Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inapenda kuwatahadharisha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017
na umma kwa ujumla kuwa imepokea taarifa kuwa kuna watu wasio waaminifu
ambao si watumishi wa Bodi ambao huwapigia simu baadhi ya waombaji kwa
lengo la kuwatapeli.
Taarifa hizo za kitapeli zimekuwa
zikisambazwa katika siku za hivi karibuni kupitia mitandao mbalimbali ya
kijamii zikiwataka baadhi ya waombaji wa mikopo au wadhamini wao kutuma
fedha (Tshs 39,000/-) kwa namba ya simu 0716463190
ili fomu zao za maombi ya mikopo zilizowasilishwa Bodi zirekebishwe kwa
kuwa zimeonekana zina makosa na hivyo hawatapata mikopo.
Namba inayotumika kusambaza taarifa hiyo au kupiga simu kutoa taarifa hizo ni 0764640325 na mtu anayepiga anajitambulisha kwa jina la Charles Amos.
Bodi ya Mikopo inapenda kuwataarifu wadau wake wote, wakiwemo wale walioomba mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kuwa taarifa hizo si za kweli. Mtu huyo ni tapeli na si mtumishi wa Bodi ya Mikopo.
Iwapo waombaji watapigiwa simu na matapeli hao, watoe taarifa kwa vyombo vya dola kwa hatua zaidi.
Aidha, Bodi ya Mikopo inapenda
kuwataarifu waombaji wa mikopo kuwa utaratibu wa Bodi kuwasiliana na
waombaji wa mikopo ambao fomu zao za maombi hubainika kuwa na upungufu
haujabadilika. Mara baada ya kazi ya ukaguzi wa fomu kukamilika, Bodi ya
Mikopo itatoa taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo
tovuti hii ya Bodi na kuwaalika waombaji kufanya marekebisho.
Mwisho.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO,
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU,
IJUMAA, AGOSTI 12, 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni