ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 13 Mei 2015

NEC sasa yaanza kugawa majimbo


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza rasmi mchakato wa kugawa majimbo ya uchaguzi nchini ambapo inatarajia kuanza uchunguzi wa mipaka ya majimbo hayo hivi karibuni, ikiwa ni hatua ya maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Aidha, tume hiyo imesisitiza kuwa uchaguzi mkuu lazima ufanyike Oktoba mwaka huu, kwa mujibu wa Katiba, na kufafanua kuwa kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji wapigakura kwenye daftari la wapigakura, uandikishaji huo unatarajiwa kukamilika Julai mwishoni au Agosti mwanzoni mwaka huu.
Akifungua mkutano baina ya tume hiyo na vyama vya siasa jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Damian Lubuva, alisema uchaguzi na mgawanyo huo wa majimbo unafanyika chini ya Katiba ya sasa ya mwaka 1977.
“Tume inapenda kuwahakikishia kuwa ugawaji huu wa majimbo utakamilika kwa wakati na wananchi watajulishwa ili vyama vya siasa viweze kuteua wagombea katika majimbo hayo,” alisisitiza Jaji Lubuva.
Alisema kwa sasa utaratibu wa kuandikisha wananchi kwenye daftari hilo la kudumu la wapigakura unaendelea vizuri na Serikali imeshatoa fedha zote za ununuzi wa vifaa vya kuandikishia zikiwemo BVR kits.
Alisema hadi sasa jumla ya BVR 4,800 zimeshawasili na zinaendelea kutumika katika uandikishiaji na Mei 20, mwaka huu BVR kits 1,600 zinatarajiwa kuwasili na Mei 29, mwaka huu pia BVR 1,520 zitawasili kwa ajili ya uandikishaji.
Alisema ratiba ya uandikishaji tayari imeshatoka na kwamba kwa sasa tume hiyo inaendelea kuandikisha ambapo Mei 19, mwaka huu tume hiyo itaandikisha wananchi wa mikoa ya Singida, Tabora, Igoma na Kagera na kufuatiwa na mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Simiyu.
Aidha pia ratiba hiyo inaonesha baada ya mikoa hiyo, uandikishaji utaendelea katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Zanzibar na kumalizikia mkoani Dar es Salaam.
Naye Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alitaja vigezo vitakavyotumika kugawa jimbo kuwa ni mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu ambao utazingatia takwimu za idadi ya watu kutoka Ofisi ya Takwimu (NBS) na idadi ya majimbo ambayo kwa sasa ni 239.
“Kwa mujibu wa makadirio ya ofisi ya takwimu Watanzania wote Tanzania bara wamefikia milioni 47.1, kwa upande wa majimbo ya mjini yana watu takribani milioni 10 na vijijini watu milioni 37,” alisema Malaba.
Alisema kutokana na takwimu hizo, mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu kwa majimbo ya mjini utazingatia watu 325,000 na kwa upande wa majimbo ya vijijini wastani utakuwa ni watu 250,000, hivyo majimbo yatakayogawanywa ni yale yenye idadi ya watu zaidi ya mgawanyo huo.
Alitaja vigezo kingine kuwa ni upatikanaji wa mawasiliano kama vile barabara, simu na vyombo vya habari, hali ya kijiografia kwa mfano maeneo ya mlimani, visiwani au mabondeni ni kigezo kingine cha mgawanyo wa jimbo pamoja na hali ya uchumi.
Kigezo kingine ni ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja lisiwe ndani ya wilaya au halmashauri mbili ambapo endapo kwa sasa zipo wilaya au halmashauri zilizogawanywa, tayari zimeshatoa mgawanyo wa majimbo.
Aidha kigezo kingine ni kata moja isiwe ndani ya majimbo mawili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, mazingira ya muungano, uwezo wa ukumbi wa Bunge na viti maalum vya wanawake ambavyo kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya mwaka 1977 imetenga zaidi ya asilimia 30 ya viti vya ubunge kwa ajili ya wanawake.
Alisema tume hiyo inatarajia kukutana na wadau na kujadiliana juu ya vigezo na utaratibu utakaotumika kuchunguza mipaka na kugawa majimbo, kupokea maombi na mapendekezo ya kugawa, kurekebisha mipaka au kubadili majina ya majimbo kutoka kwa wadau na kuainisha maombi hayo.
Malaba alisema tume hiyo imeweka utaratibu wa wadau kuwasilisha maombi ya kurekebisha mipaka na kugawa majimbo au kubadili majina ya majimbo ambayo yatawasilishwa kwa mkurugenzi wa halmashauri husika na kujadiliwa na vikao rasmi.
“Mkurugenzi atawasilisha maombi au mapendekezo hayo kwa Katibu Tawala wa Mkoa, ambaye atayawasilisha katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ili kupata maoni zaidi na mwisho Katibu Tawala wa Mkoa atawasilisha maoni hayo kwa NEC,” alisisitiza.
Kwa upande wake Kamishna wa Tume, Profesa Amone Chaligha, alisema tume hiyo inatarajia kutoa ratiba kamili ya ugawaji wa majimbio hayo na matangazo yake kesho ili suala hilo, litekelezwe mapema iwezekanavyo.
Nao wawakilishi wa vyama vya siasa, akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, na Mwenyekiti wa chama cha NLD, waliitaka tume hiyo, kuweka wazi ratiba zote zinazoendana na mchakato wa uchaguzi, ili vyama hivyo vijiandae vyema.(HABARI LEO)

Hakuna maoni: