ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 23 Aprili 2016

fuatilia simulizi ya kusisimua

MIRATHI YA KAKA SEHEMU YA 1
Kiza kinene kilikuwa kimetanda pande zote za dunia, sikuelewa kama nipo peke yangu ama tupo wengi  kutokana na kutoona umbali hata wa sentimita moja mbele yangu.
Nilifikicha macho na kutazama huku na kule,
‘Mungu wangu! Nipo wapi huku, nimefikaje na nimefika saa ngapi?’ Nilishindwa kupata jibu.
Nilikodoa macho kwa nguvu kama mtu aliyeshikwa ugoni; bado nilikuwa sioni chochote mbele ya mboni za macho yangu zaidi ya weusi wa giza totoro lililokuwepo.
Niligeuka kushoto sikuona chochote, nikageuka kulia pia sikuona chochote. Niliamua kugeuka mzimamzima, bado sikupata picha hata kidogo, moyo wa woga ulianza kuniingia,  nikataka kukimbia lakini nikashindwa.
Nilipojaribu kunyanyua mguu wangu wa kuume nipige hatua kuelekea mbele, mguu ulikuwa mzito.
Ndipo nilipogundua kuwa nguvu zimeniishia, viungo vyote vya mwili nilivihisi vimelegea; vilikuwa vimekufa ngazi kabisa. Nilibaki nikitetemeka palepale, nikajaribu kufumbua kinywa changu angalau nipige yowe la kuomba msaada. Hata hivo nilijikuta nikishindwa kuongea, nikaishia kumung’unyamung’unya maneno utadhani anaongea bubu vile. Kinywa kilikuwa kizito kufumbuka.
Kijasho chembamba kilianza kunitoka, nikajikuta nimelowana chepechepe mwili mzima utadhani nimemwagiwa maji. Ghafla nikadondoka chini mzimamzima, nikaanguka  puu kama gunia la mtama liangukavyo linapotupiwa chini hasahasa na mtu mzembe ama aliyechoka kubeba.
Nilianza kuona mwanga mweupe, mwanga huo ulikuwa ni mkali mara kumi zaidi ya ule wa radi; mwanga huo ulizidi kujirudiarudia.
Ghafla mwanga ulisitisha kumulika; mara nikamuona mtu mbele yangu, mtu huyo alikuwa amevaa kanzu iliyong’aa japokuwa gizani. Nilijaribu kuinua kichwa changu nimwangalie huenda nitang’amua kuwa ni nani.
Nilijikuta nikipigwa na butwaa baada ya kuinua macho yangu kwani nilimuona mtu huyo ni wa ajabu mno. Ni miaka ishirini na saba sasa tangu nizaliwe lakini sijawahi kuona mtu mrefu namna hii hapa chini ya jua. Nilijaribu kukifuatilia kiwiliwili chake ili nione kichwa chake kilipoishia .
Niligundua kuwa mtu huyo alikuwa ni mrefu kuzidi maelezo kwani nilishindwa kuuona mwisho wake.
Sijakaa sawa mtu huyo akapotea, nilibaki nikiwaza bila kupata jawabu.                           ‘Nitasalimika kweli leo?’ Nilijiuliza kimoyomoyo bila kutoa sauti. Nikaangaza pande zote, giza lilikuwa bado lipo palepale. Nilijaribu kuinuka ili nikimbie, hata hivo  nilishindwa kwa vile mwili ulikuwa bado hauna nguvu. 

Sauti za ngurumo kama za radi zilianza kusikika kwenye ngoma za masikio yangu. Zilizidi kujirudiarudia kabla ya kusindikizwa na tetemeko kubwa la ardhi. Nilihisi ardhi yote inatikisika, woga ukazidi kuongezeka. Mapigo ya moyo wangu yakaanza kwenda kasi zaidi.
‘Nitapona kweli leo?’ Huu ni mfano wa baadhi ya maswali yaliyokuwa yanaisumbua akili yangu kwa wakati huo. Nilikosa majibu ya maswali yangu, nikaishia kujisemea kuwa Mungu yupo.
 

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 2


Tetemeko lilikoma ghafla, pakawa shwari tena, lakini giza lilikuwa lipo palepale. Mvua kubwa ilianza kunyesha, mwanga na miungurumo ya radi nilizidi kuvishuhudia.  
Nilibaki nimeduwaa baada ya kugundua kuwa pale nilipokuwa silowi licha ya mvua kubwa kuendelea kunyesha. Hakuna hata tone moja la maji lililokuwa likinifikia utadhani nilikuwa chini ya mwamvuli, nilizidi kuchanganyikiwa.
Hata kwa chini maji hayakunigusa hivyo nyayo zangu zilikuwa kavu. Lakini mvua nilikuwa naishuhudia ikinyesha, tena ni bonge la mvua.
Nilibaini kuwa kumbe nilikuwa nipo juu ya kilima baada ya mwanga wa radi kumulika. Lakini hapakuwa hata na mwamvuli juu yangu licha ya kutoangukiwa na tone hata moja.
Mara niliona kitu kama shuka jeupe kikishuka kutoka angani. Nilikisubiri kwa hamu kitu hicho ili nione ni nini kitatokea.
Woga ulianza kupungua. Siyo kwa kuwa nilikuwa nimeyazoea mazingira; la hasha! Ulipungua kutokana na kukata tamaa nikijua kuwa kuokoka kwangu ni asilimia 0.0025. Nilijipa uhakika wa kupoteza uhai endapo kudura za Mwenyezi Mungu zisingechukua nafasi.
Kitu hicho kilizidi kuteremka taratibu, tena kilikuwa wima mithili ya kitambaa cha sinema. Japokuwa giza lilikuwa limetanda angani kote, kitu hicho kiling’ara na niliweza kuushuhudia mng’ao wake. Shauku ya kutaka kuona kitakachotokea ilizidi kunishika, moyo wa woga haukuwepo tena kwa wakati huo.
Kitu hicho kilianguka chini, moshi mwingi niliushuhudia kilipokuwa kimeangukia. Moshi uliendelea kutoka mahali hapo lakini kitu hicho mfano wa shuka kilikuwa hakionekani tena.
Kufumba na kufumbua niliwaona watu katikati ya moshi huo, nikashindwa kujua idadi yao kamili kwa sababu walikuwa wanatembeatembea bila ya kutulia. Licha ya moshi mwingi kutanda eneo hilo, watu hawa walionekana ‘live’ tena bila chenga.
Nilizidi kuchanganyikiwa nilipoanza kuwatambua baadhi yao, kilichokuwa kinanishangaza ni kwamba kila niliyemtambua alikuwa kashatangulia mbele ya haki tukamzika, yaani namaanisha alishakufa kitambo.
Itaendelea......

Hakuna maoni: