Baraza la Mitihani Tanzania limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2015 ambapo ufaulu umeshuka kwa 1.85% toka 69.75% mwaka 2014 hadi 67.91% mwaka 2015.
SERIKALI ya India imeiomba radhi serikali ya Tanzania, kufuatia
kudhalilishwa na kupigwa kwa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini
humo.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika, Kikanda na Uhusiano wa
Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, aliliambia Bunge, jana, mjini hapa,
wakati akitoa taarifa ya serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa serikali
ya India kufuatia tukio hilo.
Alisema tayari serikali ya India, imewachukulia hatua wote waliohusika na tukio hilo na wamefikishwa mahakamani.
Balozi Mahiga alisema serikali ya India, imeagiza kuwa wanafunzi wa
Watanzania wapewe ulinzi maalumu kwenye maeneo wanakoishi na
wasindikizwe wanapokwenda masomoni.
Aidha alisema serikali ya India ilimtaka balozi wa Tanzania afuatane
na maofisa waandamizi, wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India kwenda
Bangalore ili kukutana na wanafunzi wa Tanzania na wengine wa Afrika
kufanya mikutano na wanafunzi hao.
Balozi Mahiga alisema tukio hilo lilitokea baada ya uendeshaji mbaya
wa gari uliofanywa na mwanafunzi kutoka Sudan ambaye aligonga pikipiki
tatu na baada ya hapo kumgonga mama wa kihindi aliyekufa papo hapo.
Alisema baada ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alikimbia na wananchi
waliokuwa jirani walichoma gari lake moto na kwamba baada ya muda
lilitokea gari lingine likiwa na wanafunzi wanne Watanzania akiwemo
msichana mmoja.
Balozi Mahiga alisema wananchi hao walilisimamisha gari hilo na
kuwatoa nje wanafunzi hao ambapo mwanafunzi wa kike alivuliwa nguo na
kutembezwa mitaani uchi, huku wanaume wakipigwa sehemu mbalimbali za
miili yao na gari lao lilichomwa moto.
“Katika gari hilo kulikuwa na simu zao na document (nyaraka) mbalimbali ambazo ziliteketea,” alisema.
Alisema baada ya muda, polisi walifika lakini walishindwa kutoa
ushirikiano ingawa waliwachukuwa na kuwapeleka hospitali. Balozi Mahiga
alisema, “Kule hospitali walionekana wana majeraha makubwa, walitibiwa
lakini ikabidi waondoke kwa sababu walikuwa hawana fedha za kutosha za
kugharamia matibabu”.
Alisema baada ya hapo, Balozi wa Tanzania aliyeko India aliandika
dokezo la kidiplomasia kwa serikali ya India kulaani kitendo hicho na
kuitaka serikali ya India, ichukue hatua za kisheria na za haraka katika
kupeleleza tukio hilo.
KAMBI rasmi ya upinzani bungeni, imetangaza baraza lake la mawaziri
kivuli ambalo Chama cha ACT Wazalendo, chenye mbunge mmoja, Kabwe Zitto,
ndicho hakikuingizwa kwenye baraza hilo. Kiongozi wa kambi hiyo,
Freeman Mbowe alitangaza jana bungeni baraza hilo.
Chadema chenye wabunge wengi katika kambi hiyo, kina mawaziri vivuli
wengi ikilinganishwa na vyama vingine na wakati huo huo, kina wizara
nyingi ambazo kinaongoza peke yake kwa maana ya kuwa na mawaziri na
naibu mawaziri vivuli.
Mawaziri, naibu mawaziri vivuli wa Chadema ni katika Wizara ya Ofisi
ya Rais, Tamisemi, ambayo Waziri Kivuli ni Mbunge wa Moshi Mjini,
Japhary Michael (Chadema) na Naibu wake ni Mbunge wa Ukerewe, Joseph
Mkundi (Chadema).
Wizara ya Fedha na Mipango inaongozwa na wabunge wa Chadema ambao ni
Halima Mdee wa Kawe na Mbunge wa Momba, David Silinde. Kwa upande wa
Wizara ya Nishati na Madini pia inaongozwa na wabunge wote wa Chadema.
Waziri kivuli ni Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Naibu wake ni Mbunge
wa Tarime Vijijini, John Heche.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
inaongozwa na Mbungewa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) na naibu wake ni
Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru (Chadema).
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaongozwa na wabunge
wa Chadema; ambao ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye ni
waziri kivuli akisaidiana na wa Viti Maalumu, Devotha Minja.
Kwa upande wa wizara ya Utumishi, Utawala Bora inaongozwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema) pekee bila naibu.
Mawaziri Chadema kuhusu wizara ambazo mawaziri vivuli ni wa Chadema
na manaibu ni wa vyama vingine, ni Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu inaongozwa na Mbunge wa Bunda Mjini,
Ester Bulaya (Chadema). Bulaya anasaidiana na manaibu ambao wote ni wa
CUF.
Nao ni Mbunge wa Chake Chake, Yusuf Kaiza Makame na Abdallah Maftah wa Mtwara Mjini .
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa inaongozwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Naibu
wake Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Mngwali (CUF).
Mambo ya Ndani ya Nchi amepangiwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema
(Chadema) akisaidiwa na Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF),
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaongozwa na Mbunge wa
Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa
Viti Maalumu, Salma Mwassa (CUF).
Waziri kivuli mwingine ni Suzane Lyimo wa Viti Maalumu anayeongoza
Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi akisaidiana na Mbunge wa
Mgogoni, Dk Ali Suleiman Yusuf (CUF) ambaye ni naibu.
Wizara ya Katiba na Sheria inaongozwa na Mbunge Singida Mashariki,
Tundu Lissu (Chadema ) akisaidiana na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolela
(CUF).
Mawaziri wa CUF, Wizara zinazoongozwa na CUF kwa maana ya waziri
kivuli kutoka chama hicho, ni Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira, ambayo Mbunge wa Malindi, Ali Saleh Ali(CUF) anasaidiana na
Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema).
CUF imepata pia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo Waziri
kivuli ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) na naibu ni Mbunge wa
Viti Maalumu, Dk Immaculate Semesi (Chadema).
Kwa upande wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa, inaongozwa
na Mbunge wa Ole, Juma Hamad Omary (CUF) na naibu wake ni Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara (Chadema). Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF)
anaongoza wizara ya Maji na Umwagiliaji akisaidiwa na Mbunge wa
Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema).
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR) amepangiwa wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano akisaidiwa na Naibu ambaye ni Mbunge wa Karatu,
Qambalo Qulwi (Chadema). Kiongozi wa Upinzani bungeni, Mbowe aliomba
wote wanaohusika watoe ushirikiano kwa baraza hilo kadri inavyowezekana.