Akizungumza
jana bungeni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly alisema
taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo, ilifikishwa bungeni juzi na jana
asubuhi wamepewa na wakaanza kuujadili papo hapo.
“Wametuletea
taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo leo asubuhi (jana), ila taarifa
hiyo ilifika bungeni jana (juzi), na sisi kamati tumekaa asubuhi
kuijadili kama tulivyokubaliana wakati wa vikao vya kamati mjini Dar es
Salaam na tutatoa taarifa ya maamuzi ya kamati,” alisema Aeshi ambaye ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini.
Akizungumza
baada ya kuahirisha kikao cha kamati hiyo jana jioni, Aeshi alisema
hawajafikia maamuzi na kwamba leo wataendelea kujadili taarifa hiyo na
mchana watatoa maazimio ya kamati.
“Tumeahirisha
kikao hadi kesho (leo) na bado tunapitia taarifa hiyo na kama kamati
itaona haja ya kuwaita tena jeshi hilo kutoa maelezo, tutajua baada ya
kufikia maamuzi,” alisema Aeshi na kuongeza kuwa kwa sasa
wanachambua taarifa hiyo na iwapo wataona kuna haja pia ya kuutaka
mkataba huo watatoa maelekezo.
Awali,
Aprili 5, mwaka huu mjini Dar es Salaam, kamati hiyo ilitoa siku saba
kuanzia siku hiyo kwa Jeshi la Polisi nchini, kupeleka mkataba
walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi iliyopewa zabuni ya kufunga
mashine 108 katika vituo tajwa nchini, ila hadi sasa ni vituo 14 tu
ndivyo vilivyofungwa mashine hizo.
Hatua
hiyo ilikuja baada ya kamati hiyo kukutana na jeshi hilo kupitia
taarifa ya hesabu za jeshi hilo za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kubainika kuwa
na ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo.
Ukiukwaji
wa utekelezaji wa mkataba huo mwingine ni pamoja na kampuni hiyo
kulipwa asilimia 99 ya fedha zote za mkataba huo wenye thamani ya Sh
bilioni 37, huku kazi iliyofanywa ni chini ya robo.
“Ukiangalia
kazi iliyofanywa tangu mwaka 2011 hadi leo ni kidogo na pesa hawa
kampuni wameshachukua asilimia 99, sasa tumewaagiza watuletee huo
mkataba ndani ya wiki moja walioingia na kampuni hiyo ili tuupitie,” alisema Aeshi wakati wa vikao vya Dar es Salaam.
Hata
hivyo, baada ya maagizo hayo, taarifa hiyo ya utekelezaji
haikuwasilishwa kwenye kamati hiyo ndani ya muda uliokubaliwa na Aeshi
alisema siku zote wamekuwa wakitoa maagizo kwa mdomo na taasisi nyingi
zimekuwa zikitekeleza.
Aliongeza
ila hilo la mkataba wa Lugumi lilikuwa tabu kutekelezwa hadi kamati
hiyo, ilipochukua hatua za kukumbushia kwa kuandika maelezo.
Hata
hivyo, baada ya taarifa za mkataba huo,zilisambaa habari kwenye vyombo
vya habari kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ni Mbunge wa Chalinze,
Ridhiwani Kikwete (CCM), Said Lugumi na vigogo wengine.
Kutokana
na sakata hilo, mbunge huyo alikanusha kuhusika kwake na kusema ni
kweli kwamba ana urafiki wa kawaida na Said Lugumi na kusisitiza kwamba
hahusiki kwa njia yoyote na kampuni hiyo.
“Kwanza
kabisa mimi si mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, hilo ni jambo la
msingi kabisa watu waelewe na sijawahi kufanya biashara yoyote na
Lugumi. Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo tunafahamiana naye
na ni rafiki yangu,” alisema Ridhiwani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni