Kwa ufupi
Kwa mara ya kwanza, CCM inakabiliwa na kazi ngumu ya
kuamua hatima ya makada iliowafungiwa katika kipindi muhimu cha kuteua
mgombea mpya wa urais kutokana na mwenyekiti wa sasa wa chama hicho,
Jakaya Kikwete kutoweza kugombea nafasi hiyo kwa kipindi cha tatu
kutokana na matakwa ya kikatiba.
Kwa mara ya kwanza, CCM inakabiliwa na kazi ngumu
ya kuamua hatima ya makada iliowafungiwa katika kipindi muhimu cha
kuteua mgombea mpya wa urais kutokana na mwenyekiti wa sasa wa chama
hicho, Jakaya Kikwete kutoweza kugombea nafasi hiyo kwa kipindi cha tatu
kutokana na matakwa ya kikatiba.
Mmoja wa watu walio karibu na uongozi wa chama
hicho aliiambia Mwananchi jana kuwa CCM imejikita zaidi katika kutafuta
mwanachama atakayekipa ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu, lakini suala la
makada waliofungiwa ambao baadhi yao wanapewa nafasi kubwa ya
kupitishwa, halitachukua muda mrefu kulijadili.
Kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa
Halmashauri Kuu uliopo jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa, maarufu
kama White House mjini Dodoma.
Ukumbi huo una historia ya muda mrefu ndani ya CCM
ya kutolewa kwa uamuzi mgumu katika matukio kadhaa ya kisiasa, ukiwamo
ule ulioweka historia ya Aboud Jumbe kuingia akiwa Rais wa Zanzibar na
mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, lakini akatoka bila cheo chochote
mwaka 1984.
Pia kwenye ukumbi huo kulifanyika uamuzi wa mambo
mengine makubwa, hasa nyakati za kuchuja wagombea urais au uongozi wa
chama, mambo ambayo pia yanaweza kutokea katika vikao vinavyoanza leo au
vya baadaye.
Alipoulizwa kuhusu kikao hicho jana, katibu wa
itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Rais Kikwete ataongoza
kikao cha leo kilichopangwa kuanzia saa 4:00 asubuhi na kwamba
maandalizi yamekamilika, huku baadhi ya wajumbe wakiwa wameshawasili.
Alipoulizwa kuhusu nini wategemee wanachama na
wananchi, Nape alijibu kwa kifupi kuwa watarajie kuwa “CCM watatoka
wakiwa kitu kimoja” kuliko inavyotarajiwa na wengi.
Hata hivyo, mbali na hofu kuhusu hatua za
kinidhamu kwa wajumbe walioadhibiwa kwa kuanza kampeni mapema na kukiuka
maadili, taarifa nyingine kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa vikao hivyo
zilidai kuwa mkutano huo utajikita zaidi kuangalia utaratibu mzima wa
kuchukua fomu za wagombea wote wa urais, ubunge na udiwani.
“Vikao hivi vinaangalia utaratibu tu wa jinsi ya
kuchukua fomu na wala havitagusia suala la mchujo wa wagombea urais wala
ubunge,” alisema mtoa taarifa huyo.
Kamati Kuu imetanguliwa na vikao vya mfululizo vya Sekretarieti na Kamati ndogo ya Kanuni.
Kamati ya Kanuni na Maadili ilitarajiwa kukutana jana usiku au leo asubuhi kabla ya Kamati Kuu
Mtoa taarifa mwingine ambaye ni mjumbe wa NEC, alidokeza kuwa
vikao hivyo havitajikita sana na uchujaji wa majina ya wagombea urais,
badala yake kwa kuwa muda umekwenda, wameamua kushughulikia ratiba kwa
ajili ya uchukuaji wa fomu za wagombea wa ngazi zote za uchaguzi ili nao
wapate muda wa kwenda kutafuta wadhamini kabla ya mchujo.
Hata hivyo, mtoa habari mwingine kutoka ndani ya
CCM, alisema licha ya kushughulikia masuala ya ratiba, kanuni na
kuangalia ilani, bado suala la mchujo wa wagombea ni tata na huenda
wakaangalia mgombea ambaye anaweza kukipa ushindi chama kwenye Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, hoja ya watangaza
nia sita ya kukiuka kanuni za chama haitakipotezea muda, zaidi ya
kuangalia nani anaweza kukipa chama ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba.
Taarifa za ndani kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa
vikao hivyo vya juu vya CCM alidokeza kuwa kwa hali ya sasa ya kisiasa
na joto linavyozidi kupanda hasa kasi ya Ukawa, CCM itafanya kama
ilivyofanya kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 wakati Kamati ya Usalama
na Maadili ilipokwenda Zanzibar ikiwa na faili la tuhuma za mmoja wa
wagombea, lakini vikao vilijikita kwenye mgombea ambaye angekipa ushindi
chama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mambo mengi hasa
malalamiko ya ukiukwaji wa maadili wa baadhi ya viongozi ngazi za chini,
yatamalizwa na Kamati Kuu na yale yatakayohitaji uamuzi wa mamlaka za
uteuzi yatapelekwa Halmashauri Kuu.
Mtoa taarifa huyo alisema suala la Mkuu wa Wilaya
ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Paul Makonda na makada wawili CCM,
Mgana Msindai ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho mkoani Singida, na
John Guninita, ambao wamefungua kesi ya madai mahakamani, linaweza
kuibua mjadala.
Hivi karibuni Nape alikaririwa akisema kuwa chama
hicho katika kushughulikia matatizo yote yaliyojitokeza kitatumia kanuni
zake na hakuna atakayeonewa.
“Nasisitiza ni kanuni na wala si mimi, nasisitiza pia kuwa sijazuia watu kuchukua fomu bali chama kinafuata kanuni,” alisema.
Alisema kada yeyote wa CCM akiamua kufanya kampeni
kabla ya muda ataadhibiwa, lakini akisubiri hana hatia kwani
kinachongomba ni kanuni.
Maelezo hayo ya Nape yalikuwa yanalenga uamuzi wa
Kamati Kuu ya CCM kuwafungia kwa miezi 12 vigogo wa chama hicho
uliotolewa Februari mwaka jana kwa kuanza kampeni kabla ya wakati na
kikiuka maadili ya chama.
Wakati huo huo, hoteli na nyumba za kulala wageni
zimejaa na hiyo kufanya baadhi ya wageni wanaoingia mkoani hapa
kulazimika kutafuta malazi nje ya mji.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa wa nyumba za
kulala wageni katikati ya mji umebaini kuwa wageni waliojaza nyumba hizo
ni wajumbe na wapambe.(Source Mwananchi)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni