ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 29 Mei 2015

Midahalo ya watangaza nia CCM sasa ruksa

07 June 2015

By Stella Nyemenohi, Bukoba

WATANZANIA sasa watapata fursa pana zaidi ya kufahamu kwa undani wanachama wa CCM waliotangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, baada ya Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, kuridhia midahalo kwa wanachama hao.
Akizungumza katika ziara ya siku 28 ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuzungumza na Watanzania katika mikoa ya Kanda ya Ziwa jana, Kinana alisema hakuna kipingamizi kwa watangaza nia hao kwenda katika midahalo.
“Wanachama wetu wamealikwa kwenye midahalo, sasa wamenipigia simu na kuniuliza twende ama tusiende. Jibu langu hiari yao kwenda na ni hiari yao kutokwenda, kwa hiyo wana uhuru wa kwenda.
“Hawa walipotangaza nia walisema mengi sana, ni sawa sawa na mdahalo mwingine, walipochukua fomu walikutana na waandishi wa habari walisema mengi sana, huo nao ni mdahalo mwingine, huko wanakopita kupata wadhamini, wanasema mengi nayo ni midahalo, kwa nini sisi tukatae mdahalo ambao watu wameomba?
“Walialikwa kwa barua, wakanipigia wakasema wameshakubali waende wasiende, nimewaambia ruksa nenda wakitaka, lakini CCM haiandai mdahalo, CCM haimtumi mtu na CCM haimnyimi mtu, hiari ni yao,” alisema Kinana.
Uamuzi huo wa Kinana umekuja siku moja baada ya kutolewa kwa taarifa ya katazo kwa watangaza nia hao kushiriki katika midahalo hiyo.
Katazo hilo lilitolewa juzi na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ya Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib, ambaye alisema chama hicho hakiruhusu midahalo kwa makada wake hao, kwa kuwa hakina mgombea mpaka sasa.
Nafasi ya Watanzania Akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa midahalo kwa watangaza nia hao, Kinana ambaye ameshazungumza mara nyingi kuwa nafasi ya urais ni kubwa, hivyo kunahitajika umakini kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete, alisema ni vizuri wanaCCM na Watanzania watumie midahalo hiyo kupima watangaza nia hao.
“Hawa wanaoomba nafasi kupitia CCM, nafasi wanayoomba ni kuongoza Watanzania, kwa hiyo kama kuna mdahalo utakaosaidia watu kujibu maswali, kueleza sera zao na kutoa ufafanuzi kwa masuala mbalimbali, wanachama wa CCM wakapima vizuri zaidi na wananchi wakatumia nafasi hiyo kupima na kuwaelewa vizuri zaidi, hakuna ubaya.
“Lengo la mdahalo iwe kwa Watanzania kufahamu wagombea vizuri zaidi, kufahamu sera zao, kuwapima vizuri zaidi uwezo wao wa kujenga hoja,” alisisitiza.
Hadhari Hata hivyo, Kinana hakuacha kutoa hadhari kwa waandaaji wa midahalo na kuwaomba waandae midahalo hiyo kwa kuzingatia haki ili lengo liwe kutoa fursa kwa wana CCM na Watanzania, ya kuwafahamu na kuwaelewa zaidi wagombea hao na kamwe isiwe sababu ya kujenga mifarakano isiyo na sababu.
Maandalizi Kwa hatua hiyo ya Kinana, sasa Taasisi ya CEO Round Table Tanzania (CEOrt), iliyoandaa midahalo hiyo, itaendelea na ratiba yake kesho kwa watangaza nia sita wa kwanza waliothibitisha kushiriki.
Kwa mujibu wa taarifa za CEOrt zilizotolewa mwishoni mwa wiki, watangaza nia waliothibitisha kushiriki ni sita na mdahalo huo utafanyika mara tatu, mara ya pili ukihusisha watangaza nia wa vyama vya upinzani hasa kutoka muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD na mara ya tatu utahusu watangaza nia wengine kutoka CCM.
Watangaza nia watakaoanza kesho katika mdahalo utakaorushwa moja kwa moja na luninga mbalimbali za hapa nchini, utawahusisha aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye na mmoja wa wanadiplomasia wakubwa nchini ambaye pia ndiye mwanamke pekee, Balozi Amina Salum Ali.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Tekinolojia, January Makamba; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Hoja kiongozi Akizungumza kuhusu mdahalo huo katika redio ya Clouds FM mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CEOrt, Ali Mufuruki alisema mdahalo huo utakuwa na muongoza mdahalo (moderator) na kutakuwa na maswali ambayo watangaza nia hao watayajibu.
Mbali na maswali hayo yatakayotokana na hoja mbili mahususi; mosi kipaumbele chao cha uchumi katika kipindi cha mwaka 2015 mpaka 2020 na pili mikakati yao katika jitihada za kuhakikisha kunakuwepo utawala bora na kushinda vita dhidi ya rushwa, moderator huyo atakuwa na fursa ya kuuliza maswali zaidi, ili kupata ufafanuzi wa kina kutoka kwao.
Licha ya hoja hizo mbili mahususi, pia watangaza nia hao wanatarajiwa kuzungumza kuhusu malengo yao ya muda mrefu yatakayoleta maendeleo na kutunza utajiri wa maliasili ya Tanzania.
Pia walitarajiwa watoe maoni yao kuhusu dira zao, mikakati na jitihada za kuipeleka Tanzania katika mambo muhimu yatakayoharakisha uchumi wa muda mrefu.
Washiriki wa mdahalo huo kwa mujibu wa Mufuruki, ni watu mbalimbali kutoka sekta binafsi na katika umma wa Watanzania kwa ujumla, lakini watatakiwa kulipia kiingilio cha Sh 100,000.
Kwa mujibu wa Mufuruki, mpaka mwishoni mwa wiki kulikuwa na kasi nzuri ya washiriki waliokuwa wamekwishalipia kiingilio na wengine wakiwasiliana na waandaaji kwa ajili ya kulipa kiingilio, ambapo alihadharisha kuwa nafasi ni chache kwa kuwa ukumbi wa mjadala unachukua watu wasiozidi 300.
Waliochukua fomu Mpaka jana wana CCM 14 walikuwa wamechukua fomu, baada ya watatu kuchukua juzi na mmoja jana, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba. Mwanachama Mussa Godwin Mwapango naye alitarajiwa kuchukua fomu jana.
Waliochukua juzi ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani. Wanachama wengine 10 walichukua kuanzia Jumatano iliyopita ambayo ilikuwa siku ya kwanza ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira.
Wengine ni Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Marekani, Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere ambaye ni mtoto wa Mwalimu Nyerere.
Pia mawaziri wakuu wa zamani Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal, Balozi mstaafu Ali Abeid Karume - mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume na Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli, Mussa Godwin Mwapango.
Waliokwisha kutangaza nia ambao hawajachukua fomu ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba, wabunge William Ngeleja (Sengerema), Dk Hamis Kigwangalla (Nzega) na Luhaga Mpina (Kisesa).
(source habari leo)

 




Hakuna maoni: