Imeandikwa na John Nditi, Morogoro
WATUHUMIWA sita kati ya 11 wa udhalilishaji, ubakaji na usambazaji wa
picha za video, zikimwonesha msichana mwenye umri wa miaka 21,
akilazimishwa kufanya mapenzi eneo la Dakawa, Morogoro wamepandishwa
kizimbani. Imebainika kuwa miongoni mwa makosa yanayowakabili, lipo pia
la kulawiti.
Mamia ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro walifurika katika jana katika
viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, kushuhudia
watuhumiwa hao wakipandishwa kizimbani. Watuhumiwa hao walifikishwa
mahakamani hapo na walisomewa mashitaka yao na mahakimu wawili tofauti
katika vyumba vya mahakama hiyo.
Wawili katika watuhumiwa hao, wanakabiliwa na shitaka la kubaka ,
kulawiti na kupiga picha za video za kujamiiana na kuzisambaza kwenye
mitandao ya kijamii. Walioshitakiwa kwa kosa kumlawiti na kumbaka
msichana huyo kisha kupiga picha za video wakati wakifanya tendo la
kujamiiana kwa lengo la kuzisambaza picha hizo kwenye mitandao ya
kijamii, ni Idd Adamu (32) mkazi wa Makambako, mkoani Iringa na Zuberi
Thabiti (30) mkazi wa Mbalali, mkoani Mbeya.
Ulinzi katika viwanja vya mahakama hiyo, uliimarishwa huku wananchi
na waandishi wa habari, wakizuiwa kuingia kusikiliza kesi hiyo ikisomwa
ndani ya mahakama. Hali hiyo ilielezwa na uongozi wa mahakama kuwa
inatokana na matakwa ya sheria ya makosa ya ubakaji na ulawiti, kuzuia
kesi hiyo kusomwa hadharani.
Watu walijaa kila kona na ilielezwa kuwa kesi hiyo ni ya aina yake,
kutokana na kugusa hisia za wengi. Baadhi ya watu nje ya mahakama,
walionekana wakilia na miongoni mwao walidai wanamuonea huruma msichana
aliyetendewa unyama huo, kwani baadhi ya wahusika waliosambaza picha
hizo mitandaoni, wana undugu na msichana huyo.
Akisoma shtaka linalowakabiliwa watuhumiwa wawili wa makosa ya
ubakaji, ulawiti na kupiga picha za video wakati wakifanya tendo la
kujamiiana kwa lengo la kuzisambaza picha hizo kwenye mitandao ya
kijamii, Wakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mkoa, Mary Moyo, alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja
walitenda kosa hilo Aprili 27, mwaka huu.
Alidai watuhumiwa walitenda kosa hilo Aprili 27 , mwaka huu majira ya
jioni katika nyumba ya kulala wageni iliyofahamika kwa jina la Titii
iliyopo Dakawa wilayani Mvomero. Aidha, watuhumiwa hao wawili
waliunganishwa na watuhumiwa wengine wanne waliofikishwa mbele ya Hakimu
Mkazi wa Mahakama hiyo, Ivan Msack kwa kosa la kusambaza picha za video
za kujamiiana kwenye mitandao ya kijamii, ikiwamo ‘WhatsApp’, jambo
ambalo ni kosa chini ya Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015
Kifungu Namba 14 (1b) na (2b).
Washtakiwa hao ni Rajabu Salehe (30), Ramadhan Ally (26), Musini Ngai
(36) na John Peter (26), wote wakiwa ni wakazi wa Dakawa Wilaya ya
Mvomero mkoani Morogoro. Alidi kuwa washitakiwa hao wote kwa pamoja,
walitenda kosa hilo katika nyakati tofauti kati ya Aprili 28 hadi 30,
mwaka huu, ambapo walisambaza picha hizo huku wakijua kufanya hivyo ni
kosa kisheria.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, ambapo wote walikana, upande wa
mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila, Edga
Bantulaki na Calstus Kapinga, uliwasilisha mahakamani hapo hati ya zuio
la dhamana kwa washtakiwa hao.
Katika hati hiyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa endapo washtakiwa
hao watakuwa nje kwa dhamana, wataharibu upelelezi wa kesi hiyo na pia
kutahatarisha usalama wa mlalamikaji na washtakiwa hao, kutokana na kesi
hiyo kuvuta hisia za watu wengi.
Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni Mosi mwaka huu, itakapotajwa
tena na kusikiliza suala la dhamana, kufuatia maamuzi ya maombi hayo ya
pande mbili. Washitakiwa wote sita walirudishwa rumande.
Wakati kesi ikiendelea mahakamani hapo baadhi ya watu waliokuwemo
waliangua kilio huku baadhi yao walisikika wakidai kuwa baadhi ya
washitakiwa waliosambaza picha wanauhusiano wa kindugu na binti huyo.
Katika hatua nyingine, kabla ya kufikishwa watuhumiwa hao mahakamani,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alikutana na
waandishi wa habari na alisema kuwa kati ya watuhumiwa 11 waliokuwa
wamekamatwa, sita upelelezi wake ulikamilika. Alisema watuhumiwa wengine
watano, upelelezi unaendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani.
TANGAZO
NEW MWALIMU EDUCATION CENTRE
Mahali:
Ilula madizini katika majengo ya kanisa katoriki kigango cha madizini
karibu na soko la TASAF.
Inawatangazia
kuwa inaendelea na utoaji wa huduma (tuition) kuanzia kidato cha kwanza
mpaka cha sita: tuition hii ni mahususi kwaajili ya likizo ya
mwezi wa sita itaanza usajiri wake kuanzia tarehe 30/05/2016.
Ada ni
shilingi Elfu kumi(10,000) kwa muda wote wa likizo
- kwa wanafunzi wa kidato cha
nne(form 4) tutafanya
solving ya past paper na maswali mbalimbali
pia mwanafunzi
atapewa peni bure na notes zilizo andaliwa na walimu mahili mara tu baada ya kufanya usajiri. Nyote mnakaribisha kwa mawasiliano
piga simu no +255769694963 au +255784428256.