ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumapili, 1 Aprili 2018

WARAKA WATIKISA

Askofu Mkuu wa Makanisa ya Babtisti Tanzania, Mchungaji Arnold Manase amewataka viongozi wa dini kushauri kwa namna njema bila kutabiria nchi mambo mabaya kwani ubaya huenea haraka kuliko wema.

Aidha, amesema kila dhehebu nchini likisimama na kutoa waraka wake taifa halitakalika.

Askofu Manase ameyasema hayo leo Jumapili Aprili Mosi, jijini Arusha wakati akitoa salam kwenye Ibada ya Pasaka katika Kanisa la Jerusalem Babtisti lilipo Ngarenaro mjini Arusha.

Kupitia Ibada hiyo, Askofu Manase amewaomba wadau wa amani nchini, ikiwamo Serikali kukaa na wadau ili kujadili mustabali wa taifa.

“Tunahitaji kuomba amani ya Mungu itawale, kama ambavyo Yesu Kristo alivyotuachia amani yake.

“Tukiwa kama viongozi wa dini kama kuna mambo tunaweza kushauri basi tuyashauri kwa namna njema tusitabirie nchi mambo mabaya Kwani ubaya unaenea haraka kuliko wema, nawasihi tuhubiri amani,” amesema Askofu Manase.

Pamoja na mambo mengine, Askofu Manase katika Ibada hiyo ameongoza maombi kuomba hekima kwa viongozi wa Serikali, madhehebu yote nchono ili hekima ya Yesu Kristo ikatawale kwenye mioyo yao

Wanaopotosha Ukweli Waraka Wa Maaskofu KKKT Ni Wajinga

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amesema wale wote wanaojaribu kupotosha ukweli wa waraka wa maskofu kwa kuupaka matope ni wajinga.

Askofu Shoo ametoa kauli hiyo leo katika Usharika wa Moshi Mjini Dayosisi ya kaskazini, mkoani Kilimanjaro wakati akitoa salamu za Pasaka katika ibada maalumu ya kusherekea sikukuu hiyo.

Amesema kumekuwa na baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kupotosha waraka  wa maaskofu hao na kulipaka kanisa matope kwa malengo yao binafsi jambo ambalo halipendezi na kwamba watu hao ni wajinga.

“Wapo wanaotumia nguvu nyingi kutaka kupotosha ujumbe wa waraka wa maaskofu na wamekuwa wakilipaka kanisa matope ili waweze kurejea katika waraka ule, watu hawa naweza kuwaita ni wajinga lakini pamoja na hilo nataka wakayatafakari na kama wanaona kuna hatua za kuchukua wachukue.

“Kanisa limekuwa linapata kejeli za aina mbalimbali kutoka kwa watu hao na kuwatuhumu kuwa maskofu walifikia maamuzi ya kuandika waraka huo kutokana na sababu za kimaslahi kwa maana ya sadaka makanisani kupungua jambo ambalo si la kweli.

“Kanisa linasitikika sana, tunaposema jambo la kweli na jambo linalohusu maisha ya Watanzania wote, halafu kunatokea watu chache ambao naweza kuwaita wajinga wanakebehi na kusema eti kwa sababu sadaka zimepungua kanisani sisi sadaka hazijapungua kwani wakristo wanajitoa sana na hatujapungukiwa na kitu ila tunasema yale tunayoyaamini,” amesema.

Askofu Shoo amesema anafahamu kuwa kupitia waraka ule maaskofu wa kanisa hilo watabatizwa majina ya aina mbalimbali na kwamba hizo ni jitihada za kujaribu kuuzima ukweli ulipo katika wataka huo na wao hawajali kuhusu hilo bali watasimamia ukweli zaidi.

“Najua tutaitwa majina mengi maaskofu na hizo ni jitihada za upotoshaji wa ule ukweli ulipo katika waraka na tukumbuke hili si jambo la hivi hivi tu…. kwani kwa wakati mmoja mabaraza ya  maaskofu wa makinsa makubwa mawili nchini kukaa na kutoa waraka ambao una ujumbe ulioshabihiana si kitu cha kawaida mimi nasema kuna kitu Mungu anataka kutuambia kupitia ujumbe ule tutafakari hili kama taifa,” amesema.

Halima Mdee kufikishwa mahakamani Jumanne

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, anatarajia kufikishwa mahakamani Jumanne Aprili 3, kuungana viongozi wengine wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, wanaoshtakiwa kwa makosa manane yakiwamo uchochezi, kuhamasisha maandamano na uasi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hayo leo na kuongeza kuwa mbunge huyo amekiuka masharti yaliyomtaka kuripoti kituo cha polisi pamoja na viongozi wengine saba wa chama hicho kabla ya kufikishwa mahakamani.

Halima alikamatwa leo Jumapili Aprili Mosi, saa tisa alfajiri katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), alipokuwa akirejea nchini akitokea Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu.

Aidha, alipoulizwa ni kwanini Halima amekamatwa wakati mawakili wake walikuwa wakitoa taarifa zake, Mambosasa amesema: “hayo ni maneno tu, anafahamu taratibu zikoje, anafahamau sheria zinasemaje kwa sababu wanatunga wenyewe huko bungeni hilo si suala la kujadili na mimi, asubiri atajibu hayo mahakamani.

Mambosasa amesema hayo muda mchache baada ya Chadema kulitaka Jeshi la Polisi kumpatia dhamana Mbunge ili aweze kuendelea na matibabu.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje ya chama hicho, John Mrema amesema licha ya kwamba Mbunge huyo kuwa mgonjwa ambaye hivi punde ametoka hospitali, lakini pia dhamana ni haki yake na lawama zote zitakuwa juu yao endapo afya ya mbunge huyo itatetereka.

“Hadi mchana wa leo Aprili Mosi, Jeshi la Polisi limeendelea kumshikilia Katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na hajapatiwa dhamana pamoja na daktari wake kuwathibitishia polisi kuwa Mheshimiwa Halima ni mgonjwa.

“Tunasikitishwa na kulaani kitendo hiki cha polisi kuendelea, kumshikilia mgonjwa ambaye alikuwa amelazwa hospitalini, , tumetuma mawakili daktari wake lakini hawajafanikiwa mwisho, Jeshi la Polisi litawajibika kwa Watanzania endapo afya ya Halima Mdee ikitetereka au ikidhoofu zaidi na lawama zote zitakuwa juu yao,” amesema Mrema

Bavicha kula Pasaka mahabusu na kina Mbowe

Viongozi wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) kesho watasherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa kuwatembelea viongozi wa chama hicho waliopo magerezani.

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi ataongoza msafara wa viongozi wa baraza hilo watakaokwenda Segerea kumtembelea Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na wenzake.

Amesema wamefikia uamuzi huo kwa lengo la kwenda kuwatia moyo na kuwa nao pamoja.

Amesema viongozi wengine watakwenda Mbeya kwa ajili ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Katibu wa Chadema, Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga.

"Tunataka kusherehekea nao Pasaka na kuwafahamisha kuwa chama kinaendelea, hatuwezi kurudishwa nyuma wala kutetereshwa,"amesema.

Ole Sosopi pia amewataka vijana wa baraza hilo kuwa tayari kupambana kwa ajili ya chama.

Amesema; "Kuna mambo mengi yanaendelea na tunafahamu wazi kuna ajenda ya kutaka kukifuta Chadema, sasa nawaambia hakuna namna chama hiki kitafutwa, tupo imara na tunazidi kuimarika,'

“Vijana kazi yetu ni kulinda chama na kazi hiyo tutaifanya kwa nguvu zote bila woga, hatutaogopa kufa," amesema.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya 01/04/2018



Jumatano, 28 Machi 2018

Machinga kupewa vitambulisho

Na Veronica Kazimoto,-Dar es Salaam,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  jana imezindua rasmi utoaji wa vitambulisho vya Wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi ikiwa ni pamoja na Wamachinga.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Kichere alisema kuwa, utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo unatokana na marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 yaliyofanywa na Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.

“Baada ya marekebisho ya Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, zoezi hili la kuwatambua wafanyabiashara wadogo lilianza kutekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji”, alisema Kichere.

Kichere alieleza kwamba, TRA  kwa kushirikiana na wadau hao, ilianza kutekeleza jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambapo leo hii baadhi yao wamepatiwa vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho hivyo.

Aliongeza kuwa,  zoezi la kutambua vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo na kuwapatia Kitambulisho cha Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi linaendelea kufanyika nchi nzima na kubainisha kuwa, ili wafanyabiashara wadogo waweze kupata vitambulisho hivyo maalum,  wanatakiwa kujiunga katika vikundi vinavyotambuliwa kisheria na Serikali, kuwa na Kitambulisho cha Taifa, kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi ya kikundi alichojiunga nacho pamoja na kuchangia shilingi 10,000.

“Zoezi la kuwatambua wafanyabiashara wadogo linaendelea kufanyika nchi nzima na vitambulisho maalum vinavyotolewa kwa  wafanyabiashara hao vitadumu na kutumika kwa kipindi cha miaka mitatu (3). Maelezo ya mfanyabishara mdogo yaliyopo kwenye kitambulisho hicho maalum ni pamoja na jina na picha ya mfanyabiashara, jina la eneo analofanyia biashara, Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na Sahihi ya mfanyabiashara husika”, Alifafanua Kichere.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam Mhe. Sophia Mjema aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kuwatambua wafanyabiashara wadogo ili waweze kupiga hatua kiuchumi kutoka daraja la chini hadi la kati na hatimaye kuweza kuchangia maendeleo ya nchi kupitia ulipaji wa kodi mbalimbali.

“Lakini kwanza naomba nimshukuru Mhe. Rais wetu John Pombe Magufuli kwa hii ndoto yake ya kuwasaidia wanyonge waliokuwa wanafanya biashara ndogo ndogo kutambulika na Serikali na kisha waondoke katika hali ya daraja la chini na kufikia daraja la kati.  Nafurahi kuwaeleza kwamba, ndoto ya Mhe. Rais wetu imetimia”, alisema Mjema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam Steven Lusinde alisema kuwa, wamefurahishwa na azma ya Serikali ya kuwatambua wafanyabiashara walio kwenye sekta isiyo rasmi kwa kuwa wamekuwa na hamu ya kuchangia maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu.

“Sisi wamachinga tumekuwa na hamu kubwa sana ya kuchangia Taifa letu kwa sababu tunaamini chochote tunachokiona katika nchi hii bila sisi kuchangia hakiwezi kwenda”, alieleza Lusinde.

Moja ya majukumu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ni kukusanya mapato ya Serikali sambamba na kutoa elimu kwa walipakodi na watanzania kwa ujumla ili kuongeza uhiari wa ulipaji kodi na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yanahitajika katika kuleta maendeleo ya nchi pamoja na wananchi wake

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya March 28