Na Online Team, Mwananchi
Posted Jumanne,Mei5 2015 saa 8:24 AM
Posted Jumanne,Mei5 2015 saa 8:24 AM
Kwa ufupi
Mgomo huo ulioanza jana umesababisha usumbufu mkubwa
kwa raia sehemu nyingi nchini Tanzania ambao walikuwa wamejiandaa
kusafiri kuelekea katika mikoa mingine jana na leo kwa ajili ya shughuli
zao mbalimbali zikiwemo za kibiashara na kijamii.
Hatimaye madereva wa mabasi na malori wameamua
kusitisha mgomo leo baada ya Serikali kuwahakikishia kuwa inaandaa
utaratibu mzuri wa kujibu na kushughulikia matatizo yao.
Mgomo huo ulioanza jana umesababisha usumbufu
mkubwa kwa raia sehemu nyingi nchini Tanzania ambao walikuwa wamejiandaa
kusafiri kuelekea katika mikoa mingine jana na leo kwa ajili ya
shughuli zao mbalimbali zikiwemo za kibiashara na kijamii.
Taarifa zilizotufikia ni kwamba Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni Paul Makonda akiwa na viongozi wengine wa Serikali walifika
katika kituo cha mabasi yaendao mikoani cha ubungo na kuzungumza na
madereva hao wakiwataka wasitishe mgomo wao na kuanza kazi kwani mambo
yao Serikali inayafanyia kazi na hivi karibuni watajibiwa.
Kufuatia hali hiyo maderva hao walikubaliana na
ombi hilo la Serikali baada ya kutokea kwa Mwenyekiti wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo Freeman Mbowe ambaye naye aliwasihi waache mgomo
huo kwani Serikali itafanyia kazi maombi yao.
Nchi yasimama: Madereva mabasi, malori wagoma sehemu kubwa ya Tanzania
Dar/mikoani. Nchi imesimama. Hii ndiyo sentensi
inayofaa kuelezea tukio la jana la mgomo wa madereva nchini kote ambao
kwa mara ya kwanza ulisababisha mabasi yote kutoka Dar es Salaam kwenda
mikoani na nchi jirani kushindwa kuondoka.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT), kushindwa kutoa huduma kwa sababu yoyote ile.
Tangu asubuhi hadi jioni, hakuna basi hata moja
lililotoka wala kuingia katika kituo hicho hadi abiria walipoanza kukata
tamaa na baadhi yao kuondoka na wengine kuanza kushinikiza kurejeshewa
nauli.
Mgomo huo ambao ni mwendelezo wa ule uliofanyika
Aprili 9, mwaka huu ulipewa uzito na madereva hao baada ya ahadi
walizopewa na Serikali kutofanyiwa kazi kama ilivyoahidiwa na Waziri wa
Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda kamati ya
iliyotangazwa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta ya kusimamia usafiri
barabarani itakayowakutanisha wadau wote ili kutatua matatizo katika
sekta hiyo kila yanapotokea.
Polisi wachemsha Dar
Tangu saa 2.30 asubuhi, polisi walijaribu
kuyasindikiza mabasi waliyodhani madereva wake wako tayari kuondoka
Ubungo lakini walishindwa baada ya kutoungwa mkono.
Mkuu wa Trafiki Ubungo, Inspekta Yussuf Kamotta
akiwa na Inspekta Solomon Nkindwa ambaye pia ni mkaguzi wa magari,
waliingia katika basi la Kampuni ya Master City na kuliondoa kituoni
hapo wakiwa na mmiliki wa kampuni hiyo, Abdallah Mohammed huku
wakimtafuta dereva bila mafanikio na kulazimika kulitafutia sehemu
salama ya kuliegesha baada ya madereva kulizingira.
Kitendo cha askari hao kilisababisha kuzomewa kwa
Inspekta Nkindwa wakisema mkaguzi huyo arudi shule akasome...
“Solomoooon… rudi shuuuule… gia nane… zimekushinda,” walisikika madereva
hao wakiimba huku wakikimbia mchakamchaka kurudi zilipo ofisi zao.
Kutokana na vurugu zilizotokea nje ya kituo hicho,
polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu
waliokuwa katika makundi.
Nje ya UBT, magari sita ya polisi yaliegeshwa
katika makutano ya barabara za Sam Nujoma, Nelson Mandela na Morogoro
wakati mengine yakielekea Mwenge na Buguruni kwenda kukabiliana na
tishio lolote ambalo lingeweza kutokea.
Saa 5.30 askari wa Kikosi cha Mbwa waliwasili
kuongeza nguvu na kuvutia macho ya wengi kutokana na jinsi walivyokuwa
na pilikapilika bila ya kuwapo kwa mhalifu yeyote anayetafutwa.
Sikukuu ya madereva
Tofauti na migomo mingine, huu haukuwa na vurugu
zozote wala sintofahamu kwani kila mtu aliyekuwa UBT alionekana akiwa
katika sehemu yake akiendelea na hamsini zake. Abiria walikuwa katika
mabasi husika huku mawakala na makarani wakiendelea kukatisha tiketi za
safari na kupanga mizigo ya abiria.
Huku wakiendelea na mazungumzo yao katika vikundi
katika kituo hicho, madereva hao walisikia wakisema hapakuwa na mgomo,
bali sikukuu yao.(CHANZO MWANANCHI)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni