ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumapili, 18 Desemba 2016

Simba kibarua kigumu kwa Ndanda

 Imeandikwa na Mwandishi Wetu
SIMBA na Azam FC leo zinashuka dimbani kusaka pointi tatu kwenye viwanja tofauti katika michezo yao ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba itakuwa mgeni kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara dhidi ya Ndanda FC na Azam FC ikikaribishwa na African Lyon kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Wekundu hao wa Msimbazi huenda wakaendeleza rekodi yao ya kuifunga Ndanda FC baada ya mchezo wao wa mzunguko wa kwanza kuwachapa mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa wa kwanza katika ligi kwa kipa mpya wa Simba Mghana Daniel Agyei ambaye anatarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha kwanza baada ya kipa Vicent Angban wa Ivory Coast kusitishiwa mkataba wake.
Pia, wachezaji wengine wapya ni kiungo James Kotei, mshambuliaji Pastory Athanas, Juma Luizio, Moses Kitandu na beki Vicent Costa.
Simba yenye pointi 35 inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kurejea kileleni mwa msimamo baada ya jana Yanga kuishusha. Yanga inaongoza kwa pointi 36 sasa. Vile vile, Ndanda FC yenye pointi 19 iliahidi kufuta rekodi ya kufungwa na timu hiyo ikijivunia kusajili wachezaji wawili wapya Ayub Shaban na Ismail Mussa watakaokuongeza nguvu.
Kwa upande wa Azam FC yenye pointi 25 itacheza leo kwenye uwanja wa Uhuru ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya African Lyon katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Chamazi.
Pengine, mchezo wa leo Azam FC kwa vile imefanya mabadiliko makubwa ikafanya vizuri tofauti na African Lyon yenye pointi 17 ambayo imeondokewa na wachezaji wake wengi waliojiunga na Mbeya City.
Wachezaji wapya wanaotarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha Azam FC ni Samwel Afful, Mohamed Yahaya, Yakubu Mohamed, Enock Agyei, Stephani Kingue, Joseph Mahundi na Abdallah Kheri.
Azam FC inahitaji kushinda katika mchezo huo ili kuingia katika mbio za kuligombania taji la ligi. Pia, Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya dhidi ya Majimaji huku Mbao FC ikiwa kwenye uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza ikiwakaribisha Stand United.

Hakuna maoni: