Jumanne, 2 Agosti 2016
Jumatatu, 1 Agosti 2016
Jumapili, 31 Julai 2016
Jumamosi, 30 Julai 2016
Ijumaa, 29 Julai 2016
Lowassa Akoleza Moto CCM
Aliyekuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa ana
uhakika kuwa bado kuna wanachama wanaomuunga mkono ndani ya CCM na sasa
anawataka waendelee kushikamana naye, kauli ambayo inaweza kuchochea
moto ndani ya CCM.
Katika
taarifa yake fupi kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Lowassa
amewahakikishia wananchi kuwa kwa sasa ana “ari, nguvu na hamasa kuliko
wakati mwingine wowote”.
Lowassa,
ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne,
alijiondoa kwenye chama tawala Julai 28 mwaka jana baada ya jina lake
kuondolewa kwenye orodha ya wagombea urais kwa tiketi ya CCM.
Kuondoka
kwake kulisababisha mawaziri wa zamani, wabunge, wenyeviti wa mikoa,
madiwani na wanachama wengine wa CCM, wakiongozwa na waziri mwingine
mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kukihama chama hicho, hali
iliyosababisha ushindani kuwa mkubwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, huku
CCM ikilalamikia kusalitiwa.
Wakati
CCM ikifikiria hatua za kuchukua dhidi ya wasaliti wa chama
wanaotuhumiwa kuunga mkono harakati za upinzani wakati wa Uchaguzi Mkuu
uliopita, Lowassa ameongeza petroli kwenye moto ulioanza kuwaka.
“Kwa wale wenzangu waliobaki CCM na wanaoniunga mkono, tuendelee kushikamana na kunipatia taarifa kwa hatima ya nchi yetu,” amesema Lowassa ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
“Nawashukuru Watanzania kwa kuendelea kuniunga mkono mimi na wenzangu ndani Chadema.”
Kauli
hiyo kuwa kuna watu ndani ya CCM ambao wanampatia taarifa mbunge huyo
wa zamani wa Monduli na ombi lake la kutaka waendelee kumpa taarifa,
inaweza kusababisha hali ngumu zaidi kwa chama hicho, ambacho kinaamini
kuwa makada wake walikihujumu wakati wa uchaguzi kwa kumfanyia kampeni
kisiri.
Katika uchaguzi huo, Rais John Magufuli alishinda kwa kupata asilimia ndogo ya kura kulinganisha na watangulizi wake.
Ingawa
alipata kura milioni 8.8 na Lowassa kufuatia kwa kupata kura milioni
6.07, ushindi huo ni wa asilimia 58.46 dhidi ya asilimia 39.67
kulinganisha na ushindi wa asilimia 61.17 aliopata Kikwete mwaka 2010
dhidi ya asilimia 26.34 alizopata Dk Willibrod Slaa wa Chadema.
Tangu
Januari mwaka huu, CCM imekuwa ikijadili wasaliti hao katika ngazi ya
wilaya na taarifa za mapendekezo ya hatua dhidi yao kutumwa Halmashauri
Kuu kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.
Katika
hotuba yake ya kuaga, Jakaya Kikwete alimkabidhi mwenyekiti mpya wa
CCM, Rais Magufuli ripoti ya hali ilivyokuwa kwenye uchaguzi, akisema
yeye ndiye atakayeamua adhabu dhidi ya wale wote walioonekana kufanya
makosa. CCM imeshasema kuwa wasaliti wote ni lazima washughulikiwe.
Katika taarifa yake ya jana, Lowassa ameeleza kuwa uamuzi alioufanya wa kuihama CCM na kujiunga na Chadema “haukuwa
rahisi, lakini kwa ushupavu, ujasiri na mwongozo wa Mungu nilifanya
hivyo” na kwamba huo ni “uamuzi wa kihistoria katika nchi yetu.
“Najivunia
kwa uamuzi ule, kwani umewafungua macho Watanzania wengi na kuimarisha
demokrasia. Nimeingia Chadema nimewakuta viongozi na wanachama walio na
moyo wa dhati wa kuliletea maendeleo Taifa lao kivitendo,” anasema Lowassa katika taarifa yake fupi.
“Watanzania
bado wanataka mabadiliko na imezidi kuthibitisha kuwa hawawezi kuyapata
ndani ya CCM. Watanzania wanataka sera na mtu mbadala wa kuongoza
mabadiliko hayo. Vyote hivyo watavipata ndani ya Chadema na Ukawa kwa
jumla.”
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)