USAJILI: Simon Msuva aiangukia Yanga
Na Khatimu Naheka na Iman Makongoro,
Kwa ufupi
- Ukiacha Nonda Shaaban ‘Papii’, hakuna mchezaji mwingine aliyefanikiwa kung’ara au kuuzwa nje ya nchi akitokea Yanga.
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa
Yanga, Simon Msuva amereja nchini akitokea Afrika Kusini kufanya
majaribio ya soka la kulipwa na amewaangukia viongozi wake kutofanya
makosa ya kuzuia uhamisho wake.
Msuva mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara,
katikati ya wiki iliyopita alitoroka na kwenda Afrika Kusini kufanya
majaribio katika klabu ya Bidvetes Wits inayoshika nafasi ya tatu katika
msimamo wa Ligi Kuu nchini humo ikiwa na pointi 52 juu ya Mamelodi
Sundowns 57 na vinara Kaizer Chiefs wenye pointi 69.
Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kuwasili
juzi, Msuva alisema amefanikiwa kuandika historia katika maisha yake ya
soka kwa kufanya majaribio katika klabu ya Wits na sasa anasubiri majibu
ya majaribio hayo kabla ya kuanza mchakato wa uhamisho.
Msuva ambaye amefunga mabao 17 katika Ligi Kuu
msimu huu alisema anauomba uongozi wa klabu yake chini ya mwenyekiti
Yusuf Manji kutoweka ugumu katika uhamisho huo badala yake wafanye
taratibu nyepesi ili aweze kucheza soka nje ya Tanzania.
“Unajua haya ni maisha na hii ni nafasi yangu ya
pekee niliyopata, nashukuru kila kitu kilienda sawa, ombi langu kwa
uongozi ni kunisaidia nikamilishe ndoto yangu,”alisema Msuva.
“Uongozi ningeuomba endapo hawa jamaa (Wits)
watakuja kuanza mchakato wa usajili wasiwe na tamaa ya fedha kwa kutaja
kiasi kikubwa ambacho kitakwamisha uhamisho wangu.”
Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha
alilithibitishia gazeti hili jana kuwa hawana mpango wa kumuwekea
vikwazo Msuva huku akibainisha kuwa wanachohitaji ni taratibu zifuatwe
ingawa hadi jana mchana hakuna kiongozi wala wakala wa klabu ya Bidvest
aliyewafuata.
“Kama kweli wana nia na Msuva, tuko tayari
kumwachia akatafute maisha mengine ya soka nje ya nchi, madai kuwa tuna
mpango wa kuweka dau kubwa ili kumkomoa si kweli, tutaweka dau ambalo
kwetu tunaona ndilo linafaa kumuuza Msuva,” alisema katibu huyo.
“Kama timu inayomtaka itashindwa dau letu basi
haimuhitaji, mbona kuna wachezaji wanauzwa hadi dola milioni moja, dola
laki saba na kuendelea? Hivyo Msuva ‘akithitibisha’ anaweza, fedha
tunayoitaka haitakuwa ya kushtua,” alisema Tiboroha bila kubainisha ni
kiasi gani.
Tiboroha alisema walitarajia kukutana na Msuva jana jioni ili kujua hatma yake endapo anaondoka Yanga au la.
Yanga imekuwa na tabia ya kuwazuia wachezaji wake
wanapotakiwa na klabu mbalimbali nje ya nchi, ilishafanya hivyo kwa
Jerryson Tegete na Mrisho Ngassa na Haruna Niyonzima.
Mwaka 2009, Ngassa alitakiwa bila ya kufanya
majaribio katika klabu ya Lov-Ham ya Norway kwa gharama ya Dola za
Marekani 50,000, lakini Yanga walisema klabu yao ni kubwa ambayo haina
shida na ina uwezo wa kuwalea wachezaji wake na ndiyo maana haipo tayari
kuwauza nyota wake kwa bei rahisi na pengine wangelipwa zaidi ya Dola
za Marekani 100,000 wangeweza kumwachia.(Mwananchi)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni