Na Veronica Kazimoto,-Dar es Salaam,
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) jana imezindua rasmi utoaji wa vitambulisho
vya Wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi ikiwa ni
pamoja na Wamachinga.
Akizungumza
wakati wa hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Kichere alisema kuwa, utoaji wa
vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo unatokana na marekebisho ya
Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 yaliyofanywa na Bunge la
Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo moja ya marekebisho hayo ni
kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio
kwenye sekta isiyo rasmi.
“Baada
ya marekebisho ya Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, zoezi
hili la kuwatambua wafanyabiashara wadogo lilianza kutekelezwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama
vile Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini
(RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji”, alisema Kichere.
Kichere
alieleza kwamba, TRA kwa kushirikiana na wadau hao, ilianza kutekeleza
jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es
Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa na Namba ya
Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambapo leo hii baadhi yao wamepatiwa
vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi
wa utoaji wa vitambulisho hivyo.
Aliongeza
kuwa, zoezi la kutambua vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo
na kuwapatia Kitambulisho cha Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipa
kodi linaendelea kufanyika nchi nzima na kubainisha kuwa, ili
wafanyabiashara wadogo waweze kupata vitambulisho hivyo maalum,
wanatakiwa kujiunga katika vikundi vinavyotambuliwa kisheria na
Serikali, kuwa na Kitambulisho cha Taifa, kuwa na Namba ya Utambulisho
wa Mlipakodi ya kikundi alichojiunga nacho pamoja na kuchangia shilingi
10,000.
“Zoezi
la kuwatambua wafanyabiashara wadogo linaendelea kufanyika nchi nzima
na vitambulisho maalum vinavyotolewa kwa wafanyabiashara hao vitadumu
na kutumika kwa kipindi cha miaka mitatu (3). Maelezo ya mfanyabishara
mdogo yaliyopo kwenye kitambulisho hicho maalum ni pamoja na jina na
picha ya mfanyabiashara, jina la eneo analofanyia biashara, Namba ya
Utambulisho wa Mlipakodi na Sahihi ya mfanyabiashara husika”, Alifafanua
Kichere.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam Mhe. Sophia Mjema
aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John
Pombe Magufuli kwa kuwatambua wafanyabiashara wadogo ili waweze kupiga
hatua kiuchumi kutoka daraja la chini hadi la kati na hatimaye kuweza
kuchangia maendeleo ya nchi kupitia ulipaji wa kodi mbalimbali.
“Lakini
kwanza naomba nimshukuru Mhe. Rais wetu John Pombe Magufuli kwa hii
ndoto yake ya kuwasaidia wanyonge waliokuwa wanafanya biashara ndogo
ndogo kutambulika na Serikali na kisha waondoke katika hali ya daraja la
chini na kufikia daraja la kati. Nafurahi kuwaeleza kwamba, ndoto ya
Mhe. Rais wetu imetimia”, alisema Mjema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga wa Kariakoo jijini
Dar es Salaam Steven Lusinde alisema kuwa, wamefurahishwa na azma ya
Serikali ya kuwatambua wafanyabiashara walio kwenye sekta isiyo rasmi
kwa kuwa wamekuwa na hamu ya kuchangia maendeleo ya Taifa kwa muda
mrefu.
“Sisi
wamachinga tumekuwa na hamu kubwa sana ya kuchangia Taifa letu kwa
sababu tunaamini chochote tunachokiona katika nchi hii bila sisi
kuchangia hakiwezi kwenda”, alieleza Lusinde.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni