ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumapili, 18 Desemba 2016

Simba kibarua kigumu kwa Ndanda

 Imeandikwa na Mwandishi Wetu
SIMBA na Azam FC leo zinashuka dimbani kusaka pointi tatu kwenye viwanja tofauti katika michezo yao ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba itakuwa mgeni kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara dhidi ya Ndanda FC na Azam FC ikikaribishwa na African Lyon kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Wekundu hao wa Msimbazi huenda wakaendeleza rekodi yao ya kuifunga Ndanda FC baada ya mchezo wao wa mzunguko wa kwanza kuwachapa mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa wa kwanza katika ligi kwa kipa mpya wa Simba Mghana Daniel Agyei ambaye anatarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha kwanza baada ya kipa Vicent Angban wa Ivory Coast kusitishiwa mkataba wake.
Pia, wachezaji wengine wapya ni kiungo James Kotei, mshambuliaji Pastory Athanas, Juma Luizio, Moses Kitandu na beki Vicent Costa.
Simba yenye pointi 35 inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kurejea kileleni mwa msimamo baada ya jana Yanga kuishusha. Yanga inaongoza kwa pointi 36 sasa. Vile vile, Ndanda FC yenye pointi 19 iliahidi kufuta rekodi ya kufungwa na timu hiyo ikijivunia kusajili wachezaji wawili wapya Ayub Shaban na Ismail Mussa watakaokuongeza nguvu.
Kwa upande wa Azam FC yenye pointi 25 itacheza leo kwenye uwanja wa Uhuru ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya African Lyon katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Chamazi.
Pengine, mchezo wa leo Azam FC kwa vile imefanya mabadiliko makubwa ikafanya vizuri tofauti na African Lyon yenye pointi 17 ambayo imeondokewa na wachezaji wake wengi waliojiunga na Mbeya City.
Wachezaji wapya wanaotarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha Azam FC ni Samwel Afful, Mohamed Yahaya, Yakubu Mohamed, Enock Agyei, Stephani Kingue, Joseph Mahundi na Abdallah Kheri.
Azam FC inahitaji kushinda katika mchezo huo ili kuingia katika mbio za kuligombania taji la ligi. Pia, Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya dhidi ya Majimaji huku Mbao FC ikiwa kwenye uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza ikiwakaribisha Stand United.

Makamu wa Rais: “Kila Jumamosi ya pili ya mwezi ni siku ya Mazoezi nchi nzima”


makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa muda wa miezi Mitatu kwa halmashauri zote nchini kurudisha serikalini haraka maeneo ya michezo yalivamiwa na watu kwa ajili ya kufanya shughuli zao binafsi ambapo pia ametoa agizo kuwa kila Jumamosi ya pili ya mwezi iwe ni siku ya mazoezi kwa watanzania wote ilikujiimalisha afya zao.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo baada ya kushiriki matembezi na kuzindua wa kampeni ya Kitaifa ya kudhibiti Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye viwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais ameonya kuwa kama watendaji wa mikoa na halmashauri watakaoshindwa kurudisha maeneo hayo basi watenge haraka maeneo mengine kwa ajili ya wananchi kufanya mazoezi kama hatua ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Katika kuunga mkono utaratibu wa kufanya mazoezi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wa mikoa na wilaya zote kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi angalau kwa mwezi mara Moja.

“Nitamke kuwa kila Jumamosi ya pili ya mwezi itakuwa siku ya mazoezi kwa afya kwa sababu mazoezi ni afya na nawaasa wananchi kufanya mazoezi na kuanzisha na kujiunga na vikundi vya mazoezi na serikali itatimiza wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia mazoezi kote nchini”

Makamu wa Rais pia ameagiza watendaji wa Wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia kurudisha mchakamchaka mashuleni kulingana na maeneo yalivyo. Amesema mchakamchaka utasaidia kuimarisha afya za wanafunzi na kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

“Natoa rai utaratibu wa mchakamchaka katika shule zetu urudishwe mara Moja katika Muda ambao utaonekana ni mwafaka kwa shule husika”.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Afya kukamilisha haraka mchakato wa kuunda kamati ya kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza itakayojumuisha wadau kutoka wizara mbalimbali nchini.
Amesisitiza kuwa mchakato huo ni lazima ukamilike tarehe 1 machi mwaka 2017.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yanaongezeka sana duniani kote hasa kwenye nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania ambapo magonjwa hayo mpaka sasa yanachangia asilimia 27 ya vifo Duniani.

Amesema utafiti uliofanyika mwaka 2012 uliohusisha wilaya 53 hapa nchini umeonyesha viashiria hatarishi vya magonjwa hayo ambapo asilimia 26 ya wananchi ni wanene kupita kiasi,asilimia 26 wana lehemu nyingi mwilini na asilimia 25.9 wanashinikizo kubwa la damu.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 15.9 ya wananchi wanavuta sigara na asilimia 97.2 ya wananchi wanakula mboga mboga na matunda chini ya mara tano kwa siku.

Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema watanzania wanaweza kukabiliana na magonjwa hayo kwa kufanya mazoezi ya viungo angalau mara tatu kwa wiki kwa muda wa nusu saa, kuzingatia ulaji wa vyakula unaofaa,kupunguza matumizi ya pombe kupita kiasi na kujiepusha na matumizi ya tumbaku.

Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi katika nasaha zake amewahimiza Watanzania kufanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya zao.

Amesema kama watanzania watafanya mazoezi wataepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo,kisukari,uti wa mgongo na mifumo ya neva na figo.

Kauli mbiu ya uzinduzi wa kampeni ya Kitaifa ya Kudhibiti Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza ni “Afya yako,Mtaji wako”

Breaking news:Mvua yaanza kuwatesa wanailula

Msimu wa mvua ukiwa umeanza, Watu waanza kuathirika na mvua hizo kutokana na kufanya uharibifu mbalimbali ikiwamo kuezua Nyumba katika maeneo hayo
Tukio hill limetokea ilula isele ambapo takribani Nyumba sita zimeezuliwa mapaa kutokana na mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali