wa Taifa alipomkabidhi kijiti Rais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Rais Jakaya Kikwete.”
Alisema anafahamu changamoto zinazolikabili Taifa na anaitazama nchi iendelee kulinda misingi iliyoachwa na waasisi wa Taifa kwa kuendeleza amani.
Alisema umoja, undugu na mshikamano atakaoulinda, utaifanya Tanzania iwe na nguvu ya kutatua changamoto za sasa na za kesho.
Huku akipigiwa makofi na wapambe wake, Nyalandu alisema waliambiwa zamani kuwa wazee wanaotawala vyema wanastahili heshima maradufu.
“Tutaendelea kuwaenzi wazee waliotutawala, wamekuwa wakitulea katika miji na vijijini, tutaendelea kuwaangalia vijana na wanawake kwa kuangalia nini ambacho tumefanikiwa katika awamu hii ya Rais Kikwete. Tutaangalia mageuzi tutakayoyafanya ili kijana wa Kitanzania aonekane si mzigo,” alisema.
Alisema endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo, serikali yake itajikita katika kuinua uchumi wa nchi.
“Tutajikita katika kuwekeza katika rasilimali watu, kuwawezesha wananchi kiuchumi… na sisi wenyewe kama Taifa tutasimama kwa miguu yetu. Tutatembea vichwa vikiwa vimesimama imara tuishangaze dunia kwa pamoja,” alisema.
Jambo jingine ni kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na uwezo wa kujilinda na raia wake.
“Tutaendelea kuhakikisha mifumo ya matatizo ikiwa ni pamoja na magonjwa, tatizo la Ukimwi, mshtuko wa ebola tulioupata ambao ulitetemesha utalii duniani, changamoto za kigaidi, tutajipanga kama Taifa na kama umoja kuhakikisha tunakabiliana nazo,” alisema.

Nyalandu alisema njia bora ya kuwawezesha watu ni kuboresha mfumo wa elimu ambao umefanikiwa chini ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Alisema  endapo atafanikiwa katika safari yake hiyo ya kuutafuta urais, atahakikisha kila shule ya msingi na sekondari inakuwa na kitengo cha mafunzo stadi.
Alipoulizwa iwapo chama kingine cha siasa kitashinda upande wa pili wa Muungano, alisema: “Ni muungano wa mapenzi ya ndani, ni muungano ambao unazidi tofauti zetu za dini, kabila na uwepo wa Bara na Visiwani na hali kadhalika, unazidi tofauti zetu za itikadi za vyama.”
Alisema atashirikiana na viongozi wa Zanzibar katika kuuenzi Muungano wa Tanzania ili uwe ishara ya amani na mshikamano.
Mulenda: Kipaumbele ni elimu bora
Mulenda (41) amechukua fomu ya kuwania kuteuliwa na chama chake kugombea urais huku akisema kipaumbele chake cha kwanza ni elimu bora.
Kada huyo ambaye alisindikizwa na watu wasiozidi sita, alisema kaulimbiu yake ni Serikali sikivu, makini na inayojali shida za watu.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi za Makao Makuu ya CCM, Mulenda alisema amejitathmini na kujipima kuwa anaweza kuwa kiongozi wa Tanzania. Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuhakikisha CCM inakuwa imara zaidi.
“Kwa upande wa chama nitahakikisha  nasimamia kwa vitendo katiba ya chama, kanuni na taratibu bila kuacha sheria na miongozo inayoongoza nchi yetu,” alisema.
Alisema atasimamia uamuzi wa vikao na kuhakikisha unatekelezwa na kupima matokeo kwa kufanya tathmini juu ya malengo waliyojiwekea.
Mulenda alisema endapo atashinda na CCM ikawa ndicho chama tawala, atakuwa na kazi ya kuisimamia Serikali.
“Ukiona Serikali inafanya vibaya na chama kinachotawala kinaona sawasawa, basi siku za kukaa madarakani za chama hicho zinahesabika,” alisema.
Alisema endapo atafanikiwa katika safari yake hiyo, atahakikisha Serikali yake kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM inakuwa sikivu, makini na inayojali shida za watu.
“Nawahakikishia wananchi kuwa kwa kutambua shida zao ni dhahiri nitajua wanataka nini na hawataki nini na kwa msingi huo, Serikali itakayokuwa chini yangu wakati wote tunahakikisha Watanzania tunawapeleka kule wanakotarajia kwa kutumia uwezo wetu ambao ulijengwa na waasisi wa Taifa hili,” alisema.
Alisema wazee waliwaambia kuwa nchi ina raslimali za kutosha na kinachotakiwa ni kujiongoza ili kutumia amani na utulivu kujenga nchi.

Hakuna maoni: