ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 16 Mei 2015

SHULE ZA KIDATO CHA TANO ZIONGEZWE-RAIS

RAIS Jakaya Kikwete ameagiza Wakuu wa Mikoa na Maofisa Elimu wote nchini, kuanza ujenzi wa shule maalumu za kidato cha tano na sita kwa kila kata na wakishindwa, katika shule za sekondari za kata, wachague baadhi na kujenga madarasa ya vidato hivyo.

Alitoa agizo hilo jana katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, yaliyoadhimishwa kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na kuwakumbusha kuwa kati ya wanafunzi waliofaulu kwenda kidato cha tano mwaka huu, ni asilimia 75 tu walioendelea na masomo hayo.

“Wakuu wa mikoa na maofisa elimu mliopo hapa naagiza na hili ni kwa nchi nzima, tuanze utaratibu wa kuwa na shule za kidato cha tano na sita za kata. Mnaweza kujenga shule mpya, au mchague baadhi ya sekondari za kata ziwe na kidato cha tano na sita,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kusema si vyema kuwaacha mtaani asilimia 25 wenye sifa ya kuingia kidato cha tano.

Alisema bila kuchukua hatua hiyo, Tanzania inaweza kurudi katika hali ya elimu aliyoikuta ambapo wanafunzi wenye sifa ya kuendelea na masomo, waliachwa kutokana na ufinyu wa nafasi za kuendelea na elimu.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakati alipokuwa akiingia madarakani, alikuta asilimia sita tu ya wanafunzi waliokuwa wamefanya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, ndio waliokuwa wakichaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari.

“Leo kila anayefaulu darasa la saba, anakwenda sekondari… tukisema leo mwanafunzi amefeli darasa la saba amefeli kweli tofauti na zamani ambapo walikuwa wakichaguliwa,” alisema Rais Kikwete.

Tanzania ilipotoka Rais Kikwete alielezea sababu ya Serikali inayomaliza muda wake kuwekeza zaidi katika elimu, kiasi kwamba bajeti ya elimu katika Mwaka wa Fedha unaoisha kuwa kubwa kuliko ya sekta zingine, inayofikia Sh trilioni 3.4 kutoka Sh bilioni 600 iliyokuwepo mwaka 2005.

Sababu ya kwanza Rais Kikwete alisema, waliona kuwa kuwekeza katika elimu ndio kuwekeza katika taifa na Serikali isingechukua uamuzi huo, Watanzania hawataweza kutawala mazingira yao na kutumia vizuri rasilimali zao.

Pili alisema alipoingia madarakani, alikuta Tanzania yenye watu wengi zaidi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iko nyuma ikilinganishwa na Kenya na Uganda, kwa idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za sekondari na vyuo.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mwaka 2005 wanafunzi waliokuwa wakisoma sekondari ni zaidi ya 500,000, wakati nchini Uganda waliokuwa wakisoma sekondari walikuwa zaidi ya 700,000 na Kenya zaidi ya 900,000.

Kwa upande wa vyuo vikuu, Tanzania ilikuwa na wanafunzi 40,000 tu wakati Uganda ilikuwa na wanafunzi 124,000 na Kenya 180,000.

“Kuwa nyuma katika kutoa fursa ya elimu ikilinganishwa na wenzetu ilikuwa inaweka nchi yetu katika mazingira mabaya katika ushindani wa soko la ajira la Afrika Mashariki,” alisema Rais Kikwete.

Mbali na mazingira mabaya katika ushindani wa soko la Afrika Mashariki, Rais Kikwete alisema Watanzania nao walifikia hatua ya kuamua kupeleka watoto wao kwenda kusoma Kenya na Uganda.

Hatua zilizochukuliwa, Rais Kikwete alisema Serikali kwa kushirikiana na wananchi, waliamua kujenga shule za sekondari za kata, ambapo wananchi walihamasishwa, wakahamasika wakajenga shule mpaka Mkurugenzi mmoja wa elimu, akahofia kukosa walimu wa kupeleka katika shule hizo.

“Tulihimiza wadau wengine wajenge vyuo vya elimu ya juu na kuamua mikopo ya elimu ya juu itolewe kwa wanafunzi wa vyuo vyote,” alisema Rais Kikwete.

Alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina wanafunzi 1,800,000 wanaosoma sekondari na imeshaipita Uganda yenye wanafunzi 1,700,000 wanaosoma elimu ya sekondari, lakini imezidiwa na Kenya ambayo ina wanafunzi 2,100,000.

Hata hivyo alisema ni rahisi kuipita Kenya kwa hilo pengo la wanafunzi 300,000, kwa kuwa shule za sekondari zilizopo zina nafasi ya kuongeza wanafunzi milioni mbili zaidi.


“Hapa lazima tuwafukuzie Wakenya, lazima tuwakute na kuwapita na huu ni ushindani mzuri kwa kuwa ni ushindani wa maendeleo,” alisema Rais Kikwete.

Kwa upande wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema vyuo vikuu vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.


Chanzo:
Habari Leo

Hakuna maoni: