ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 7 Aprili 2016

Mpango wa bajeti ya Tanzania 2016/2017 nouma zaidi ya trilion tano zaongezeka

Imeandikwa na Waandishi Wetu
SERIKALI imewasilisha mbele ya wabunge wote Mapendekezo ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2016/2017, inayotarajiwa kuwa ya Sh trilioni 29.539. Kiasi hicho cha bajeti ya mwaka ujao wa fedha, kinatofautiana na bajeti ya mwaka huu wa fedha unaomalizika kwa takribani Sh trilioni tano.
Katika bajeti ya mwaka huu unaoishia, jumla ya Sh trilioni 22.495 zilitengwa kwa ajili ya bajeti nzima kutoka vyanzo vya ndani na nje. Mapendekezo ya mwaka ujao, ambayo yametajwa na baadhi ya wadau wa masuala ya siasa kuwa ni hatua kubwa na nzuri ya serikali, yanaonesha Serikali inalenga kutumia Sh trilioni 15.105, sawa na asilimia 82 ya mapato ya ndani. Mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ni Sh trilioni 2.693 na mapato kutoka halmashauri ni Sh bilioni 665.4.
Fedha za washirika wa maendeleo zinazotarajiwa ni Sh trilioni 3.600, ambayo ni sawa na asilimia 12 ya bajeti yote. Akiwasilisha mapendekezo ya ukomo wa bajeti hiyo katika mkutano wa wabunge wote jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango, alitaja vipaumbele vya bajeti hiyo kuwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2016/2017 wa miaka mitano.
Viwanda, ulipaji madeni Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu na mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara.
Alisema bajeti hiyo, pia itaweka mkazo zaidi katika ukamilishaji wa miradi inayoendelea, miradi mipya, ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa na utekelezaji wa maeneo yote ya vipaumbele, yaliyoainishwa katika Mpango huo wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.
Akizungumzia mfumo wa bajeti hiyo, Waziri huyo alisema pamoja na michango ya ndani, pia washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.600 sawa na asilimia 12 ya bajeti yote ambayo ni misaada na mikopo, inayojumuisha miradi ya maendeleo, mifuko ya pamoja ya kisekta na ya kibajeti.
“Pia Serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 5.374 kutoka soko la ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva pamoja na mikopo mipya kwa ajili kugharimia miradi ya maendeleo ya pamoja na kulipia malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa.
Mkopo nje “Vilevile ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 2.101 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara,” alisisitiza Dk Mpango.
Akichanganua mapendekezo hayo ya bajeti, alisema kwa upande wa matumizi katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inapanga kutumia Sh trilioni 17.719 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh trilioni 11.820 kwa matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 40 ya bajeti yote. Aidha kiasi cha Sh trilioni 8.702 ni kwa ajili ya fedha za ndani na Sh trilioni 3.117 ni fedha za nje.
Bajeti inayomalizika Katika bajeti ya mwaka huu unaoishia, jumla ya Sh trilioni 22.495 zilitengwa kwa ajili bajeti nzima kutoka vyanzo vya nje na ndani. Jumla ya Sh trilioni 8.987 zilikuwa ni makusanyo ya ndani, halmashauri zikijumuishwa, sawa na asilimia 97 ya makadirio ya kukusanya Sh trilioni 9.281 katika kipindi hicho.
Dk Mpango alifafanua kuwa katika bajeti hiyo, mapato ya kodi yalikuwa ni Sh trilioni 7.931 sawa na asilimia 99 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 8.016 kwa kipindi hicho.
Alisema mapato yasiyo ya kodi, yalikuwa Sh bilioni 786.1 sawa na asilimia 86 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 916.1. Mapato yaliyokusanywa na halmashauri, yalikuwa Sh bilioni 270 sawa na asilimia 78 ya makadirio ya Sh bilioni 347.9 kwa kipindi hicho.
Alisema kwa mujibu wa matarajio ya bajeti hiyo, washirika wa maendeleo waliahidi kutoa Sh trilioni 2.322 kama misaada na mikopo nafuu, lakini hadi kufikia Februari mwaka huu, walitoa jumla ya Sh trilioni 1.017 ambazo ni sawa na asilimia 62.5 ya malengo.
Alisema Serikali ilitarajia kukopa mikopo yenye masharti nafuu ya kibiashara kutoka vyanzo vya nje na ndani jumla ya Sh trilioni 6.175.
Alisema kutofikiwa kwa malengo ya mikopo ya kibajeti, kulitokana na baadhi ya washirika wa maendeleo kupunguza ahadi zao, kuweka masharti mapya na wengine kuamua kutotoa fedha walizoahidi kwa sababu ya kubadilika kwa sera za ndani za nchi zao zinazohusu misaada kwa nchi zinazoendelea.
Aidha alisema hadi kufikia Februari mwaka huu, Serikali ilishakopa cha Sh trilioni 3.688 ikiwa ni asilimia 101 ya kiasi kilichopangwa kukopwa katika kipindi hicho.
Kati ya kiasi hicho Sh trilioni 2.133 zilikopwa kwa ajili ya kulipia amana za Serikali zilizoiva na mikopo mipya ilikuwa ni Sh trilioni 1.554 sawa na asilimia 101 ya kiasi kilichopangwa kukopwa.
Akizungumzia mgawanyo wa fedha za bajeti hiyo inayoishia, Dk Mpango alisema Serikali ilitoa mgawo wa Sh trilioni 13.152 kwenda kwenye mafungu mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti hiyo sawa na asilimia 92 ya makadirio ya bajeti hiyo.
Alisema jumla ya Sh trilioni 10.595 zilitolewa katika eneo la matumizi ya kawaida, linalojumuisha mishahara na malipo ya deni la taifa wakati jumla ya Sh trilioni 2.557 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Dk Mpango alisema hadi kufikia Februari mwaka huu, deni la taifa linalojumuisha Serikali na sekta binafsi, lilifikia dola za Marekani milioni 19.9 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 19.6 kwa kipindi kinachoishia Juni mwaka jana.
Alisema kati ya kiasi hicho, dola za Marekani milioni 17.5 zilikuwa ni deni la Serikali na dola za Marekani milioni 2.3 ni deni la sekta binafsi hivyo deni la Serikali liliongezeka kwa asilimia nne.
Aliyataja mafanikio ya bajeti hiyo kuwa ni kuendelea kukua kwa uchumi kwa asilimia saba, kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya ndani hadi kufikia asilimia 99 ya lengo, kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei na kufikia asilimia 5.6 na kutia kwa wakati fedha za miradi ya maendeleo yenye vyanzo mahsusi kama vile mfuko wa barabara, wakala wa nishati, mfuko wa maji na reli.
Mafanikio mengine ni kuendelea kujenga miundombinu katika sekta za nishati, barabara, mawasiliano na uchukuzi, kufanikisha uchaguzi mkuu mwaka jana kwa kutumia fedha za ndani, kupunguza malimbikizo ya madai ya watumishi, wazabuni na wakandarasi na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo waliohakikiwa.
Waziri Mpango alisema katika mwaka ujao wa fedha Serikali imelenga kuhakikisha kuwa pato halisi la taifa linakua kwa asilimia 7.2 kutoka asilimia saba, kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei, ukusanyaji wa mapato ya ndani na halmashauri kuongezeka na kufikia asilimia 14.8 na mapato ya kodi kufikia asilimia 12.6.
Aidha alisema pia Serikali inatarajia kuongeza matumizi kutoka asilimia 23.9 ya pato la taifa hadi kufikia asilimia 27 na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
“Katika Serikali ya awamu ya tano tunatarajia mapato ya Serikali yataongezeka na kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ambayo imekuwa haitabiriki kwa siku za karibuni,” alisisitiza.
Alisema katika mwaka ujao wa fedha Serikali itasimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria ya bajeti na maelekezo ya viongozi wa juu wa Serikali, lengo likiwa ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma.
Alisema ili kufanikisha azma hiyo, Serikali imepanga kuwianisha matumizi na mapato halisi yatakayopatikana kwa kila mwezi, kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya Serikali ili yatumike kama ilivyokusudiwa, kusimamia maagizo yaliyotolewa na Serikali kama ununuzi wa samani na magari, kuziunganisha halmashauri zote katika mfumo wa malipo ya kibenki.

vichwa vya magazeti ya leo tar 07/04/2016











Jumatano, 6 Aprili 2016

MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA WA IRINGA AFARIKI KWA AJALI .


TANZIA.!
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa Ndg.Sinkala Mwenda amepata ajali jioni ya leo eneo la Tanangozi na kukimbizwa Hospitalini kwa ajili ya matibabu. Lakini amefariki dunia muda mfupi uliopita wakati madaktari wakijitahidi kuokoa uhai wake. Pumzika kwa amani Kamanda Sinkara.!


 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiURS8unHWqPLjZ7lS8VqDGY7D2FC8WTe3ZeZc4uFUDAy0R4IGJYQ_23W2JrVw1UBD1C67dZXYkU2Sx3k7kpLpA4eVYocaUcTsVpBy19HJZT2r-DF4HV-R1YyDDjVLuTbHxgl8YXLuCRIo/s640/jamiiforums-20160405-0003.jpg

Kocha: Yanga imenoga Pemba

Imeandikwa na Mohamed Akida na Grace Mkojera BAADA ya kuanza kambi ya `nguvu’ kisiwani Pemba, Yanga imetamba ina uhakika wa kupata ushindi mnono Jumamosi wiki hii itakapokutana na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Kwanza wa Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema vijana wake wameiva vya kutosha na ana matumaini makubwa ya kupata ushindi mnono.
Alisema kwa namna ambavyo wachezaji wake wanavyotimiza majukumu yao vizuri kwenye mazoezi Uwanja wa Gombani, ana uhakika ushindi lazima na mashabiki wasiwe na hofu.
“Nafarijika kuona vijana wangu wakitimiza kikamilifu majukumu yao katika mazoezi ambayo tunawapa, kila mchezaji amekuwa akionesha bidii kwa anachotakiwa kufanya, jambo hili linatupa matumaini na kuamini tuna uwezo wa kushinda ingawa ni vigumu kutabiri idadi ya mabao, lakini yatakuwa ya kutosha,” alisema Mwambusi.
Kocha huyo ambaye anamsaidia Mholanzi Hans Pluijm, alisema katika siku tatu zilizobaki kabla ya mchezo huo wamepanga kuwafundisha wachezaji vitu vichache ambavyo ni muhimu vitakavyowapatia matokeo mazuri.
Alisema wanaelekea kwenye mchezo huo wakiwa na furaha baada ya idadi kubwa ya wachezaji wao kuwa fiti kwa ajili ya pambano hilo isipokuwa kiungo Haruna Niyonzima ambaye hatacheza kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.
“Ukimtoa Niyonzima, wachezaji wengine wote wapo katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo huo, akiwemo Juma Abdul na Nadir Haroub `Cannavaro’…,” alisema Mwambusi na kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumamosi kuwashangilia wakiwa na imani kwamba hawatawaangusha.
Alisema wanataka kushinda ili watakaporudiana ugenini mambo yasiwe magumu zaidi na kusisitiza kuwa ushindi ni lazima kwa mchezo wao.
Zitarudiana wiki ijayo huko Misri. Yanga ilifikia hatua ya raundi ya pili baada ya kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius katika mchezo wa raundi ya awali kwa jumla ya mabao 3-0 na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.
Lakini jana Pluijm (pichani) alikaririwa akisema ushindi katika mchezo huo utategemea na namna wachezaji watakavyojituma na kucheza kama wanavyoelekezwa kutokana na siku za karibuni washambuliaji wake kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini wanashindwa kuzitumia.

UPINZANI WAPEWA NAFASI ZANZIBAR


RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameteua wanasiasa saba kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwamo watatu waliowania Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.
Hao ni aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais wa chama cha ADC, Hamad Rashid Mohammed, Said Soud Said aliyewania nafasi ya urais kupitia AFP Wakulima na Juma Ali Khatib wa ADA-TADEA.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, wengine walioteuliwa ni Balozi Ali Karume, Waziri wa zamani wa Fedha na Uchumi katika Serikali ya Rais mstaafu Dk Salmin Amour, Balozi Amina Salum Ali pamoja na Mohamed Aboud Mohamed aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Pia yumo Mouldine Castico ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi, Rais Shein aliahidi kuunda serikali itakayovishirikisha vyama vya siasa kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi wote bila ya kujali itikadi za kisiasa.

Rais Magufuli ziarani Rwanda leo

maguuli 
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli leo anatarajia kuondoka nchini kuelekea Rwanda, ikiwa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aapishwe kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ilieleza kuwa katika ziara hiyo Rais Magufuli na mwenyeji wake Rais Paul Kagame wanatarajia kufungua daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha pamoja cha ukusanyaji ushuru mpakani, ambacho ni moja ya miradi muhimu iliyoanzishwa kwa hisani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Miundombinu hiyo ambayo ipo katika mpaka wa Tanzania-Rwanda, ni muhimu si tu katika kurahisisha mchangamano baina ya nchi hizi mbili, bali pia kuunganisha zaidi ardhi zisizo na bahari katika mataifa ya Afrika Mashariki na Kati na Bahari ya Hindi.
Baada ya sherehe ya ufunguzi, viongozi hao wawili wataelekea mjini Kigali, ambako watafanya mazungumzo pamoja na kuweka shada la maua kuadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Kama mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ziara ya kwanza ya kigeni ya Rais Magufuli katika eneo hilo pia inaashiria dhamira yake ya kupanua mchakato wa uchangamano na kuimarisha uhusiano baina ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Rais Magufuli ambaye staili yake ya kubana matumizi na vita dhidi ya ufisadi, maarufu kama ‘utumbuaji majipu’ imeteka vyombo vya habari duniani, ataanza ziara hiyo ya siku mbili kwa kufungua kituo cha mpakani cha Rusumo.
Baada ya ufunguzi wa kituo hicho cha pamoja cha ukusanyaji ushuru, ambacho kinaunganisha mataifa haya mawili jirani, atafanya mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Rais Kagame.
Katika siku yake ya pili ya ziara hiyo ya kikazi kesho, Rais Magufuli ataungana na Wanyarwanda kote duniani kuadhimisha miaka 22 ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Siku hiyo ambayo Wanyarandwa huomboleza vifo vya watu zaidi ya milioni moja vilivyotokea mwaka 1994, wengi wao wakiwa Watutsi, Rais Magufuli na mwenyeji wake Kagame pamoja na wake zao wataweka mashada ya maua na kuwasha mishumaa ya kumbukumbu.
Baada ya tukio hilo, Dk. Magufuli ataungana na Wanyarwanda katika matembezi yajulikanayo kama ‘Walk to Remember’ maalumu kwa kumbukumbu ya mauaji hayo na kuwasaidia walionusurika kabla ya kuhudhuria mkesha kwenye Uwanja wa Taifa wa Amahoro mjini Kigali.
Rais Magufuli amekuwa akitumia muda mwingi akiwa Ikulu Dar es Salaam kwa shughuli za utendaji kazi kwa Serikali yake na alisafiri mara chache nje ya jiji hilo kwenda mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza, Morogoro, Singida na Geita.

Jumanne, 5 Aprili 2016

Mamlaka ya mji mdogo ILULA na idara ya afya vinara kwa rushwa IRINGA 2015/2016

kikoti blog
WAFAMASIA wawili, mmoja wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na mwingine wa hospitali ya wilaya ya Mufindi pamoja na watuhumiwa wengine wawili waliokuwa viongozi wa kijiji cha Ilula Mwaya wilayani Kilolo wamefikishwa mahakamani kati ya Januari na Machi mwaka huu wakituhumia kwa makosa mbalimbali ya rushwa.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi ya kipindi hicho, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa, Eunice Mmari alisema watuhumiwa hao wanne wamefikishwa mahakamani kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Aliwataja wafamasia hao kuwa ni Lucas Mwandi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na Selemani Fulano wa hospitali ya wilaya ya Mufindi, na Deogratias Vangiliasas aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Ilula Mwaya na Robert Kisaka aliyekuwa afisa mtendaji wa kijijiji hicho.
Azungumza na wanahabari ofisini kwake jana, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa, Eunice Mmari alisema wafamasia hao wanashitakiwa kupitia kesi namba 53/2016 na kesi namba 39/2016 kwa makosa ya wizi wa mali ya umma wakiwa mtumishi wa umma kinyume na kifungu cha 270 cha sheria ya kanuni ya adhabu iliyorekebishwa mwaka 2002.
Kuhusu waliokuwa viongozi wa kijiji hicho, alisema nao wanashitakiwa kwa makosa ya wizi wa mali za umma kupitia kesi namba 23/2016, kinyume na sheria hiyo ya rushwa kifungu namba 28, 29, 30 na 31.
Mmari alisema katika kipindi hicho cha Januari hadi Machi, Takukuru pia imepokea malalamiko 28 ya rushwa na 14 kati yake yamefunguliwa majadala ya uchunguzi, malalamiko tisa yanafanyiwa uchunguzi wa awali, huku malalamiko matano yakifungwa baada ya kukosekana kwa ushahidi.
Alikitoa mchanganuo wa mamalamiko hayo alisema afya iliongoza kwa kuwa na malalamiko saba, serikali za mitaa, vijiji na kata (6), elimu (3), ardhi (2), sekta binafsi (1), Tanroads (1), Ushirika na Kilimo (2), Polisi (1), Ujenzi (1) na sekta binafsi (2).
Akizungumzia mwamko wa wakazi wa mkoa wa Iringa kuyaripoti matukio ya rushwa katika taasisi yao, Mmari alisema; “mwamko ni mdogo sana ikilinganishwa na mikoa mingine.”
Alisema Takukuru inaamini kuwepo kwa makosa mengi yanayoangukia katika sheria ya rushwa lakini yemekuwa hayaripotiwi katika taasisi yao jambo linalowaathiri wananchi wenyewe na uchumi wa Taifa.
Aliwataka wananchi hao kutoa taarifa kwao wakati wowote wanapokosa huduma baada ya kudaiwa rushwa au pale wanapobaini miradi ya maendeleo katika maeneo yanayowazunguka inafanywa chini ya kiwango.
Kwa kupitia elimu kwa umma, Mmari alisema wananchi 4,957 wamepatiwa elimu ya rushwa katika kipindi hicho, wakiwemo wanafunzi 3,693.
Alisema ofisi yao pia imefanya vikao vinne vya kujadili dhibiti zilizofanyika ili kuziba mianya ya rushwa katika usimamizi wa mali za vijiji, zabuni ya ununuzi wa pampu ya kusukuma maji katika mji wa Mafinga, ajira za vibarua katika mamlaka ya maji Mafinga na taratibu za kuchukua walimu wa kujitolea shule za msingi za mjini Iringa.