ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 5 Agosti 2016

Vyama 9 Vya Siasa Kufutwa

 








Vyama tisa vya siasa kati ya 22 vyenye usajili wa kudumu vipo hatarini kufutwa kutokana na kushindwa kukidhi vigezo na matakwa ya kisheria yaliyoviwezesha kupata usajili wa kudumu. 
Hatua ya kufutwa vyama hivyo, vikiwamo baadhi visivyo na ofisi za kudumu (vyama vya mfukoni) itafikiwa ikiwa vitashindwa kujieleza kutokana na makosa ambayo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imebaini katika ukaguzi uliofanyika hivi karibuni Bara na Visiwani. 
Jukumu kubwa la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni kusimamia, kuboresha, kuendeleza na kudumisha demokrasia ya vyama vingi hapa nchini majukumu ambayo yanatokana na Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi Na. 7 ya mwaka 2010. 
Majukumu mengine ya ofisi ya msajili ni kusajili vyama vya siasa na kuvifuta vyama ambavyo havikidhi matakwa ya sheria hiyo na kusimamia ugawaji wa ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria.
 Akizungumza ofisini kwake jana, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema uhakiki uliofanywa na ofisi yake katika vyama hivyo upande wa Bara na Visiwani umebaini kasoro nyingi zikiwamo za ukiukaji wa masharti ya usajili.
 “Katika uhakiki uliofanywa na ofisi yangu tumebaini kasoro mbalimbali ambazo kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ni miongoni mwa vigezo muhimu vinavyoangaliwa ili chama kiwe na sifa ya kusajiliwa,” alisema. 
“Kasoro tulizozibaini ni nyingi na baadhi ya vyama kutokana na mapungufu waliyo nayo huhitaji kutoa nafasi tena….unaweza kuvifuta hapohapo.” 
Msajili hakutaka kutaja majina ya vyama hivyo ambavyo tayari vimeandikiwa barua lakini alitaja makosa kuwa baadhi havina ofisi za kudumu Tanzania Bara na Visiwani au upande mmoja na vingine havina anuani ya posta. 
“Unakuta chama fulani kina ofisi labda Zanzibar lakini hakina ofisi Bara,” alisema Jaji Mutungi. Alisema vyama vingine havina viongozi wa kitafa kutoka pande mbili za Muungano na pia havina bodi ya wadhamini iliyosajiliwa kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) kama sheria inavyohitaji. 
Katika ukaguzi huo, Msajili alibaini pia kasoro nyingine kuwa ni kukosekana kwa orodha ya wanachama wa chama husika jambo alilosema nalo ni muhimu kila chama kuwa na orodha ya idadi ya wanachama wake. 
Vilevile, baadhi ya vyama hivyo vimeshindwa kuonyesha akaunti ya fedha ya chama hali inayotia shaka namna vinavyojiendesha.

Hakuna maoni: