WAKATI
takribani asilimia 20 ya viongozi wa umma kwa mwaka 2011 hadi mwaka
jana hawakuwasilisha matamko ya mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma kwa wakati, mwaka huu serikali imetangaza kuhakiki
matamko ya mali za viongozi 500.
Aidha,
serikali hiyo imebainisha wazi kuwa haitowafumbia macho viongozi,
watakaoshindwa kuwasilisha matamko ya mali zao kwa mujibu wa sheria,
ikiwemo viongozi watakaowasilisha matamko ya mali yatakayobainika kuwa
na udanganyifu.
Hayo
yalibainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki wakati akifungua warsha ya
wadau, kujadili taarifa ya matokeo ya utafiti kuhusu hali ya maadili
nchini Dar es Salaam jana.
Kairuki
alikiri kuwa hata katika tafiti nyingine ndogo, zilizofanyika kuhusu
hali ya maadili nchini pamoja na takwimu kubadilikabadilika, lakini
zilibainisha kuwepo kwa viongozi wasiowasilisha matamko yao ya mali na
wengine kutowasilisha kwa wakati.
Alisema
taarifa hiyo ya utafiti kuhusu hali ya maadili ya viongozi nchini kwa
miaka mitano kuanzia 2011 hadi mwaka jana, ilibainisha kuwa pamoja na
kuwepo kwa mwamko wa viongozi kuhusu suala zima la maadili, bado
asilimia 20 ya viongozi hao wa umma hawakuwasilisha matamko yao ya mali
kwa wakati.
“Tumepokea
taarifa hii na imetutia hamasa kwa kweli, tumeona asilimia 20
hawarejeshi kwa wakati matamko yao, hawa ni wengi sana ikizingatiwa kuwa
ni viongozi, tunatoa onyo hakuna atakayefumbiwa macho endapo atakiuka
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kwani atachukuliwa hatua stahiki
za kisheria,” alisisitiza.
Alisema
kwa kawaida endapo kiongozi asipowasilisha tamko la mali zake hadi
ifikapo Desemba 31, huhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma,
lakini pia inapothibitika kuwa alikiuka kwa makusudi sheria hiyo ya
maadili ya viongozi huchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema
mwaka huu, kuna jumla ya viongozi wa umma 15,624 kati ya hao viongozi
500 tayari wameshatengewa fedha kwa ajili ya mali zao kuhakikiwa na
endapo fedha zitapatikana idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia
1,000.
“Miaka
ya nyuma tulikuwa tunahakiki kwa mwaka viongozi 100 hadi 200, safari
hii tumejipanga kuanza na viongozi 500. Lakini katika hili tunaomba
wananchi nao watusaidie kuhakiki mali za viongozi hawa wa umma kwani
sheria inawa ruhusu kufanya hivyo, ili kuweza kubaini viongozi
wadanganyifu,” alisema.
Akiwasilisha
matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine
(SUA), Profesa Kessy aliyefanya utafiti huo kwa kushirikiana na
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, alisema lengo la utafiti huo ni
kuangalia hali halisi ya maadili nchini kuanzia viongozi hadi kwa
wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni