ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 31 Agosti 2016

Makusanyo Kodi za Simu Yapanda Maradufu

Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu, imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato lililoanza kushuhudiwa kutoka kampuni za simu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), iliambiwa kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka huu, mwezi uliopita serikali imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato, yaliyotolewa na kampuni za simu.

Taarifa hiyo ilitolewa jana kwenye Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, imeonesha Kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria, Julai pekee mwaka huu imelipa Sh bilioni 1.9.

Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin Barongo aliiambia kamati hiyo kuwa kwa upande wa Kampuni ya Tigo, walikuwa wanatoa wastani wa Sh milioni 250 kwa mwezi, lakini sasa wametoa Sh bilioni 1.48.

Barongo ambaye ni Meneja Msaidizi, Kitengo cha Walipa Kodi Wakubwa TRA alikuwa akizungumzia namna Mtambo Maalumu wa Kusimamia Mawasiliano na Udhibiti wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS) unaosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha ukusanyaji mapato.

“Pamoja na mabadiliko ya sheria yaliyoanza mwezi Julai mwaka huu, kampuni za simu zilikuwa zikitoza transfer, lakini sheria ilikuwa haigusi kwenye kutoa, Baada ya hiyo, tuligundua kuwa sasa kamisheni nyingi zilipelekwa kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye transfer zinapungua,” alisema Barongo.

Aliendelea kusema, “Kwa hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi ambayo tunatoza kwenye kuweka na kutoa, yametusaidia.” 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso alisisitiza kuwa wabunge wanategemea Wizara ya Miundombinu kupitia sekta ya mawasiliano, ichangie mapato mengi kwa serikali.

Baada ya Bunge kupitisha mabadiliko ya sheria ya fedha yaliyopitisha utozaji kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na simu za mkononi, ulijitokeza mjadala ambao baadhi ya watu walidai ushuru huo utaathiri wateja wa kampuni za simu na benki.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alifafanua kwamba serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha au vyote kwa kadri itakavyotozwa akisisitiza kwamba utalipwa na benki na kampuni na si mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala itakayofanyika

Hakuna maoni: