Jumamosi, 10 Septemba 2016
Ijumaa, 9 Septemba 2016
Alhamisi, 8 Septemba 2016
Marais EAC Kukutana kwa Dharura Jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyeji wao Rais Magufuli
Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika Jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitisha Mkutano wa
17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) utakaofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Septemba,
2016.
Mkutano
huo ambao ulitanguliwa na vikao vya maandalizi vya Makatibu Wakuu na
Mawaziri vilivyofanyika Jijini Arusha utajadili agenda kuu nne ambazo
ni:- Mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa
Kibiashara (EPA).
Agenda
zingine ni Kupokea Taarifa ya Mwezeshaji wa mazungumzo ya Amani nchini
Burundi, Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania; Kupata
taarifa ya hatua za kukamilisha uanachama wa Sudan Kusini kwenye EAC; na
Kuapishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka
Rwanda.
Akizungumzia
mkutano huo kwa Waandishi wa Habari, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa
mkutano huu umeitishwa kwa dharura ili kuzungumzia agenda hizo muhimu
hususan ile ya nchi wanachama kukubaliana kwa pamoja kusaini au
kutosaini Mkataba wa EPA ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016.
Kuhusu
Mkataba wa EPA, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki ilianza mazungumzo na Jumuiya ya Ulaya ya kushirikiana
kibiashara kupitia EPA miaka 14 iliyopita na kuingia makubaliano ya
awali mwaka 2014.
Alieleza
kuwa kwa mujibu wa makubaliano hayo ya awali EU na EAC zilikubaliana
Mkataba huo usainiwe kwa pamoja na nchi zote za Jumuiya mwezi Julai 2016
kabla ya kuanza utekelezaji wake.
Hata
hivyo Tanzania ilitangaza kutosaini makubaliano hayo kwa sababu mkataba
huo unaweza kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya
Tanzania nchi ya Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo 2025.
Aidha,
Tanzania inahitaji kujadiliana zaidi na nchi wanachama ili kujiridhisha
kuwa mkataba huo hautoathiri Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika
Mashariki hususan hatua ya mwanzo ya mkataba ambayo ni Umoja wa Forodha.
Kuhusu
nchi nyingine wanachama Mhe. Mahiga alieleza kwamba, tayari Kenya na
Rwanda zimesaini mkataba huo huku Uganda ikisubiri majadiliano ya nchi
wanachama kabla ya kusaini na Burundi ikijitoa kusaini mkataba huo kwa
vile tayari nchi za Ulaya zimeiwekea vikwazo vya kiuchumi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 07 Septemba 2016.
Jumatano, 7 Septemba 2016
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)