ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 13 Aprili 2016

Kutenguliwa Anne Kilango kwaendelea kuwa gumzo

KUTENGULIWA kwa uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela kumeendelea kuwa gumzo huku viongozi wengine wakiambiwa wawe macho kwa kuchukulia uamuzi huo wa Rais Magufuli, kama funzo la kutambua aina ya uongozi anaoutaka katika Serikali yake ya Awamu ya Tano.
Wakati viongozi hususani wa kuteuliwa wakitakiwa kuzingatia ukweli kwamba serikali ya awamu hii haihitaji wanaoficha mabaya wakitaka mazuri ndiyo yaonekane, baadhi wameshauri mfumo uliopo, hususani wa kupeana taarifa uangaliwe kwa kuwa una tatizo linalohitaji kufanyiwa kazi.
Miongoni mwa watu ambao gazeti hili lilizungumza nao jana kuhusu hatua hiyo ya Rais kutengua uteuzi wa Kilango, ni mwanasiasa mkongwe nchini, Paul Kimiti aliyetaka viongozi wengine kutambua kwamba, Magufuli ni kiongozi asiyependa unafiki.
“Uongozi wake tangu mwanzo umejidhihirisha wazi kuwa ni kiongozi anayependa uwazi na ukweli hataki short cut (njia za mkato),” alisema Kimiti. Kimiti aliyewahi kushika uwaziri katika Serikali zilizopita, alisema hatua hiyo ya Rais ni ishara na funzo kwa viongozi wengine hasa wale walio madarakani kuhakikisha kuwa wanawajibika ipasavyo kwa kufuata misingi ya uwazi na kutokimbilia njia za mkato.
Alisema kwa hali ilivyo, ni vyema viongozi waliopo wakaanza kufuata heshima na taratibu za kiongozi aliyewaweka madarakani, hali ambayo itawasaidia kutowajibishwa.
Mwanasiasa huyo ambaye alionesha kuguswa kwa mtazamo chanya na hatua anazochukua Rais, alisema kumekuwa na utaratibu wa watendaji kutoa taarifa zisizo sahihi na zisizo kamili kwa wakuu wao wa kazi kwa lengo la kuonesha kuwa mambo ni mazuri.
Alisema jambo hilo ni tatizo kubwa linalopaswa kukemewa. Utendaji wa kujikomba “Hii ni kero kubwa, watendaji wengi wanaficha taarifa za ukweli kwa wakuu wao ili kuonesha mambo ni mazuri, hili ni jambo baya kabisa kwani matokeo yake ndiyo haya; anakuja kuwajibishwa mtu mwingine ambaye huenda hakuhusika na taarifa hizo,” alisisitiza.
Alisema utendaji wa aina hiyo ni sawa na utendaji wa kujikomba ambao hauna tija, kwani pamoja na kuficha ukweli na uhalisia wa mambo, mwisho wake siku wananchi ndio waathirika na baadaye ukweli hufichuka.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja alisema kilichotokea ni funzo kubwa kwa viongozi wengine kuhakikisha kuwa kila taarifa wanayopatiwa lazima wanaifanyia kazi na kujiridhisha kabla ya kuitoa kwa umma.
“Mama Kilango kwa vyovyote vile bado ndio alikuwa anaanza kazi ya ukuu wa mkoa, hivyo lazima atakuwa amepatiwa taarifa aliyoitoa kwa umma na watendaji wake. Hii ilikuwa ni kawaida, viongozi wengi huuamini mfumo unaowapatia taarifa,” alisema Semboja.
Hata hivyo, alisema kiongozi huyo alipaswa baada ya kupatiwa taarifa ya awali, angewasiliana na vyanzo mbalimbali kupata uhakika kwa kutumia madaraka aliyonayo wakiwemo waajiri na wanaofanya malipo kujiridhisha.
Alisema anaamini hatua aliyoichukua Dk Magufuli ni ishara na njia yake ya kutambulisha kwa umma mtindo wa uongozi unaozingatia uwazi na uwajibikaji. “Hiki kwetu ni kitu kipya hatujakizoea, lakini sasa ni vyema kila kiongozi awe makini na kutambua kuwa akikosea lazima awajibike,” alisisitiza.
Mfumo uangaliwe
Pamoja na hayo, alimuomba Rais Magufuli awe mvumilivu na atambue kuwa huenda tatizo kubwa bado lipo kwenye mfumo uliopo wa kupeana taarifa ambao utahitaji kuangaliwa kwa umakini na kuchukuliwa hatua stahiki.
Alisema Dk Magufuli ni kiongozi anayefuata mfumo wa kisheria na kwamba hatua zote alizochukua zinatokana na nia njema aliyonayo kwa watanzania. “Huyu ni mtakatifu baada ya Mungu, ana moyo mzuri na nia njema kwa watanzania,” alisema Profesa Semboja.
Akizungumzia watumishi hewa, Profesa Semboja alishauri baada ya operesheni ya kuwatafuta upande wa rasilimali watu ndani ya utumishi wa umma lazima utoe taarifa nzima na kufafanua kilichotokea.
Kwa upande wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, alisema hatua aliyoichukua Dk Magufuli ya kumvua uongozi Kilango ni ishara kuwa anatoa kipaumbele katika suala zima la uwajibikaji lakini pia hapendi viongozi wasiojishughulisha.
“Inaonesha dhahiri Dk Magufuli katika masuala nyeti yanayogusa taifa hapendi majibu mepesi wala njia za mkato. Hii inamaanisha kuwa viongozi hawana budi kuzifanyia kazi taarifa wanazopewa na kujiridhisha kwanza,” alisema Dk Bana.
Awali gazeti hili lilizungumza na Kilango kwa njia ya simu ili kuweza kupata upande wake kuhusu nini kilitokea na kusababisha kutoa taarifa hiyo isiyo sahihi kuhusu watumishi hewa mkoani Shinyanga, ambapo mara baada ya salamu, mwandishi alipojitambulisha alikata simu.
Juzi Rais Magufuli alitengua uteuzi wa mkuu huyo wa mkoa baada kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari kuwa mkoani kwake hakuna watumishi hewa. Alisema baada ya taarifa hiyo, aliunda timu maalumu kwa ajili ya uhakiki wa watumishi hewa mkoani humo na ndani ya siku moja, walibaini kuwepo kwa watumishi hewa 45 waliokuwa tayari wamelipwa mishahara yenye gharama ya Sh milioni 339.9.

Hakuna maoni: