WAZIRI
wa Mambo ya ndani, Dk Mwigulu Nchemba amewataka walimu kuendelea kutoa
elimu bora kwa wanafunzi kwa kuwafundisha maadili mema na inapobidi
matumizi ya fimbo yatumike.
Akizungumza
katika harambee ya ujenzi wa mabweni ya Shule ya Sekondari Lulumba
Wilaya ya Iramba mkoani Singida, jana, Dk Nchemba alisema walimu
wanatumia fimbo kunyoosha nidhamu za wanafunzi ili kutengeneza hatma ya
nchi.
“Kuna
wakati walimu wananyoosha nidhamu za wanafunzi lakini ninyi hamuoni hii
na kulalamika tu, kinachofanyika ni kwa manufaa yetu…niwaombe kwenye
kutumia mifano tumieni mifano na kwenye kutumia fimbo fanyeni hivyo ili
kutengeneza taswira ya nchi yetu,” alisema Dk Mwigulu.
Alisisitiza kuwa ni lazima kuendelea kulinda hadhi za walimu kwa kuwapatia miundombinu bora ya ofisi na vyumba vya madarasa.
Alisema
majengo ya taasisi yanapaswa kuwa bora zaidi na sio kutumia ramani za
awali pekee kwani zinapaswa kuboreshwa kulingana na maendeleo yaliyopo.
“Naunga
mkono ujenzi huu wa mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa vyumba vya
madarasa na ofisi za walimu hivyo nachangia mifuko 200 ya saruji
nawaahidi pia kutoa Sh milioni sita,” alieleza.
Mkuu
wa Wilaya Iramba, Emmanuel Luhaula alisema shule higo imekuwa ikifanya
vizuri kitaaluma kutokana na umahiri wa walimu kwani watoto hao wanajua
kujieleza kama vile wanasoma chuo kikuu.
Alisema wananchi wa Iramba wanatakiwa kujivunia kuwa na shule zao pamoja na walimu hao ili kuboresha elimu wilayani humo.
“Unafanya
jitihada ili kuhakikisha kila sekondari kunajengwa mabweni ili kuondoa
kero za wanafunzi.Sisi wa Iramba tushindwe wenyewe kukutumia. Nimekuwa
Mbunge lakini anayoyafanya mbunge huyu Mimi sikuyafanya,” alisema
Luhaula.
Naye,
Mkuu wa shule hiyo, Jeremiah Kitiku alisema licha ya kufanya vizuri
kitaaluma, wanakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa baadhi ya majengo,
upungufu vitabu vya masomo ya kiada 274.
“Mahitaji
ya vitabu vya kiada no 2,802 vilivyopo 2,328 upungufu ni 274. Pia
tunachangamoto ya kutokuwa na uzio kwa usalama wa wanafunzi, walimu na
mali za shule,” alisema Kitiku
Hata
hivyo, alisema malengo ya shule hiyo ni ukarabati wa vyumba tisa vya
madarasa na ofisi za nane za walimu ambazo zitagharimu Sh Milioni
169.4.
Katika
harambee hiyo, saruji iliyokusanywa ni mifuko 209, ahadi ya fedha ni
8,486,000, ahadi ya mifuko ya saruji 572, Gypsum 50 na nondo tani moja
jumla ya ahadi na fedha taslimu ni 19,494,300
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni