ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumamosi, 8 Agosti 2015

Dk Magufuli, Lowassa pambano la karne


Dk John Magufuli (Kushoto) na Edward Lowassa (kulia)
Kwa ufupi

Dk Magufuli na Lowassa ni kati ya makada saba waliosimamishwa na vyama saba kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambao inaelekea kuwa ndiyo watakaochuana vikali, hasa kutokana na ukweli kuwa Dk Magufuli anatoka chama tawala na Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, anaungwa mkono na vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimesalia siku 14 kabla ya kuanza kwa kampeni za urais, ubunge na udiwani, macho na masikio ya wengi yanaelekezwa kwa wagombea wawili kutoka vyama vikuu vya siasa, Dk John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema, ambao uchambuzi wa gazeti hili unaonyesha wana mengi yanayoshabihiana.

Wawili hao ni kati ya makada saba waliosimamishwa na vyama saba kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambao inaelekea kuwa ndiyo watakaochuana vikali, hasa kutokana na ukweli kuwa Dk Magufuli anatoka chama tawala na Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, anaungwa mkono na vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Wengine wanaowania urais ni Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, Chifu Lutayosa Chemba (ADC), Macmillan Limo (TLP), Hashimu Rungwe (Chauma), Fahami Dovutwa (UPDP) na mgombea wa ACT Wazalendo ambaye bado hajateuliwa.

Pamoja na kwamba katika siasa lolote linaweza kutokea, wagombea hao watano hawatazamiwi kuweka ushindani mkubwa zaidi ya ule wa Dk Magufuli na Lowassa.

Dk Magufuli hakutarajiwa kupita kwenye mbio za urais ndani ya CCM, ambako Lowassa na vigogo wengine walikuwa wakipewa nafasi kubwa, lakini ushindi wake umemfanya awe mgombea wa chama chenye mtandao mkubwa nchini na hivyo mwanzoni kupewa nafasi kubwa ya kushinda.

Hata hivyo, uamuzi wa Lowassa kujivua uanachama wa chama kilichomlea na kilichompa umaarufu mkubwa, umebadili upepo na sasa vita ya kuingia Ikulu Oktoba 25 inaonekana kuwa ya watu hao wawili.

Gazeti la Mwananchi linaangalia sifa ambazo wawili hao wanashabihiana pamoja na tofauti zao, kwa kuzingatia maelezo ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa.

Wote wamesomea ualimu

Moja ya mambo ambayo wawili hao wanashabihiana ni kusomea ualimu, ingawa wa fani tofauti. Dk Magufuli, ambaye atakuwa akitimiza miaka 56 siku nne baada ya Uchaguzi Mkuu, ni mwalimu aliyejikita kwenye masomo ya kemia na hesabu.

Alipata diploma ya ualimu mwaka 1982 kwenye Chuo cha Elimu Mkwawa, kabla ya kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata shahada yake ya kwanza, ya umahiri na ya uzamiri akijikita kwenye somo la kemia.

Lowassa, ambaye Agosti 26 atakuwa akitimiza miaka 62, alisomea shahada ya ualimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1977, lakini shahada yake ya uzamili ilijikita kwenye masomo ya maendeleo ya jamii.

Dk Magufuli alitumia taaluma yake kufundisha kemia na hesabu kwenye Shule ya Sekondari ya Sengerema, lakini Lowassa hakufundisha.

Wote ni makini

Pengine ni kutokana na maadili ya ualimu, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni watu makini katika utendaji wao, jambo ambalo limekuwa likiwafanya watu wanaofanya kazi chini yao kuwa na wasiwasi kila wanapowapeleka taarifa.

Dk Magufuli na Lowassa hutumia muda mwingi kujiridhisha na taarifa wanazopelekewa kabla ya kufanya uamuzi ambao wakati mwingine huonekana kama wamekurupuka.

Mhandisi mmoja ambaye amewahi kufungiwa leseni na Magufuli aliiambia Mwananchi kuwa kosa moja kubwa alilofanya ni kumwandikia Dk Magufuli taarifa ndefu, lakini iliyojaa mambo yasiyo sahihi.

Anasema kuwa aya hiyo ilikuwa ukurasa wa 20, lakini ndani ya muda mfupi Magufuli aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi.

Hali ni kama hiyo kwa Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu aliwahi kumtimua mkandarasi wa Wilaya Temeke kwa kushindwa kukagua ujenzi wa maghorofa ikiwemo la Chang’ombe Village lililoporomoka na kusababisha maafa ya mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa mwaka 2006.

Uchapakazi

Mbali na umakini, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni wachapakazi hodari katika wizara na taasisi walizopitia kiasi cha kujijengea jina kubwa kwa wananchi.

Utendaji wa Dk Magufuli hauna shaka na ameshaeleza bayana kuwa hapendi wazembe na wasiowajibika sanjari, kama Lowassa ambaye hata siku ya kwanza alipoingia ofisini mwaka 2005 aliwataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Wakati Dk Magufuli alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wengi walidhani kuwa amemaliza kisiasa, lakini mbunge huyo wa Chato alifanya kazi kubwa ya kutambua fursa za kiuchumi zilizoko hasa kwenye uvuvi na akafanikiwa kuonyesha ni kiasi gani Serikali ilikuwa ikipoteza fedha.

Wakati huo, Tanzania iliingia makubaliano na Afrika Kusini na nchi nyingine za ukanda huu kufanya doria kwa pamoja kwenye pwani ya Afrika Mashariki na juhudi hizo zilifanikiwa kunasa meli ya Tawaliq 1 iliyokuwa na samaki wenye thamani ya Sh20 bilioni.

Uchapakazi wake umedhihirika hasa kwenye ujenzi wa barabara, akiwa amefanikiwa kuunganisha takriban mikoa yote ya Tanzania katikja kipindi alichokaa Wizara ya Ujenzi.

Lowassa anaonekana zaidi katika kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika shughuli za maendeleo baada ya mpambano mkali dhidi ya Misri, ambayo ilikuwa na ukiritimba wa maji hayo kabla ya nchi tano kuungana na kusaini makubaliano ya matumizi ya maji hayo.

Lowassa pia anajinadi na mafanikio ya ujenzi wa shule za kata, ambazo kwa kiasi kikubwa zimefanikisha watoto wengi kupata elimu kwa gharama nafuu, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambao aliufanya kwa kukutanisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kuiamuru ichangia gharama za ujenzi.

Jambo lingine walilonalo Dk Magufuli na Lowassa ni misimamo. Dk Magufuli ni kiongozi mwenye misimamo isiyotia shaka na siku zote husimamia anachokiamini, sanjari na Lowassa, ni mwenye misimo yake na itakumbukwa alipokuwa Waziri wa Maji na baadaye Waziri Mkuu alionyesha misimamo.

Dk Magufuli alitofautiana hata na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati aliposimamia uendeshaji wa kivuko cha Kigamboni, na suala la kiwango cha mizigo inayobebwa na malori.

Moja ya kauli zilizonukuliwa sana ni ile ya “asiyekuwa na nauli ya kulipia kivuko, apige mbizi”, ambayo ilitafsiriwa kuwa ya kutojali wananchi, lakini faida zake ndio zinamfanya aonekane kuwa msimamo wake ulilenga kunufaisha wananchi.

Hali kadhalika Lowassa anajulikana kwa kusimamia uamuzi kama wa kubomoa maghorofa yaliyojengwa kinyume na sheria Masaki jijini Dar es Salaam. Msimamo wake pia kwenye suala la mkataba wa City Water iliyokuwa ikihusika na ugavi wa maji jijini Dar es Salaam ndio uliosababisha uvunjwe.

Ufuatiliaji

Lowassa na Dk Magufuli pia wanajulikana kwa kuwa wafuatiliaji wazuri kwa watu walio chini yao au wanaofanya kazi chini ya mamlaka zao. Dk Magufuli, ambaye anajulikana kwa kukariri tarehe, kiwango cha miradi, urefu wa barabara na kiwango cha fedha zilizotengwa kwenye miradi, hutumia talanta hiyo kufuatilia miradi mbalimbali na hasa muda wa kumalizika, hali inayomfanya kila mara atishia kuvunja mikataba na wakandarasi au kuivunja kabisa.

Hilo pia limekuwa likifanywa na Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu alikuwa akihakikisha wakuu wa wilaya na mikoa wako sehemu zao za kazi na yeyote ambaye alitaka kutoka alitakiwa awe na kibali, kwa mujibu wa baadhi ya watu waliofanya kazi naye.

Udhaifu

Mbali na sifa hizo nzuri, wanasiasa hao wanashabihiana katika udhaifu, hasa uamuzi wa papo kwa papo ambao pia husababishwa na kiu yao ya kutaka kuona kazi inafanyika.

Wote wawili hufanya uamuzi wa papo kwa pamo ambao wakati mwingine huwa na athari za kisheria. Uamuzi kama huo huwa na kadhia kwa wafanyakazi na makandarasi wanaopewa zabuni mbalimbali na Serikali.

Hawaachi mfumo wa utendaji

Udhaifu mwingine wa wawili hao ni hali ya kujituma wao bila ya kutengeneza mfumo ambao unaendeleza ufanisi na badala yake wanapoondoka, hali hubakia kama ilivyokuwa awali.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Dk Magufuli kwenye wizara alizopitia kama ya uvuvi na hali kadhalika kwa Lowassa.

Pia wanatofautiana

Tofauti kubwa kati ya Dk Magufuli na Lowassa ni mgombea huyo wa CCM kutokulia ndani ya chama na badala yake amekuwa kwenye nafasi za utendaji zaidi na uwaziri. Dk Magufuli amekuwa mwanachama wa CCM na mbunge, nafasi ambayo humuingiza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu pekee.

Lakini Lowassa ameshika nafasi mbalimbali kwenye chama kuanzia katibu wa mkoa hadi mjumbe wa vyombo vya juu vya CCM.

Kauli za wachambuzi

Baadhi ya wachambuzi na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Udsm) wamesema kwa nyakati tofauti kwamba wagombea hao wanaonekana kuwa na tofauti kubwa zinazoweza kufanikisha ushindi katika uchaguzi huo.

Mohammed Bakari, ambaye ni mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema wagombea hao wanafanana katika kigezo cha utendaji kazi lakini kiuamuzi na uzoefu wanatofautiana.

“Dk Magufuli ana uamuzi wa kukurupuka ila Lowassa ametulia,” alisema. “Kuhusu uzoefu pia Lowassa ni mzoefu kiuongozi kuliko Dk Magufuli.”

Alisema suala la uadilifu siyo rahisi kupata kiongozi mwadilifu kwa wagombea hao na bila kuzitaja kashfa hizo, alisema wote wana kashfa. Aliongeza kwamba, Lowassa ni mgombea anayeweza kuleta mabadiliko kwa Taifa hili, lakini Dk Maghufuli hawezi kutokana na mfumo uliopo kwenye chama chake.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Udsm, Dk Alexander Makulilo pia anaona sifa hizo zinazolingana.

Alisema wagombea hao wanafanana kwa utendaji mzuri wa kazi na uamuzi wa papo kwa hapo. Aidha, alisema Magufuli ni kiongozi anayeweza kuleta siasa mpya zisizokuwa na makundi.

Alisema Lowassa ni mgombea anayekabiliwa na changamoto ya Richmond iliyomfanya ajiuzulu uwaziri mkuu, wakati Dk Magufuli hana kashfa kubwa iliyowahi kujadiliwa bungeni.

“Lakini hali hiyo haiwezi kuwa changamoto kubwa kutokana na mwamko mkubwa wa kundi linalohitaji mabadiliko ya uongozi serikalini. Uchaguzi huu ninaufananisha na Zambia wakati chama cha UNIP kilipoondolewa madarakani kwa kuwa makundi ya kijamii yalikuwa yameamua kiondoke madarakani,” alisema.

Kuhusu mfumo kuibeba CCM, Dk Makulilo alisema ni sehemu ya changamoto kubwa inayoweza kufanikisha ndoto za Lowassa kuingia madarakani.

Jumatano, 29 Julai 2015


Hotuba ya Lowassa kujiunga Chadema



Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa akionyesha kadi yake ya uanachama wa Chadema baada ya kujiunga rasmi Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Kwa ufupi

Nilipokuwa natangaza nia ya kugombea urais kule Arusha, nilieleza nia yangu ya kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya nchi yetu na kuondokana na umaskini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma, azma hii bado iko palepale.

Ndugu waandishi wa habari na ndugu Watanzania wenzangu.

Yamepita majuma mawili tangu mchakato wa kuchagua mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ukamilike. Nimetumia muda huu kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika siasa nchini. Ninajua marafiki wengi na wananchi wenzangu wanaoniunga mkono wamekuwa wakisubiri kwa hamu nitoe kauli.

Nilipokuwa natangaza nia ya kugombea urais kule Arusha, nilieleza nia yangu ya kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya nchi yetu na kuondokana na umaskini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma, azma hii bado iko palepale.

Lakini nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetupa sisi pumzi ya kuendelea kuwa wazima wa afya njema hadi hivi sasa. Nawashukuru pia mke wangu Regina, wanangu, wanafamilia na marafiki wote kwa mapenzi, msaada na uvumilivu wao wakati wa kipindi hiki kigumu tunachopitia. Nawashukuru sana pia maelfu ya wanachama wa CCM walionidhamini na mamilioni zaidi walioniunga mkono.

Katika safari zangu za mikoani wakati wa kuomba udhamini, nilitiwa hamasa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuniunga mkono.Aidha, ninawashukuru sana wana kamati wangu, makundi mbalimbali na mamilioni ya vijana wakiwamo; “For You Movement”, “Friends of Lowassa” “Team Lowassa”, Umoja wa Bodaboda na wengine wengi ambao walijitolea kwa hali na mali katika Safari yetu ya Matumaini.

Nitakuwa sijahitimisha orodha ya shukrani iwapo nitaacha kuwashukuru viongozi wa dini zote nchini ambao waliungana na waumini wao wengi katika maombi na kwa kuniunga mkono. Najua sote tumevunjika moyo kwa yaliyotokea Dodoma na mazingira yaliyopelekea matokeo yale.

Kama ilivyokwishaelezwa, mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa Katiba na taratibu za uchaguzi za CCM.

Zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yangu. Kikatiba, Kamati ya Maadili si chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea Urais kupitia CCM.

Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka katiba ya CCM. Aidha, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM. Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa majungu na uongo mwingi, kuhakikisha kuwa jina langu halifikishwi mbele ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kujadiliwa licha ya ukweli usiopingika kuwa nilikuwa mgombea anayeungwa mkono na wananchi na wanachama wengi wa CCM kuliko wenzangu wote. Kibaya zaidi ni kile kitendo cha kuwanyima wagombea wote 38 haki ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu.

Ni dhahiri kwamba njama dhidi yangu ndani ya CCM si jambo jipya.Kumekuwa na mkakati wa siku nyingi wa kulichafua jina langu kwa uzushi na uongo usio na kifani. Aidha, mmeshuhudia jinsi vijana kadhaa walivyotumika kunikashifu na kunitukana na bila aibu na uongozi wa CCM na Serikali kuwazawadia madaraka makubwa.

Kwa namna ya kipekee napenda kuwapongeza na kuwashukuru wazee wetu akiwamo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ikiwa ni pamoja na waheshimiwa Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Alhaj Adam Kimbisa kwa uadilifu na ushujaa wao mkubwa wa kuisimamia katiba ya CCM na misingi ya haki na kukataa maamuzi batili ya Kamati ya Maadili na Kamati Kuu kuhusu uteuzi wa wagombea.

Cha msingi kuzingatia ni kuwa ili kuhitimisha njama za kunipora mimi na wagombea wengine haki zetu za msingi za kusikilizwa, viongozi wachache walikuwa tayari kupanda mbegu ya chuki na mfarakano ambao ni mfano mbaya kwa CCM na hata Taifa letu. Watanzania walitarajia chama kinachoongoza nchi kiwe ni mfano wa utawala wa sheria na kinara katika kutetea misingi ya haki na demokrasia na siyo kuihujumu. Yaliyotokea Dodoma yameitia dosari nchi yetu.

Kwa kifupi, ninaamini sikutendewa haki katika mchakato mzima wa kupendekeza majina na kuteua mgombea wa urais kupitia CCM. Nilinyimwa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kuchaguliwa.

Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na CCM au kuwa CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki, usawa na uadilifu.

Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema imetosha na SASA BASI!

Kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyosema, CCM siyo baba yangu wala mama yangu na kwamba kama Watanzania hawapati mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sasa tuyatafute mabadiliko nje ya CCM.

Hivyo basi, baada ya kutafakari kwa kina nimeamua kuwa kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya kweli ya nchi yetu. Navishukuru vyama vyote vya siasa chini ya Ukawa, yaani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa mwaliko wao na imani yao na kuthamini mchango ninaoweza kutoa kufanikisha azma ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya kweli ya Taifa letu. Waheshimiwa Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, Mheshimiwa James Mbatia na Emmanuel Makaidi asanteni sana.

Ndugu zangu, sikuufanya uamuzi huu kwa pupa, lakini unafika wakati wa kuchukua maamuzi hata kama ni magumu kwa kuamini fika kuwa ni kwa masilahi ya Taifa letu.

Nimejiridhisha kuwa ndani ya Ukawa Taifa letu linayo fursa ya pekee na ya kihistoria kushinda Uchaguzi Mkuu ujao na ya kuleta mabadiliko ya msingi katika nchi yetu. Kwa uamuzi na ushiriki wangu huu, ninaamini kwa dhati kuwa tutaondoa uhodhi wa madaraka wa chama kimoja na kujenga demokrasia yenye ushindani wa kweli kisiasa.

Namalizia kwa kutoa wito kwa Watanzania wenye nia njema na nchi yetu na wanaotaka kujenga demokrasia na kuleta mageuzi na maendeleo ya kweli, kujiunga nasi katika safari hii mpya ya kuinusuru nchi yetu.

Safari ya Matumaini inaendelea kupitia Ukawa lakini haitafanikiwa iwapo sote hatutajiandisha kupiga kura. Natoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam, kutumia fursa iliyopo kujiandikisha kwa wingi.

Aidha, nawakumbusha Watanzania kote nchini waliojiandikisha kutunza shahada zao na kukumbushana kupiga kura ili ifikapo Oktoba mwaka huu tupate ushindi wa kishindo.

Ndugu zangu Watanzania, tuungane pamoja kuuondoa umaskini na kuleta mabadiliko ya kweli.

NARUDIA CCM SIYO MAMA YANGU

Jumanne, 21 Julai 2015

Masha amkimbia Wenje, amvaa Ngeleja, Arfi aibukia CCM

Tuesday, July 21, 2015


 Makada wa Chadema walioomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Ukonga wakiwa katika mkutano wa uchaguzi kwenye Ukumbi wa Santiago Msongola, Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory
In Summary
Aidha, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Arfi ambaye hivi karibuni alitangaza kujivua uanachama wa chama hicho, amejiunga na CCM na amechukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Nsimbo, Katavi.
By Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar/mikoani. Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya nchi, Lawrence Masha amemkwepa hasimu wake kisiasa, Ezekia Wenje katika Jimbo la Nyamagana, Mwanza na kwenda kugombea ubunge Sengerema ambako atavaana na mbunge anayemaliza muda wake, William Ngeleja.

Aidha, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Arfi ambaye hivi karibuni alitangaza kujivua uanachama wa chama hicho, amejiunga na CCM na amechukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Nsimbo, Katavi.

Masha amkwepa Wenje

Katika uchaguzi uliopita mwaka 2010, Masha aligombea kipindi cha pili katika Jimbo la Nyamagana (CCM), katika mpambano uliokuwa na ushindani mkali na kuangushwa na Wenje wa Chadema.

Awali, kabla ya uchaguzi huo, Masha akiwa waziri mwenye dhamana na mambo ya ndani, alimwekea pingamizi Wenje akidai hakuwa raia, lakini hoja hiyo haikumzuia mshindani wake, badala yake ilimwongezea kura za huruma hadi akaibuka mshindi.

Safari hii Masha amepima maji na kuamua kumvaa waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Ngeleja ambaye hivi karibuni alikuwa miongoni mwa wanaCCM 38 walioomba kuwania urais, lakini akaondolewa katika hatua za awali.

Alipoulizwa jana, Masha alisema amechukua fomu Sengerema kwa sababu ni nyumbani kwao, ndipo alikozaliwa na kukulia, hivyo ameamua kushirikiana nao kusukuma gurudumu la maendeleo.

“Nyamagana pia ni nyumbani, hivyo tutaendelea kushirikiana ili kuleta maendeleo kwa kila jimbo. Sijafanya maridhiano yoyote ya kuachiana jimbo, lakini natumia haki yangu ya kugombea popote,” alisema.

Hata hivyo, hata katika jimbo la Sengerema alikoomba kugombea hayuko salama kutokana na nguvu ya upinzani iliyopo kupitia Chadema ambacho nguvu yake ilidhihirika katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba mwaka jana pale ilipochukua viti vyote katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Sengerema na maeneo mengine ya vijijini.

Mbali na Masha na Ngeleja, wengine waliojitokeza katika jimbo hilo kupitia CCM ni Anna Shija, George Rweyemamu, Philemon Tano, Dk Omari Sukari, Dk Angelina Samike, Jumanne Mabawa, Mussa Malima, Baraka Malebele, Joshua Shimiyu na Zablon Bugingo.

Arfi atimkia CCM

Katibu wa CCM Mkoa wa Katavi, Averin Mushi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Arfi ambaye alikuwa Mbunge wa Mpanda Mjini, ameomba ubunge katika jimbo jipya la Nsimbo lililoko katika Wilaya ya Mlele.

Alisema hadi siku ya mwisho ya kuchukua na kurudisha fomu hizo juzi, makada 23 wa CCM walijitokeza kuomba kuteuliwa kuwania ubunge katika majimbo manne ya uchaguzi yaliyoko Mkoa wa Katavi.

Aliwataja walioomba kuteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Nsimbo kuwa ni Arfi, Shabir Hasanari “Dallah’, Richard Mbogo, Manamba David na Mapesa Frank.

Walioomba kugombea ubunge katika Jimbo la Katavi ni Isaack Kamwelwe, Shafi Mpenda, Maganga Kampala na Oscar Albano.

Katika jimbo jipya la Kavuu ni Zumba Emmanuel, Mselem Said na Prudenciana Kikwembe.

Jimbo la Mpanda Mjini waliochukua na kurejesha fomu ni Sebastian Kapufi, Galus Mgawe na Gabriel Mnyele na katika Jimbo la Mpanda Vijijini ni Moshi Kakoso, Abdallah Sumry, Willy Makufe, Elizabeth Sultan, Godfrey Nkuba, Rock Mgeju na Chifu Charles Malaki.

Bulaya ajipa siku mbili

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya amesema ndani ya saa 48 (kuanzia jana), atatangaza chama ambacho atahamia na kugombea ubunge.

“Ni kweli sigombei kupitia CCM, ila ndani ya siku mbili nitawaambieni chama ambacho nitatumia kugombea ubunge. Haya mambo ya vyama yapo tu na ni njia tu ya kupita, lakini lengo letu ni kuhakikisha tunaleta maendeleo kwa wananchi bungeni.

“Nilipokuwa CCM nilijitahidi kuleta maendeleo, lakini imefika wakati ambao nadhani nitaleta maendeleo zaidi kupitia chama kingine ambacho ndani ya siku mbili mtakijua,” alisema.

Guninita ajitoa

Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita aliyekuwa ameomba kugombea ubunge katika Jimbo la Kilombero ametangaza kujitoa kabla ya kura ya maoni akidai ana shaka na mchakato unavyokwenda.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kilombero, Bakari Mfaume alisema: “Sijapata taarifa ya kujitoa, ndiyo kwanza nasikia kwako, sijapata malalamiko yoyote katika wagombea 20 nilionao kwenye wilaya yangu.

“Guninita alichukua fomu Julai 18 akajaza na kurudisha siku hiyohiyo kisha akaaga kwamba hatohudhuria kikao cha wagombea wote na kamati ya siasa ya wilaya kwa kuwa amepata dharura Dar, nilimkubalia kuwa angejiunga na wenzake kujinadi kwa wanachama katika kampeni za ndani, sasa sijui kimetokea nini,” alisema Mfaume.

Guninita alisema amejitoa kwenye mchakato huo na kuamua kubaki kuwa mwanachama wa kawaida, licha ya kutumia Sh600,000 kwa ajili ya fomu na michango mingine ili kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, alisema pamoja na kuhofia mchakato huo hakusudii kujitoa kwenye chama hicho, badala yake atakuwa bega kwa bega na mgombea atakayepitishwa.

Wengine wanaogombea majimbo mbalimbali ni:

Bagamoyo: Dk Shukuru Kawambwa, Abdul Zahoro, Muharami Mkenge, Salim Abed, Mbonde Mbonde, Mathew Yungwe, Maulid Mtulya, Fabian Said, Lekesani Mvule na Chacha Wambura.

Chalinze: Ridhiwan Kikwete, Iman Madega, Mbaraka Tamimu, Changwa Mkwezu, Omar Kabanga na Hamis Devile.

Kibaha Mjini: Silvestry Koka, Rugemalira Rutatina, Idd Majuto, Rashid Bagdela na Abdulaziz Jadi.

Kibaha Vijijini: Dk Ibrahim Msabaha, Hamoud Jumaa, Bureta Allen, Hussein Chuma, Janeth Munguatosha na Shomary Sangali.

Kahama Mjini: Jumanne Kishimba, Wilbert Nkuba, Deogratius Sazia, Deogratius Mpagama, Adam Ngalawa, Michael Bundala, John Nyenye, Andrew Masanje, Masubo Julius, Luhende Shija na Godwin Kitonka.

Ushetu: Elias Kwandikwa, Isaya Bukakie na Erhard Mlyasi.

Msalala: Ezekiel Maige, John Sukili, Emmanuel Kipole, Nicholaus Magangila, John Lufunga na Wakilala Mashara.

Geita Mjini: Ngara Kanyasu, Daffa Daffa, Dk Samweli Opulukwa, Jacob Mtalitinya, Paschal Malugu, Mathayo Melikiory, Dk Leonard Mugema, Regina Mikenzi, Evarist Nyororo, Juma Malunga na Chacha Mwita.

Geita Vijijini: Jivitius Sabatho, Ernest Mabina, Thoma Ntogwakulya, John Marco, Emmanuel Sherembi na Joseph Msukuma.

Busanda: Tumaini Magesa, Lolesia Bukwimba, Luchenche Mbatilo, Francis Kiganga, John Mhonzu, Sostenes Kulwa na Marko Malembeka.

Buchosa: Dk Charles Tizeba na Eston Malima.

Mbeya Mjini: Christopher Nyenyembe, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Lazaro Mwankemwa.

Kyela: Bernard John, Babylon Mwakyambila, Lusekelo Mwasasumbe, Godfrey Mwakalukwa, Dickson Mwaipopo, Denis Maria, Claud Fungo, Bruno Lupondo, Michael Mwasanga, Clemency Kyando, Alinanuswe Mwalwange na Abraham Mwanyamaki.

Busokelo: Dk Stephen Kimondo, Ambakisye Mwakifwange, Asifiwe Mwakalobo, Isack Mwambona, Boniface Mwabukusi, Elias Mwakapimba, Simon Mwamaso na Elisha Mwambapa.

Rungwe: Deogratius Mwailenge, Ayubu Mwakasole, Nicodemas Ngwala, Ahobokile Mwaitenda, Sophia Mwakagenda, John Mwambigija, Barnaba Pomboma, Brown Mwaipasi, Yassin Mwakisole, Festo Mwaipaja, Christopher Kitweka, Richard Mbalase, Wilfredy Mwaipyana, Bertha Mwakasege, Daud Mwasanga na Yusuph Asukile.

Mbarali: Jidawaya Kazamoyo, Dickson Baragasi, Grace Mboka, Tazan Ndingo, Rajab Msingo, Liberatus Mwang’ombe na Ronilick Chami.

Lupa: Victor Kinyonga, Ernest Mwamengo, Philipo Mwakibingo, Enock Mageta, Emil Mwangwa, Sande Sanga, Moses Mwaifunga, Mohamed Hussein, Jamson Mwiligumo, Njelu Kasaka, George Mwaipungu na Peter Noah.

Mbozi: Eliud Msongole, Abraham Msyete, Solomon Kibona, Eliud Kibona, Zablon Nzunda, Abdul Nindi, Anastazia Nzowa, Happiness Kwilabya, Fannuel Mkisi, Furaha Mwazembe, Gift Kalinga, Pascal Haonga, Andrew Bukuku, Ambakisye Kabango, Stephen Mwakingili, Jerald Silwimba, Fadhil Shombe, Jonathan Mwashilindi, Fredy Haonga, Bob Mwampashe, Ostern Meru, Sophia Mwabenga, Mochael Mtafya, Mchungaji Wilhelm Mwakavanga, Seule Nzowa na Dickson Kibona.

Mbeya Vijijini: Moses Mwaigaga, Chance Mwaikambo, Franco Mwalutende, William Msokwa, Stephano Mwandiga, Frank Mwaisumbe, Elias Kwimba, Antony Mwaselela, Wila Jacob, John Mwamengo, Jeremiah Mwaweza, Adson Sheyo, Emmanuel Shonyela, Alimu Mwasile, Adam Zella, Nhungo Jisandu, Daud Mponzi na Cyprian Magulu.

Ileje: Nicolaus Mtindya, Emmanuel Mbuba, Emmanuel Msyani, Gwamaka Mbughi, Cosmas Sikinga, Leornad Fumbo, Joel Kajinga na Riziki Mbembela.

Songwe: Mpoki Mwankusye, Michael Nyilawila, John Mwaniwasa, Ofugan Wanga na Frank Mwakitalima.

Babati Vijijini: Omary Kwaang’, Damas Nakey, Vrajlal Jituson, Hassan Kaniki, Vencent Naano, Faustine George, Mary Geai, Charles Ingi, Jamal Mukta, Valerian Margwe, Atanas Kijuu, Stephano Manda, Daniel Sulle, Laurent Tara, Ester Sarwat, Leonard Mao, Daniel Marko, Herman Sanka, Salum Shawishi. Christina Kembe, Ester Sarwat na Respikia Muna (viti maalumu).

Babati Mjini: Kisyeri Chambiri, Haines Darebe, Ally Msuya, Ally Sumary, Sulei Doita, Samo Samo, Cosmas Masauda, Ramadhan Slaa, Paulina Gekul na Gabriel Kimolo.

Hanang’: Dk Mary Nagu, Dk Eliamani Sedoyeka, Peter Nyalandu, Deusdedit Mayomba, Derick Magoma, Nada Shauri, Cyiril Ako, Leonard Guti, Whilhelem Gidabudai, Dk Haite Samo na Rose Kamili anayegombea viti maalumu.

Mbulu Mjini: Zacharia Isaay, Peter Pareso, Andrew Aqweso na Juma Marmo.

Mbulu Vijijini: Fratley Gregory, Martha Umbulla, Malkiani Nari, Dk Isack Maleyeki na Simon Daffi.

Simanjiro: Christopher Ole Sendeka, Peter Toima, Simon Ndwala na James Ole Millya.

Kiteto: Benedict Ole Nangoro, Emmanuel Papien, Amina Mrisho, Joseph Mwaseba na Ally Lugendo.

Ukerewe: Sumbuko Chipanda, Osward Mwizalubi, Christopher Nyandiga, Deogratias Lyato, Dk Elias Misana, John Mkungu, Magesa Boniphace, Hezron Tungaraza, Dk Deusdedit Makalius, Marick Marupu, Laurent Munyu, Bigambo Mahendeka, Bandoma Kabulile, Gerald Robert na Emerciana Mkumbulo.

Bariadi: Andrew Chenge, Masanja Kadogosa, Cosmas Chenya na Joram Masanja.

Meatu: Donald Masanga, Oscar Paul, Romana Kitija na Salum Mbuzi.

Itilima: Daud Njalu, Masanja Ngangani, Dani Makanga, Kulwa Njanja na Hilu Kibilu.

Kisesa: Ruhaga Mpina

Maswa Mashariki: Michael Jilala, Mashimba Ndaki, Benjamin Tungu, Aron Mboje na Henry Nditi.

Maswa Magharibi: Jonathan Ngela, Stanslaus Nyongo, Ally Mtegwa, George Lugomelo, Edward Bunyongoli na George Nangale.

Busega: Dk Titus Kamani, Dk Rafael Chegeni, Bernard Kibese, Igo Shing’ombe, Dismas Shwea, Robert Nyanda, Nyangi Msemakweli na Josephat Mkwabi.

Njombe Kusini: Edward Mwalongo, Alfred Luvanda, Arnold Mtewele, Vitalis Konga, Mariano Mwanyigu, Romanus Mayemba, Deiniol Msemwa na Hassan Mkwawa.

Njombe Kaskazini: Laula Malekela, Emmanuel Nyagawa, Joram Hongoli, Lemah Hongoli, Osmund Malekela, Mussa Mgata, Gaston Kaduma, Avike Kyenga na Oscar Msigwa.

Ludewa: Deo Filikunjombe, Zephania Chaula na Kapteni Mstaafu Jacob Mpangala.

Makete: Dk Binilith Mahenge, Dk Noman Sigala, Lufunyo Kinda, Bonic Mhami na Fabian Mkingwa.

Wanging’ombe: Gerson Lwenge, Thomas Nyimbo, Yono Kevela, Kenned Mpumilwa, Malumbo Mangula, Abraham Chaula, Richard Magenge, Petro Dudange, Hoseana Lunogelo, Nobchard Msigwa, Eston Ngilangwa na Abel Badi.

Makambako: Deo Sanga na Alimwimike Sahwi.

Viti Maalumu Njombe: Pindi Chana, Neema Mgaya, Nebo Mwina, Rosemary Staki, Suzan Kolimba, Margaret Kyando na Erica Sanga.

Kilombero: Kanali mstaafu Harun Kondo, Vitus Lipagila na Abdullah Lyana, Oscar Mazengo, Japhet Mswaki, Paul Mfungahema, Abubakari Asenga na Abdul Mteketa.

Imeandikwa na Julieth Ngarabali, Faustin Fabian, Jovither Kaijage

Jumatatu, 20 Julai 2015

Vita kali ya ubunge CCM, Chadema


Monday, July 20, 2015




Mchuano mwingine mkali unatarajiwa kuwapo katika Jimbo la Bunda Mjini ambako Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira atavaana na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (pichani).
In Summary
Hadi jana, ambayo ilikuwa ni siku ya mwisho kwa vyama hivyo kuchukua na kurejesha fomu, jambo moja lilijidhihirisha katika baadhi ya majimbo kwa upande wa CCM; baadhi ya majina makubwa katika siasa za ubunge yanachuana hivyo kufanya mchakato wa kumpata mteule mmoja kuwa mgumu.

Dar/mikoani. Baada ya mchakato wa kuwania urais, sasa vita ya Uchaguzi Mkuu imehamia kwenye ubunge na udiwani hasa kutoka katika vyama vikubwa vya CCM kinachotawala na Chadema kinachoongoza upinzani.

Hadi jana, ambayo ilikuwa ni siku ya mwisho kwa vyama hivyo kuchukua na kurejesha fomu, jambo moja lilijidhihirisha katika baadhi ya majimbo kwa upande wa CCM; baadhi ya majina makubwa katika siasa za ubunge yanachuana hivyo kufanya mchakato wa kumpata mteule mmoja kuwa mgumu.

Mchuano huo na kuimarika kwa Chadema mikoani hasa kutokana na majeraha ya mchakato wa urais ndani ya CCM, vinaufanya upinzani wa kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuwa sawa na vita.

Nzega Vijijini

Makada wawili wa chama hicho, Lucas Selelii na Dk Hamisi Kigwangalla wamechukua fomu kuwania ubunge wa Nzega Vijijini.

Katika uchaguzi uliopita wa 2010, makada hao walivaana katika Jimbo la Nzega lakini wote wakaangushwa na Hussein Bashe aliyeibuka wa kwanza akifuatiwa na Selelii.

Hata hivyo, matokeo hayo yalibatilishwa na Halmashauri Kuu ya CCM na kumchukua Dk Kigwangalla aliyekuwa mshindi wa tatu.

Mgawanyo wa majimbo uliofanywa wiki iliyopita na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), umerahisisha mpambano wa makada hao, hivyo wawili hao wakamwachia Bashe Nzega Mjini.

Akichukua fomu hiyo jana, katika ofisi za CCM za Wilaya ya Nzega, Dk Kigwangalla akiwa ameambatana na wazee wa jimbo hilo, alisema shinikizo la kugombea Nzega Vijijini limetoka kwa wananchi wanaotambua umuhimu wake.

Selelii aliyekuwa Mbunge wa Nzega kwa miaka 15 hadi 2010, alichukua fomu kimyakimya bila kuzungumza na vyombo vya habari.

Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega, Empimark Makuya alithibitisha kuwa kada huyo alishachukua fomu. Wawili hao watakabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wengine wawili waliochukua fomu, John Dotto na Paul Kabelele.

Maiga aibukia Iringa

Baada ya kukwama katika harakati za kuwania urais kupitia CCM, Balozi Dk Augustine Mahiga amejitokeza kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini.

Dk Mahiga aliyechukua fomu jana na kurudisha, atapambana na Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Jesca Msambatavangu, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela na mwandishi wa habari, Frank Kibiki ambao tayari wamechukua na kurejesha fomu zao.

Mchuano katika jimbo hilo unatarajiwa kuwa mkali wakati na baada ya kura za maoni ndani ya CCM hasa ikizingatiwa kwamba Mwakalebela alikuwa amechukua namba moja katika kura za maoni za chama hicho mwaka 2010 kabla ya jina lake kukatwa na NEC.

Mshindi atakuwa na wakati mgumu kukabiliana na kishindo cha upinzani hasa kutoka Chadema ambako Mchungaji Peter Msigwa aliyeshinda katika uchaguzi uliopita, jana alipokewa na umati mkubwa wa watu alipowasili mjini hapo.

Profesa Maghembe na Thadayo tena

Mshikemshike mwingine unatarajiwa kuibuka katika Jimbo la Mwanga ambako Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe anatarajiwa kupambana tena na hasimu wake mkubwa katika kiti hicho, Joseph Thadayo.

Katika uchaguzi wa 2010, Profesa Maghembe alimshinda Wakili huyo ambaye alionekana kuungwa mkono na wanasiasa wengine wenye nguvu katika jimbo hilo. Mbali yao wengine waliojitokeza ni Aminieli Kibali na Karia Magaro.

Wasira, Bulaya wavaana

Mchuano mwingine mkali unatarajiwa kuwapo katika Jimbo la Bunda Mjini ambako Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira atavaana na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya.

Wabunge hao wa CCM wamekuwa wakitambiana muda mrefu na wakati mwingine waliwahi kurushiana maneno hadi bungeni, lakini mwisho wa tambo zote ni kwenye kura za maoni.

Mamia warejesha fomu

Hadi muda wa mwisho wa kurejesha fomu unakamilika saa 10 jioni jana, mamia ya makada wa Chadema na CCM walikuwa wamejitokeza na kudhihirisha kuwa mchuano utakuwa mkali katika kura za maoni na hata kwenye uchaguzi wenyewe.

Kawe 22: Elias Nawera, Dk Walter Nnko, Jumaa Muhina, Kippi Warioba, Atulinda Barongo, Tegemeo Sambili, Kiganga George, Edmund Lyatuu, Charles Makongoro Nyerere, Mtiti Butiku, Yusuf Nassoro, John Mayanga, Dickson Muze, Dk Wilson Babyebonela, Colman Massawe, Amon Mpanji, Amelchiory Kulwizira, Gabriel Mnasa, Abdallah Majura na Jerry Murro, wote wakikabiliana na Halima Mdee aliyejitokeza pekee Chadema, hasa iwapo atasimama pekee kupitia Ukawa.

Kinondoni 12: Idd Azan, Wagota Salum, Tonny Kalijuna, Goodchange Msangi, Emmanuel Makene, Lusajo Willy, Mage Kimambi, Mussa Mwambujule, Stevew Nengere (Steve Nyerere), Joseph Muhonda, Michael Wambura na Macdonald Lunyiliga.

Ubungo 12: Vincent Mabiki, Timoth Machibya, Jordan Baringo, Emmanuel Mboma, Zangina Zangina, Kalist Ngalo, Hawa Ng’umbi, Jackson Millengo, Didas Masaburi, Joseph Massana, wote wa CCM wakitarajiwa kumkabili John Mnyika wa Chadema.

Ilala watatu: Mussa Azzan Zungu, Mrisho Gambo na Waziri Kindamba.

Ukonga 16: Jerry Silaa, Jacob Katama, Hamza Mshindo, Frederick Rwegasira, Anthony Kalokola, Ramesh Patel, Peter Majura, Amina Mkono, Edwin Moses, Robert Masegese, John Bachuta, Edward Rabson, Nickson Tugale, Elly Ballas, Asia Msangi, Lucas Otieno, Fredrick Kabati, Mwanaidi Maghohe, Mwita Waitara, Deogratius Munishi, Deogratius Kalinga, Deogratius Mramba, Salanga Kimbaga, James Nyakisagana, Lameck Kiyenze na Gaston Makweta.

Segerea 13: Zahoro Lyasuka, Apruna Humba, Bona Kalua, Nicholaus Haule, Baraka Omary, Benedict Kataluga, Dk Makongoro Mahanga na Joseph Kessy.

Kigamboni 10: Aron Othman, Kiaga Kiboko, Abdallah Mwinyi, Dk Faustine Ndugulile, Ndahaye Mafu, Flora Yongolo, David Sheba, Mohammed Ally Mchekwa, Khatib Zombe na Adili Sunday.

Mbagala 23: Lucas Malegeli, Mindi Kuchilungulo, Kazimbaya Makwega, Adadius Richard, Tambwe Hiza, Issa Mangungu, Ingawaje Kajumba, Siega Kiboko, Peter Nyalali, Mwinchumu Msomi, Dominic Haule, Aman Mulika, Banda Sonoko, John Kibasso, Ally Makwiro, Alvaro Kigongo, Maesh Bolisha, Kivuma Msangi, Deus Sere, Abdulrahim Abbas, Salum Seif Rupia, Ally Mhando, Fares Magessa, Stuwart Matola.

Moshi: Priscus Tarimo, Amani Ngowi, Patrick Boisafi, Davis Mosha, Buni Ramole, Halifa Kiwango, Michael Mwita, Daud Mrindoko, Shanel Ngunda, Innocent Siriwa, Edmund Rutaraka, Omari Mwariko, Basil Lema, Jaffar Michael na Wakili Elikunda Kipoko.

Busokelo: Suma Mwakasitu , Dk Stephen Mwakajumilo, Ezekiel Gwatengile, Mwalimu Juma Kaponda, Ally Mwakibolwa, Issa Mwakasendo, Aden Mwakyonde na Lusubilo Mwakibibi.

Kilombero: Kanali mstaafu Harun Kondo, Vitus Lipagila, Abdullah Lyana, Oscar Mazengo, Japhet Mswaki, Paul Mfungahema, John Guninita, Abubakari Asenga na Abdul Mteketa.

Mlimba: Dk Frederick Sagamiko, Senorina Kateule, Godwin Kunambi, Augustino Kusalika, George Swevetta, Castor Ligallama, Profesa Jumanne Mhoma, Fred Mwasakilale, Dismas Lyassa.

Namtumbo: Edwin Ngonyani, Edwin Milinga, Mwinyiheri Ndimbo, Vita Kawawa, Anselio Nchimbi, Julius Lwena, Fitan Kilowoko, Balozi Salome Sijaona, Mussa Chowo, Salum Omera, Ally Mbawala na Charles Fussi.

Tunduru Kaskazini: Mhandisi Ramo Makani, Omary Kalolo, Michael Matomola, Hassan Kungu, Issa Mpua, Rashid Mandoa, Athuman Mkinde, Shaban Mlono na Moses Kulawayo.

Tunduru Kusini: Abdallah Mtutura, Daim Mpakate na Mtamila Achukuo.

Nyasa: Christopher Chale, Bethard Haule, Adolph Kumburu, Alex Shauri, Frank Mvunjapori, Dk Steven Maluka, Stella Manyanya, Cassian Njowoka, Jarome Betty na Oddo Mwisho.

Serengeti: Dk Stephen Kebwe, Dk James Wanyancha, Juma Kobecha na Mabenga Magonera.

Sumbawanga Mjini: Aeshi Hilaly, Anyosisye Kiluswa, Fortunata Fwema, Mathias Koni, Gilbert Simya, Frank Mwalembe, Selis Ndasi, Mbona Mpaye, Sospeter Kansapa, Paschal Sanga na Victor Vitus.

Korogwe Vijijini: Stephen Ngonyani (Profesa Majimarefu), Cesilia Korassa, Allan Bendera, Ali Mussa Moza, Abdallah Nyangasa, Christopher Shekiondo, Andrew Matili, Edmund Mndolwa, Ernest Kimaya, Peter Mfumya na Stephen Shetuhi.

Kilindi: Beatrice Shellukindo, Abdallah Kidunda, Fikirini Masokola na Dk Aisha Kigoda.

Bariadi Mashariki: Masanja Kadogosa na Joram Masaga.

Mbulu: Mary Margwe amechukua fomu ya kugombea ubunge wa viti maalumu

Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye na yule wa Kilosa Kati, Mustafa Mkulo hawakujitokeza kuchukua fomu.

Imeandikwa na Julius Mathias, Bakari Kiango, Godfrey Kahango, Ngollo John, Salim Mohammed, Joseph Lyimo, Faustine Fabian, Joyce Joliga, Daniel Mjema, Burhani Yakub, Antony Mayunga, Mussa Mwangoka na Mustapha Kapalata

Msigwa asimamisha shughuli Iringa



In Summary
Msigwa ambaye alitumia mkutano huo kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama chake kugombea tena ubunge alisema kitendo chake cha kuwaelimisha wananchi juu ya haki zao ndicho kilichosababisha wakazi wa Mji wa Iringa kutowaogopa polisi wala wakuu wa wilaya kama ilivyokuwa zamani.
By Geofrey Nyanga’oro, Mwananchi

Iringa. Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa jana alisimamisha kwa muda, shughuli za maelfu ya wakazi wa jimbo hilo ambao walijitokeza kumsikiliza katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru ambao aliutumia kuelezea mafanikio aliyopata katika kipindi cha miaka mitano ikiwamo ya kuwafanya wajue haki zao.

Msigwa ambaye alitumia mkutano huo kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama chake kugombea tena ubunge alisema kitendo chake cha kuwaelimisha wananchi juu ya haki zao ndicho kilichosababisha wakazi wa Mji wa Iringa kutowaogopa polisi wala wakuu wa wilaya kama ilivyokuwa zamani.

“Ipo tofauti kati ya kiongozi na mwanasiasa, kiongozi ni yule ambaye mambo yake yanafikiria karne lakini mwanasiasa yeye hufikiria uchaguzi pekee, mtu anayefikiria masuala ya muda mrefu anawekeza kwa watu… ndiyo sababu leo wakazi wa Iringa wamejua haki zao,” alisema.

“Katika kipindi cha miaka mitano tulilia pamoja na kucheka pamoja, wengi wanakumbuka nilipowasaidia Machinga pale Mashine Tatu, tulikamatwa pamoja na kuwekwa ndani pamoja, mbunge gani anaweza kukubali kulala ndani kwa ajili ya watu wake? Nilifanya vile si kwa sababu sikuwa na mahali pazuri pa kulala, bali nilitaka watu mpate haki zenu kwa kuwa mimi niligombea nikitaka kuwa sauti ya wanyonge.”

Msigwa alisema kutokana na uelewa huo, wakazi wa Iringa waligoma kuchangia michango ya Mbio za Mwenge... “Nilipokuja kuwaambia hakuna kuchagia Mbio za Mwenge, nani alichangia hapa?.... (hakuna) nani alikamatwa kwa ajili ya kukataa kuchangia mchango huo? (hakuna) hiyo ni miongoni mwa kazi kubwa niliyoifanya.” Alisema yeye na wabunge wenzake wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kupandisha hadhi na heshima ya Bunge tofauti na mabunge yaliyopita kutokana na kujituma kwao kuwatumikia wananchi... “Tulikwenda bungeni tukakuta wabunge wanalala, tumewaamsha, hawasomi tumewafanya wanasoma, wanaogopa Serikali tumewafanya hawaogopi hata baadhi ya wabunge wa CCM kuthubutu kuikosoa Serikali yao.”

Alisema Taifa limebaki katika dimbwi la umaskini kutokana na kuongozwa na wanasiasa ambao wanafikiria uchaguzi na si masuala ya muda mrefu ya nchi na ndiyo sababu Rais Jakaya Kikwete alitumia takriban saa mbili kuzungumzia miradi wakati wa hotuba yake ya kuhitimisha Bunge.

“Leo hii tunamkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere siyo kwa sababu alijenga daraja ama uwanja ni kwa kazi yake ya kuwekeza kwa watu na ndiyo sababu sote tunakubali kuwa ni Baba wa Taifa,” alisema.

Achangiwa Sh5.1 milioni

Wananchi waliohudhuria mkutano huo walichanga Sh5.1 milioni ambazo zilitangazwa kwenye mkutano huo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Ufuatiliaji Shughuli za Bunge ya Chadema, Marcossy Albanie ambaye alisema ni kwa ajili ya kuchukulia fomu.

Mke wa Msigwa hadharani

Kwa mara ya kwanza, mke wa mbunge huyo, Kissa Msigwa alisimama jukwaani na kutoa shukrani kwa wakazi wa Iringa kwa kumpa nafasi ya uwakilishi mumewe.

Huku akishangiliwa Kissa alisema: “Ninawashukuru wakazi wa Iringa kwa kumchagua... amewakilisha vizuri naomba mmpatie tena miaka mitano ili aweze kuifanya kazi hiyo.”

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye aliongozana na Msigwa alitumia muda mwingi kwa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akisema hataweza kupambana na nguvu ya Ukawa itakayoongozwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa.

Mbilinyi alisema hivi karibuni Ukawa itatangaza mgombea urais huku akisema Dk Slaa ni jembe.

Kuhusu Msigwa, Mbilinyi alisema ni miongoni mwa wabunge ambao Iringa na Taifa linawategemea na kuwaomba wakazi wa Iringa Mjini kutompoteza.

Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha ), Grace Tendega alisema upinzani utaibuka na ushindi mwaka huu... “Kama mnavyoona katika majimbo ya Monduli na Bariadi, hali hiyo bado na itaendelea nchi nzima, watu wamechoshwa na CCM na sasa wameamua kuja Chadema na muda si mrefu tutatangaza mgombea mtamuona na atashinda Uchaguzi Mkuu mwaka huu.”

Mwenyekiti wa Chadema Iringa Mjini, Frank Nyalusi alisema: “Katika kipindi cha uongozi wake, Msigwa miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa.”

Jumamosi, 18 Julai 2015

Mgombea ‘wa nne’ aivuruga Ukawa



  1. Dk Kahangwa amechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. 
    Na Fidelis Butahe, Mwananchi
    Kwa ufupi
    • Ndiye amesababisha vyama hivyo vinne vishindwe kutangaza jina mapema kama vilivyoahidi
    • Hali imeendelea kuwa ngumu kwa upande wa Ukawa ambao hadi sasa wameshindwa kumtaja mgombea wao 
    Dar es Salaam. Wakati wa hali ya sintofahamu ikiwa imetawala uteuzi wa mgombea atakayeungwa mkono na vyama vinne vya upinzani, imebainika kuwa mzozo unaochelewesha suala hilo ni mgombea ambaye Chadema haijamuweka bayana.
    Katibu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye ambaye anapewa nafasi kubwa ya kupitishwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa mbele ya mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na kada wa NCCR-Mageuzi, Dk George Kahangwa, lakini hadi sasa vyama hivyo bado vinasita kumtangaza mteule wake.
    Profesa Lipumba alikuwa amewaahidi waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa mgombea ambaye ataungwa mkono na vyama hivyo vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD angetangazwa Julai 14, lakini siku hiyo hakuna aliyetangazwa.
    Badala yake viongozi wa Chadema, NLD na NCCR ndio waliofika Hoteli ya Coloseum jijini Dar es Salaam ambako Profesa Lipumba aliahidi kuwa ndiko jina la mgombea huyo lingetajwa, wakati viongozi wa CUF hawakuonekana na baadaye jioni wakasema kuwa walikuwa na kikao cha ndani ya chama cha kutafuta ufumbuzi wa mambo ambayo walikuwa hawajakubaliana.
    Vyama hivyo vitatu vikaeleza baadaye kuwa jina hilo litatangazwa ndani ya siku saba kuanzia Julai 14, lakini siku iliyofuata CUF ilisema suala la kuachia chama kingine jukumu la kusimamisha mgombea urais litawasilishwa  kwenye kikao cha Baraza Kuu la chama hicho ambacho kitafanyika Julai 25, jambo ambalo lilikubaliwa na vyama hivyo vitatu.
    Matamko hayo yamefanya suala la mgombea urais wa Ukawa kugubikwa na giza nene, lakini kwa siku tatu Mwananchi imefuatilia na kubaini kuwa mgombea ambaye yuko na hajatajwa rasmi kwa vyama hivyo vinne ndiye anayechelewesha mchakato huo na amesababisha kuwapo na hatari ya umoja huo kuparaganyika.
    Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya vikao vya Ukawa vilivyoanza kufanyika takribani wiki mbili jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa licha ya viongozi wa vyama hivyo kumpata mgombea wao wa urais katika kikao cha Julai 14 mwaka huu, walikwama kumtangaza kutokana na CUF kutokuwapo kikaoni ikielezwa kuwa wanapinga maendeleo ya mchakato huo.
    Taarifa hizo zinaeleza kuwa msimamo huo wa CUF umetokana na utata ulioibuka katika kikao cha Ukawa cha Julai 11 na 14,  baada ya wagombea wawili kati ya watatu, kukubali mmoja wao agombee urais, lakini chama chake kikasema kuwa kinachotakiwa ni Ukawa kutangaza jina la chama kitakachotoa mgombea na si jina la mgombea.
    Tayari Profesa Lipumba ameshachukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CUF, wakati Dk Kahangwa amechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, huku mchakato wa Chadema ukiwa haujaanza.
    Habari hizo zinaeleza kuwa awali kulikuwa na mvutano mkali kati ya Profesa Lipumba na Dk Slaa na kwamba katika kikao cha Julai 11, Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa CUF alikubali kumuachia Dk Slaa agombee urais kupitia Ukawa, lakini inaonekana hata ndani ya Chadema bado hawajaafikiana kuhusu jina la mgombea.
    Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kuwa jina la mgombea urais limeshapatikana na linasubiri muda muafaka.
    “Tutamtangaza mgombea urais wa Ukawa ndani ya wiki moja kama tulivyosema awali,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika jana.
    ananchi wanatakiwa kutulia tu, siku ikifika tutatangaza.”
    Mnyika alitoa ufafanuzi huo muda mfupi baada ya kulieleza gazeti hili jana kwamba wanaopaswa kuzungumzia suala hilo ni Dk Slaa na Profesa Lipumba.
    Jibu kama hilo la Mnyika lilitolewa pia na mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alipoulizwa kuhusu habari kwamba kuna jina la mgombea urais linalosumbua Ukawa.
    “Sijui chochote kuhusu hilo. Ila watu hawa wawili, Mbowe na Dk Slaa watakusaidia kujua kuhusu jambo hilo.”
    Alipobanwa zaidi, alisema: “Unajua hata mimi nazisikia sana habari kama hizo pamoja na nyingine nyingi. Katika Ukawa watu wanazungumza ndani ya vikao na nje ya vikao, ila wa kulithibitisha hilo ni hao watu wawili niliokutajia.”
    Lakini mpashaji habari wetu alisema ugumu wa kumpata mgombea urais wa Ukawa kutoka Chadema unasababishwa na chama hicho kutotaka kuweka bayana jina la mtu atakayebeba jukumu hilo wakati wameshakubaliana kuwa Dk Slaa ndiye asimamishwe.
    “Inaonekana kama kuna mtu mwingine hivi. Wote tumekubali mgombea awe Dk Slaa, lakini Chadema wenyewe wanazuia asitangazwe,” alisema mpashaji huyo kutoka ndani ya vikao vya Ukawa.
    Habari zaidi zinaeleza kuwa ndani ya Chadema kuna mvutano, kwani wapo wanaotaka Dk Slaa atangazwe kuwa ndiye mgombea na wanaotaka asitangazwe lakini hawaweki bayana kuwa hawamtaki au wanataka mtu mwingine.
    Hata hivyo, habari hizo zinasema kuwa sababu nyingine inayochelewesha suala hilo ni Chadema kutotaka kumtangaza mgombea wake kutokana na mchakato wake wa uteuzi wa mgombea urais kutoanza. Mchakato huo utaanza Julai 20 na kumalizika Julai 25, siku ambayo CUF itakuwa na kikao chake cha Baraza Kuu kuamua mgombea urais.
    Habari zinasema kuwa Chadema imekuwa ikisisitiza kuwa Ukawa itaje jina la chama kitakachotoa mgombea urais na si jina la mwanachama atakayegombea nafasi hiyo.
    Habari hizo zinaeleza kuwa chama hicho kinachoongoza kambi ya upinzani, kinadai kuwa Ukawa kutangaza jina la mwanachama atakayegombea urais ni kuingilia mchakato wa Chadema ambao humalizika kwa kikao cha juu kupitisha mgombea urais wa chama.
    Awali baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya CUF, Profesa Lipumba alikuwa akisema kwenye mikutano ya hadhara kuwa vyama hivyo vinne vimekubaliana kuwa kila kimoja kifanye mchakato wake wa kupata mgombea. Alisema kila chama kitalazimika kupeleka Tume ya Uchaguzi (NEC) jina la mgombea wake ili kiwe na uhakika kuwa amepitishwa halafu ndipo vikutane na kuamua mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote.
    « Previous Page
    http://www.magazetini.com/Soma vichwa vya habari vya magazeti ya Tanzania yote sehemu moja. Read Tanzania News Headlines here.
  2. http://millardayo.com/Stori zote kwenye Magazeti ya Tanzania July 18 2015 >>> Udaku, Michezo na Hardnews niko nazo hapa. Good morning mtu wa nguvu.. millardayo.com huwa ...
  3. http://www.mwananchi.co.tz/Skip to the navigationchannel.links.navigation.skip.label. Skip to the content. MCL Blog | Daily Nation | NTV | Business Daily | The East African | Daily Monitor  ...
  4. http://www.mjengwablog.com/Magazeti ya Leo. Magazeti ya leo. BOFYA HAPA KUISOMA. Matangazo Mapya. Website Design · Huduma. We provide the full IT solutions including web design  ...

magazeti ya leo tar 18/07/2015


  1. http://www.magazetini.com/Soma vichwa vya habari vya magazeti ya Tanzania yote sehemu moja. Read Tanzania News Headlines here.
  2. http://millardayo.com/Stori zote kwenye Magazeti ya Tanzania July 18 2015 >>> Udaku, Michezo na Hardnews niko nazo hapa. Good morning mtu wa nguvu.. millardayo.com huwa ...
  3. http://www.mwananchi.co.tz/Skip to the navigationchannel.links.navigation.skip.label. Skip to the content. MCL Blog | Daily Nation | NTV | Business Daily | The East African | Daily Monitor  ...
  4. http://www.mjengwablog.com/Magazeti ya Leo. Magazeti ya leo. BOFYA HAPA KUISOMA. Matangazo Mapya. Website Design · Huduma. We provide the full IT solutions including web design  ...