Imeandikwa na Vicky Kimaro
KIMAHESABU Yanga tayari ni bingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara
msimu wa 2015/2016, labda itokee miujiza ya kupoteza mechi zake zote
tatu zilizosalia katika ligi hiyo, huku mahasimu wao Simba wakishinda
mechi zote nne walizobakiwa nazo.
Lakini sare au kipigo kimoja tu kwa Simba kitaihakikishia Yanga taji
la 26 katika ligi hiyo iliyoingia katika msimu wa 51 tangu kuanzishwa
kwake mwaka 1965.
Hii ina maana kwamba, mbio za ubingwa kwa sasa zimebaki kwa Yanga na
Simba tu, baada ya jana Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuipoka Azam FC
pointi tatu na mabao matatu, hivyo kuirudisha kutoka nafasi ya pili hadi
ya tatu ikiwa na pointi 57.
Na hata kama ikishinda mechi tatu zilizosalia, itakuwa na jeuri ya
kufikisha pointi 66 ambazo zimeshavukwa na Yanga yenye pointi 68.
Simba ina pointi 58 na ikishinda zote nne itakuwa na uwezo wa
kufikisha pointi 70, lakini wakati huohuo ikiomba Yanga ipoteze mechi
zake zote tatu ili ubingwa huo utue Mtaa wa Msimbazi kwa mara ya kwanza
tangu msimu wa 2011/2012.
Keshokutwa, Simba itacheza na Mwadui FC Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, hivyo sare au kipigo kitapeleka chereko kwa Yanga, kwani huenda
wakatangazwa mabingwa bila hata kugusa mpira katika siku husika.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas
alithibitisha jana kuwa, Azam imepokonywa pointi tatu na mabao matatu na
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kosa la kumchezesha beki wake mahiri
Erasto Nyoni akiwa na kadi tatu za njano katika mchezo dhidi ya Mbeya
City mjini Mbeya.
“Azam wanatakiwa kutunza kumbukumbu za wachezaji wao, bodi imefikia
uamuzi wa kuipokonya pointi tatu Azam FC baada ya kubaini ilimtumia
Erasto Nyoni kinyume cha sheria,” alisema Lucas.
Katika mchezo huo, Azam ilishinda 3-0.
Kwa mujibu wa kanuni ya 37 (4) toleo la 2015 ya Ligi Kuu ya Tanzania
Bara juu ya udhibiti wa wachezaji; “mchezaji atakayeonywa kwa kadi tatu
za njano katika michezo mitatu, basi atalazimika kukosa mchezo unaofuata
wa timu yake.”
Aidha kanuni ya 14 (37) ya kanuni hiyo imempa ushindi wa mabao matatu na magoli matatu timu ya Mbeya City.
Kutokana na adhabu hiyo kwa Azam, ni wazi Yanga sasa imebakiza mechi
moja kutwaa ubingwa msimu huu na huenda ikatangaza ufalme Jumanne ijayo
mjini Mbeya itakayokwenda kupambana na Mbeya City. Ikishinda, itafikisha
pointi 71 ambazo hazitafikiwa na Simba.
Msemaji wa Azam, Jaffari Maganga akizungumzia adhabu hiyo, alisema;
“Tumesikia taarifa tu bado hatujapata barua rasmi ya kutujulisha
kupokonywa pointi, tutakapoipata tutalizungumzia suala hili.”
Adhabu ya aina hii imewahi kuikumba Simba 2006 na 2007 na pia Yanga
mwaka 2012 huku ligi ikielekea ukingoni. Ilivyokuwa; Mwaka 2006 Simba
ilinyang’anywa pointi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar,
baada ya kudaiwa kumchezesha Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyekuwa na kadi tatu
za njano.
Mwaka 2007 Simba ikakutana tena na adha kama hiyo ikiwa imebakiza
michezo minne mkononi kwa kupokwa pointi tatu na mabao matatu na ushindi
kupewa Azam FC baada ya kumchezesha Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa na
kadi tatu za njano.
Mwaka 2012 Coastal Union ilinufaika kwa kupewa ushindi wa chee wa
pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha mchezaji Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Machi 31
mwaka huo Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.